
Watu watano
wanaosadikiwa kuwa majambazi wameuawa kwa kupigwa risasi na polisi waliokuwa
doria.
Taarifa ya
polisi imesema watu hao waliuawa walipojaribu kuwavamia wafanyabiashara wa
madini katika machimbo ya Mwime nje kidogo ya Mji wa Kahama.
Watuhumiwa
pia wanadaiwa kuhusika na mauaji ya viongozi wa Serikali ya Mtaa, polisi na
wanasiasa mkoani Pwani katika wilaya za Kibiti, Rufiji na Mkuranga.
Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Shinyanga, Simon Haule alisema jana kwamba watu hao walijeruhiwa
usiku wa kuamkia jana katika eneo la Mwanva katika Halmashauri ya Mji wa Kahama
walipokabiliana ana kwa ana na polisi waliofika eneo hilo.
Kamanda
Haule alisema baada ya polisi kufika kwenye eneo la tukio, watu hao walijificha
kwenye mashimo yanayotumiwa kuchimba mchanga na kuanza kurushiana risasi na
askari.
Alisema
katika mapambano hayo, watuhumiwa walizidiwa nguvu na kujeruhiwa na walifariki
dunia walipokuwa njiani kupelekwa hospitali.
Alisema
katika eneo la tukio, polisi walikuta bunduki moja aina ya SMG na risasi 25
zilizokuwa kwenye magazini. Pia walikuta mabomu mawili ya kutupa kwa mkono.
Katika
uchunguzi wa awali, Kamanda Haule alidai kwamba watu hao ni miongoni mwa
waliokuwa wakifanya uhalifu mkoani Pwani ambao walikimbia huko baada ya
kudhibitiwa.
Kamanda
Haule aliwataka wananchi kufika katika Hospitali ya Mji wa Kahama kuwatambua
marehemu kauli ambayo pia ilitolewa na Mganga Mkuu wa Mji wa Kahama, Dk David
Lucas.





No comments:
Post a Comment