Shirika la
Global Fund limetoa ufadhili wa dola za Marekani 525 milioni sawa na Sh 1.1
trilioni kwa Serikali ya Tanzania kwa ajili ya kusaidia mapambano dhidi
ya malaria, kifua kikuu na Ukimwi kati ya mwaka 2018 na 2020.
Kati ya
fedha hizo, Sh 67 bilioni zimetengwa kwa ajili ya kifua kikuu zikihusisha elimu
kwa wanajamii, vipimo na dawa kwa watu ambao watabainika kuwa na
ugonjwa huo.
Hatua hiyo
inalenga kufikia dhamira ya Serikali ya kuwapa matibabu asilimia 70 ya
wagonjwa wote wa kifua kikuu ifikapo mwaka 2020.
Kuhusu
malaria Sh320 bilioni zimetengwa kwa ununuzi wa vyandarua, vipimo (mRDTs) na
dawa za kutibu ugonjwa huo.
Kwa mapambano
dhidi ya Ukimwi zimetengwa Sh769 bilioni kiasi ambacho Waziri wa Afya, Ummy
Mwalimu amekitaja kuwa ni kikubwa kuwahi kutolewa na shirika hilo kwa ugonjwa
huo.
Akizungumza
leo Jumatatu Januari 29,2018 wakati wa utiaji saini makubaliano ya ufadhili
huo, Ummy amesema Serikali inatambua na kuthamini kazi inayofanywa na wadau wa
masuala ya afya.
Waziri Ummy
amemhakikishia mwakilishi wa shirika hilo kuwa, Serikali itaongeza
usimamizi katika fedha zinazotolewa na wafadhili kuhakikisha zinatumika kama
ilivyokusudiwa.
“Rais
mwenyewe ameniambia kuwa fedha hizi ni nyingi, hivyo tufanye kila
linalowezekana kuhakikisha zinatumika kama ilivyoelekezwa, nami naahidi
nitazifuatilia kuona zinafanya kazi iliyopangwa,” amesema.
Mwakilishi
wa Global Fund nchini, Linden Morris amesema shirika hilo litaendelea kusaidia
mapambano dhidi ya maradhi hayo.
Morris
amesisitiza wasimamizi wa fedha hizo kuhakikisha zinafanya kazi iliyokusudiwa.
|
No comments:
Post a Comment