![]() |
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Kamishina Jenerali wa
Magereza, Dr Juma Malewa baada ya kikao chake na Maofisa wa Magereza kutoka Makao ya
Magereza kilichofanyika Ofisini kwake mjini Dodoma Februari 13,2017.
Katikati ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo
ya ndani Meja Jenerali Projest Rwegasira.
|
Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya
pamoja na Maofisa wa Jeshi la Magereza
Wanawake baada ya kikao chake na Maofisa wa Magereza kutoka Makao ya
Magereza kilichofanyika Ofisini kwake mjini Dodoma Februari 13,2017. Kulia kwake ni Waziri wa Mambo ya Ndani
ya Nchi, Mwigulu Nchemba.
*Ataka
karakana za ujenzi, useremala zianzishwe kupunguza gharama
*Asisitiza
ufyatuaji matofali kukabili upungufu wa nyumba za askari
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amemuagiza Kamishna Mkuu wa Magereza, Dk. Juma Malewa asimamie
zoezi la upimaji wa maeneo yanayomilikiwa na Magereza kote nchini na
kuhakikisha yanawekewa mipaka.
Ametoa agizo
hilo leo mchana (Jumatatu, Februari 13, 2017) katika kikao baina ya Kamishna
huyo mpya na Maafisa Magereza wa Mikoa yote na maafisa wanaoshughulikia kilimo
na viwanda alichokiitisha ofisini kwake mjini Dodoma.
“Magereza
yetu mengi yako kwenye maeneo ambayo hayajapimwa. Baadhi ya maeneo kuna
migogoro kwa sababu wananchi wamejenga karibu kabisa na maeneo ya Magereza.
Lazima tupime maeneo yote na kuyawekea alama mipakani ili kubainisha maeneo
yetu,” amesisitiza.
Mbali ya
maeneo ya Magereza, Waziri Mkuu amesema, jeshi hilo lina mashamba makubwa ambayo pia hayajapimwa hali ambayo
amesema imechangia baadhi ya wananchi kulima ndani ya maeneo ya jeshi hilo.
“Natambua
kuwa jeshi hili lina mashamba makubwa lakini nayo pia hayajapimwa. Kila RPO ni
mjumbe wa kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wake, tumieni wapima ardhi kutoka
kwenye Halmashauri zenu na mhakikishe kuwa maeneo hayo yanapatiwa hati,”
amesema.
Amesema
umefika wakati sasa kila gereza litambue na kuainisha fursa walizonazo ili
waweze kuamua ni kwa kiasi gani wanaweza kujitegemea kwa uzalishaji. “Kama ni
kilimo, ufugaji, au uzalishaji wa umeme, tuangalie ni kipi kinaweza kuvutia
uwekezaji, lakini cha msingi zaidi ni lazima tuwe na hati za maeneo
tuliyonayo,” amesema.
Waziri Mkuu
amesema kuna baadhi ya magereza yalikuwa maarufu kwa kilimo lakini hivi sasa
hakuna hata moja lenye trekta na kama yapo ni moja au mawili tu. “Sasa hivi
teknolojia ya kilimo imebadilika, ni lazima tutumie zana za kilimo ili kwenda
na kilimo cha kisasa.
Akizungumzia
kuhusu ufugaji na uvuvi wa samaki, Waziri Mkuu aliagiza jeshi hilo litumie
maafisa wake waliobobea kwenye sekta hizo, watumike kuendeleza na kuhamisha
ujuzi wao kwa wafungwa wanaotumikia vifungo ili wanapotoka gerezani, wawe na
ujuzi ambao utawasaidia kujikimu kimaisha wanaporudi kuishi vijijini.
“Nimetembelea
maonesho ya Nanenane na Sabasaba huko nimekuta wamejenga banda la kuku juu ya
bwawa la samaki. Hii ina maana kuku wanakula na kinyesi chao kinakuwa ni
chakula kwa wale samaki walioko bwawani,” amesema.
Amemtaka Dk.
Malewa aangalie uwezekano wa kuanzisha karakana na ujenzi kwenye kila gereza
ili maafisa na wafungwa waliopo kule watumike kufanya kazi kwenye karakana
hizo.
“Nimetembelea gereza la Isanga, nikakuta kuna milango haina komeo. Kwa
vile hakuna karakana, inabidi atafutwe fundi kutoka mtaani ili aje kutengeneza
kitasa au komeo. Tuanzishe karakana na tuziboreshe,” amesisitiza.
Amesema
uwepo wa karakana hizo ziwe ni za umeme, ujenzi au useremala, utasaidia
kupunguza gharama za uendeshaji kwa jeshi la magereza kwa matengenezo madogo
madogo yatafanywa na watu wa kwenye karakana badala ya kutumia watu wa nje.
Amesema ili
kukabiliana na tatizo la uhaba wa nyumba za askari, kila afisa magareza wa mkoa
hana budi kuandaa matofali ya kutoka kwani timu za wafyatuaji wanazo na
nguvukazi wanayo pia.
“Badala ya
kutegemea wazabuni, kule kwenye udongo mzuri, tafuteni vifaa mfyatue matofali
ya hydraform. Kule kwenye mchanga, fyatueni ya saruji. Kuweni na matofali ya kutosha kulingana na mahitaji
yenu, mtakuwa mmepunguza gharama za ujenzi wa nyumba za askari kwa kiasi
kikubwa,” amesisitiza.
Kwa upande
wake, Kamishna Mkuu huyo, Dk. Malewa amesema atafuatilia suala la upimaji wa maeneo ya magereza kwa sababu
wanao wapimaji na vifaa wanavyo. Amesema kuna magareza 11 yenye migogoro ya
maeneo na wananchi.
“Pia
tutafuatilia upimaji wa maeneo ya mashamba ya magereza. Tumeanzisha mashamba
makubwa ya kilimo na tutahakikisha maeneo hayo yote yanapimwa na kuwekewa alama
za mipaka,” amesema.
Kikao hicho
kilihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Bw. Mwigulu Nchemba; Naibu
Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Bw. William Tate Ole Nasha; Kamishna
Jenerali wa Magereza, Makatibu Wakuu wa Wizara ya Kilimo wanaoshughulikia
Kilimo na Mifugo pamoja na Katibu Mkuu wa Mambo ya Ndani.
IMETOLEWA
NA:
OFISI YA
WAZIRI MKUU,
S. L. P.
980,
DODOMA.
JUMATATU,
FEBRUARI 13, 2017.
|
No comments:
Post a Comment