![]() |
|
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
|
Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
ikiongozwa na Mwenyekiti wa Chama, Mheshimiwa Freeman Mbowe, inakutana leo tarehe
9/9/2012 katika kikao cha dharura, kujadili hali ya siasa nchini, kufuatia
mfululizo wa matukio ya mauaji yanayofanywa na Jeshi la Polisi kwenye shughuli
halali (kwa mujibu wa katiba ya nchi) za chama na njama za CCM na baadhi ya
viongozi wa Serikali kudhibiti Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) kwa mbinu haramu.
Itakumbukwa hivi karibuni baada ya
mauaji ya Ndugu Ali Singano (Zona) mjini Morogoro, yaliyosababishwa na Jeshi la
Polisi mkoani humo wakati walipoingilia kwa nia ya kuvuruga mapokezi na mkutano
wa CHADEMA, chama kilitoa kauli kumtaka Rais Jakaya Kikwete aagize kutumika kwa
Sheria ya Uchunguzi wa Vifo (Inquest Act) ili kubaini chanzo na kuondoa utata
wa kifo cha kijana huyo.
Hivi karibuni, baada ya mauaji ya
mwandishi wa habari wa Channel Ten na Magic FM, Ndugu Daudi Mwangosi, CHADEMA
kilitoa tamko kumtaka Rais Kikwete, aagize kufanyika uchunguzi huru kupitia
tume ya kimahakama. Kwani katika tukio hilo hakukuwa na utata kuwa mwandishi
huyo aliuwawa na polisi.
Hivyo uchunguzi huru ulihitajika ili kubaini
vitu vya ziada, kama vile kwa nini kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa katiba, haki
za binadamu na sheria za nchi na nani alitoa amri za mauaji hayo.
Itakumbukwa pia kuwa CHADEMA
kilipinga kuundwa kwa kamati ya kuchunguza tukio la kuuwawa kwa Mwangosi,
iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi, kwa sababu iliundwa
kinyume cha sheria ya tume za uchunguzi, ikiwa na lengo la kufunika mambo na
kurejesha uhusiano wa serikali na vyombo vya habari, badala ya kutafuta ukweli.
Kwa mara nyingine tena kilimtaka Rais Kikwete
aunde tume huru ya uchunguzi kwa mujibu wa sheria ili kweli tupu ijulikane.
Wakati chama kikitangaza kuahirisha
kwa muda mikutano ya Operesheni Sangara-Vuguvugu la Mabadiliko (M4C), mjini
Iringa, kilisisitiza kauli yake ya kumtaka Rais Kikwete kuingilia kati
kuhakikisha analinda katiba ya nchi inayotambua haki ya kuishi, kwa kuagiza
uchunguzi huru ufanyike ili kubaini ukweli wa tukio hilo na kuzuia hali hii ya
vyombo vya dola kufanya mauaji ikiwa na lengo la kutisha wapinzani na wakosoaji
wa serikali ya CCM.
Kutokana na ukimya wa Rais Kikwete
katika matukio hayo na mengine ya namna hiyo ambapo raia wasiokuwa na hatia
wametekwa, kuteswa na kuuwawa na vyombo vya dola au wakiwa mikononi mwa vyombo
hivyo, CHADEMA kimeitisha kikao cha dharura cha Kamati Kuu kujadili hali hii,
kisha kufanya maamuzi ya hatua zaidi za kuchukua dhidi ya Jeshi la Polisi na
Serikali inayoongozwa na CCM, kwa manufaa ya taifa letu na Watanzania wote kwa
ujumla.
Imetolewa 8 Septemba, 2012
Na:Tumaini
Makene,
Ofisa
Habari wa CHADEMA;
Kurugenzi
ya Habari na Uenezi;
Makao
Makuu ya CHADEMA, Dar es Salaam.







No comments:
Post a Comment