|
Katibu Mkuu
wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James (kulia) na akimweleza jambo
Kamishna wa Ushirikiano wa Kimataifa na Maendeleo wa Umoja wa Ulaya Mr. Neven
Mimica wakati wa hafla fupi ya Umoja wa Ulaya (EU) kutiliana saini makubaliano
ya msaada wa Euro milioni 50 kwa ajili ya kusaidia usambazi wa umeme vijijini
kupitia Mradi Kabambe wa Kusambaza umeme Vijijini (REA).
|
|
Katibu Mkuu
wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James akiwa pamoja na Kamishna wa
Ushirikiano wa Kimataifa na Maendeleo wa Umoja wa Ulaya Bw. Neven Mimica
wakisaini Mkataba wa msaada wa fedha za kusaidia usambazaji wa umeme
Vijijini (EURO milioni 50) katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango,
Jijini Dar es Salaam.
|
|
Katibu Mkuu
wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James na Kamishna wa Ushirikiano wa
Kimataifa na Maendeleo wa Umoja wa Ulaya Mr. Neven Mimica, wakibadilishana hati
za makubaliano ya msaada wa ruzuku ya kiasi cha EURO Milioni 50 katika ukumbi
wa wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es Salaam.
|
|
Katibu Mkuu
wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James akiagana na Kamishna wa
Ushirikiano wa Kimataifa na Maendeleo wa Umoja wa Ulaya Bw. Neven Mimica, baada
ya kusaini mkataba wa msaada wa Euro milioni 50 ambazo Umoja huo umeipatia
Tanzania kwa ajili ya kusambaza umeme vijijini kupitia Wakala wa Umeme Vijijini
REA.
(Picha na
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)
Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
TANZANIA imezidi kupata neema kutoka Jumuiya ya
Kimataifa ambapo Novemba 2, 2017, Umoja wa Ulaya (EU) umeipatia Tanzania msaada
wa Euro milioni 50, takriban Shilingi bilioni 130 kwa ajili ya kufadhili Mradi
Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini unaoendeshwa na Wakala wa Nishati Vijijini
(REA).
Mkataba wa Makubaliano hayo umetiwa saini Jijini Dar
es Salaam kati ya Katibu Mkuu na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Wizara ya Fedha na
Mipango, Bw. Doto James na Kamishna wa Ushirikiano wa Kimataifa na Maendeleo wa
Umoja wa Ulaya (EU) Bw. Neven Mimica.
Msaada huo umelenga kuwasaidia raia wa Tanzania
kufikiwa na huduma nafuu ya nishati ya umeme kwa kupanua uwezo wa gridi ya
Taifa pamoja na mtandao wa usambazaji umeme.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto
James ameushukuru Umoja wa Ulaya kwa msaada huo mkubwa utakaoiwezesha nchi kuwa
na umeme wa uhakika utakaochangia ukuaji wa uchumi wa nchi na maendeleo ya watu
wake.
“Umoja wa ulaya ni wadau wetu muhimu wa maendeleo
kutokana na misaada muhimu na mikubwa wanayotupatia, na kusadia agenda yetu ya
maendeleo” alisema Bw. James
Alisema kuwa kiasi cha msaada wa Euro milioni 50
kilichotolewa na Umoja huo bila masharti yoyote si kidogo, na kwamba kitasaidia
kutatua changamoto ya upatikanaji wa nishati ya umeme utakaochangia kuimarika
kwa sekta ya viwanda itakayochochea ukuaji wa uchumi wa nchi.
Bw. Doto James alisema kuwa tangu Mradi Kabambe wa
Kusambaza Umeme Vijijini REA uanze miaka 9 iliyopita, idadi ya vijiji
vilivyounganishiwa umeme imeongezeka kutoka vijiji 400 mwaka 2008 hadi kufikia
vijiji 4395 hivi sasa.
Alisema kuwa ni matarajio ya Serikali kwamba ifikapo
mwaka 2020, vijiji vyote 12,000 hapa nchini vitakuwa vimeunganishwa na nishati
hiyo hivyo kuchochea shughuli za uzalishaji viwandani na kiuchumi kwa wananchi,
vitaimarika.
Kwa upande wake, Kamishna wa Ushirikiano wa Kimataifa
na Maendeleo wa Umoja wa Ulaya (EU) Bw. Neven Mimica, amesema kuwa msaada huo
wa Euro milioni 50 wanaoutoa ni sehemu ya msaada wa Euro milioni 207 ambazo
wanachama wengine wa Umoja huo, ikiwemo Sweden, Uingereza, Norway na Benki ya
Dunia, watatoa kufanikisha mradi huo wa usambazaji umeme vijijini kupitia REA.
“Nguvu hizi za pamoja zitaviwezesha takriban vijiji
3,600 vilivyoko maeneo mbalimbali ya nchi ambapo watu zaidi ya milioni 1
wanatarajiwa kunufaika na mradi huo” Alisema Bw. Mimica.
Alisema hatua hiyo itachangia kuimarika kwa ubora wa
maisha ya wananchi wa Tanzania, kuimarika kwa sekta za afya, elimu na kuleta
faida za kijamii na kiuchumi zinazoonekana kwao moja kwa moja hususan wanawake
na watoto.
Misaada ya Umoja wa Ulaya kwa Tanzania imejikita
katika Nyanja tatu za Utawala bora, Umeme na Kilimo endelevu ambapo Umoja huo
kupitia Mfuko wake wa Maendeleo (EDF) umetenga kiasi cha Euro milioni 626
katika kipindi cha kuanzia mwaka 2014-2020.
|





No comments:
Post a Comment