
Chama
cha Mapinduzi (CCM), kimesema Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana
hajahudhuria vikao vya kamati kuu na halmashauri kuu kwa kuwa aliomba
udhuru wa kihali kwa kuwa anauguza ndugu yake wa karibu wa familia.
"Ndugu
yetu Kinana anauguza ndugu yake wa karibu, tumwombee apone lakini
Kinana alishiriki vyema kikao cha Sekretarieti. Kinana hajajiuzulu au
kuandika barua ya kujiuzulu," amesema Katibu wa Itikadi na Uenezi wa
CCM, Humphrey Polepole.
Chama
hicho pia kimetangaza kuwachukulia hatua kali makada wake
watakaobainika kukiuka utaratibu wa uchaguzi wa ndani wa chama hicho.
Polepole
amesema hayo leo Jumamosi alipozungumza na waandishi wa habari katika
ofisi ndogo za chama hicho Lumumba jijini hapa akitoa taarifa ya vikao
vya juu vilivyoanza juzi Ikulu ya Dar es Salaam. Amesema Mwenyekiti wa
CCM, Rais John Magufuli amesema vikao hivyo vimepitisha majina ya
wagombea wa uenyekiti ngazi ya wilaya.
Amesema
kati ya wilaya 161 za kiserikali ambazo ni sawa na za kichama, kikao
cha Kamati Kuu na Halmashauri Kuu iliyoketi leo Jumamosi imezuia
uchaguzi katika wilaya sita.
Amezitaja
wilaya hizo kuwa Moshi Mjini, Siha, Hai na Makete kwa sababu
waliojitokeza kugombea wameonekana kuwa watu hatarishi kwa chama hicho
na uchaguzi utatangazwa baadaye.
Wilaya za Musoma Mjini na Musoma Vijijini zitarudia baada ya kutenganishwa kutoka wilaya moja na kuwa mbili.
"Chama
hakitasita kuwachukulia hatua kali ikiwemo kufuta uchaguzi au
kuwafukuza uanachama wale wote watakaobainika kutozingatia maadili na
kanuni za chama chetu," amesema Polepole.
Amesema
Halmashauri Kuu imetoa onyo kali kwa wanachama wa Zanzibar walioanza
kampeni za uchaguzi mkuu ikisema muda bado na wakiendelea watachukuliwa
hatua.





No comments:
Post a Comment