Rais wa
Jamhuri ya Uturuki, Mheshimiwa Recep Tayyip Erdogan anatarajiwa kufanya ziara
ya kitaifa ya siku mbili nchini tarehe 22 na 23 Januari 2017 kwa mwaliko wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli.
Mhe. Rais
Erdogan ambaye ataambatana na Mkewe, na kuongoza ujumbe wa watu 150 wakiwemo
Mawaziri, Wabunge, Maafisa kutoka Serikalini na Wafanyabiashara anatarajiwa
kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere tarehe 22
Januari, 2017 jioni na atapokelewa na
Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Madhumuni ya
ziara hiyo ni kukuza mahusiano mazuri yaliyopo baina ya Uturuki na Tanzania
pamoja na kupanua fursa za uwekezaji hususan katika maeneo ya biashara na uwekezaji.
Wakati wa
ziara hiyo, Mhe. Erdogan atakutana na
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli
kwa mazungumzo ya faragha yatakayofuatiwa
na mazungumzo rasmi yatakayowahusisha wajumbe wa pande mbili na baadaye
Marais hao watashuhudia uwekwaji saini wa mikataba ya ushirikiano kwenye maeneo
mbalimbali.
Siku hiyo ya
tarehe 23 Januari, 2017, kutakuwa na Kongamano la Biashara kati ya Uturuki na
Tanzania litakalowakutanisha Wafanyabiashara kutoka nchi hizi mbili. Kongamano
hilolitahutubiwa na viongozi wa Tanzania na Uturuki.
Mhe. Rais
Erdogan na ujumbe wake watashiriki Dhifa ya Chakula cha jioni kilichoandaliwa
Ikulu kwa heshima yake na Mhe. Rais Magufuli.
Mahusiano ya Uturuki na Tanzania.
Mahusiano ya
Tanzania na Uturuki ni mazuri. Ikumbukwe kuwa, kufunguliwa kwa mara nyingine
kwa Ubalozi wa Uturuki hapa nchini mnamo Mei 2009 kuliongeza kasi ya mahusiano
baina ya nchi hizi mbili.
Tangu kipindi
hicho kumekuwa na ziara za viongozi wa kitaifa wa nchi hizi mbili ili kukuza na
kudumisha mahusiano. Katika hatua nyingine Tanzania imetangaza kufungua Ubalozi
wake nchini Uturuki na hivi leo Mhe. Rais atamwapisha Balozi Mteule, Prof.
Elizabeth Kiondo atakayetuwakilisha Uturuki.
Pia kumekuwa
na ziara za viongozi wakuu wa kitaifa wa nchi hizi mbili ikiwemo ziara ya Rais
mstaafu wa Uturuki, Mhe. Abdullah Gul
nchini mwaka 2009 ; ziara ya Rais wa Awamu ya Nne wa Tanzania, Mhe.
Jakaya Mrisho Kikwete nchini Uturuki mwaka 2010 na ziara ya Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein mwaka 2011.
Tume ya Pamoja ya Biashara.
Tanzania na
Uturuki zinashirikiana pia kupitia Tume ya Pamoja ya Biashara ambayo
ilianzishwa baada ya kusainiwa kwa Mkataba wa Ushirikiano kwenye masuala ya
Biashara mwaka 2010.
Kikao cha kwanza cha Tume hiyo kilifanyika Jijini Dar es
Salaam mwezi Novemba 2012. Katika kikao hicho pande zote zilikubaliana
kushirikiana kwenye maeneo mbalimbali hususan biashara na uwekezaji, elimu,
Kilimo, Nishati na Madini, Maendeleo ya viwanda na mawasiliano ya simu.
Kikao cha
Pili cha Tume ya Pamoja ya Biashara kati ya Tanzania na Uturuki kilifanyika
tarehe 11 – 12 Januari 2017, Uturuki kwa lengo la kujadili utekelezaji wa
Makubaliano ya Kikao cha Kwanza na kuibua maeneo mapya ya ushirikiano kati ya
pande hizi mbili.
Aidha, Mkutano huu pia ulikuwa na umuhimu wa kipekee kwa kuwa
ulifanyika ikiwa ni maandalizi ya ziara ya Kiserikali ya Mheshimiwa Recep
Tayyip ErdoÄŸan, Rais wa Jamhuri ya Uturuki inayotarajiwa kufanyika tarehe 23
Januari, 2017.
Pande zote
mbili zimekubaliana kuongeza nguvu katika kuhamasisha uwekezaji kwenye nchi
zetu. Katika kutekeleza hili, Uturuki imepanga kuandaa Mkutano wa Uwekezaji
kati ya Tanzania na Uturuki ndani ya robo ya pili ya mwaka huu jijini Istanbul.
Vile vile, nchi zote mbili zimekubaliana kubadilishana taarifa za fursa za
uwekezaji kupitia Balozi zetu na Baraza la Biashara la Tanzania na Uturuki.
Aidha, Taasisi zetu za Uwekezaji zimeelekezwa kuanza majadiliano ya kuingia
Mkataba wa Ushirikiano ili kuhamasisha uwekezaji nchini.
Hali kadhalika,
Uturuki imemchagua Mwambata wa Biashara katika Ubalozi wao wa Dar es Salaam na
Tanzania imeahidi kuteua Afisa Maalum ndani ya mwezi mmoja kushughulikia
uhamasishaji wa uwekezaji na biashara kati ya nchi hizi mbili.
Mafanikio yaliyopatikana kutokana na
ushirikiano kati ya Tanzania na Uturuki.
Tangu
kuanzishwa kwa Tume ya pamoja ya ushirikiano ya kiuchumi mafanikio ya
ushirikiano baina ya nchi hizi mbili yameonekana ikiwemo:- Kuimarishwa kwa
ushirikiano katika masuala ya Usafiri wa Anga ambapo Shirika la Ndege la
Uturuki lilianzisha safari tatu za moja
kwa moja kutoka Istanbul hadi Dar es Salaam, Kilimanjaro na hivi karibuni
Zanzibar.
Kuanzishwa kwa safari hizi kumekuza biashara kati ya Uturuki na
Tanzania ambapo mwaka 2009 ukubwa wa biashara ulikuwa Dola za Marekani
milioni 66 sawa na shilingi bilioni 145.2 lakini hadi kufikia Februari 2016
biashara kati ya nchi hizi mbili
iliongezeka kwa Dola za Kimarekani milioni 160 sawa na shilingi bilioni 352.
Aidha, kuzinduliwa
kwa Baraza la Biashara kati ya Tanzania na Uturuki mwaka 2013 ambalo
kumewezesha kuimarisha ushirikiano wa sekta binafsi za nchi hizi mbili na Kuongezeka kwa Makampuni ya Uturuki
yaliyowekeza nchini ambapo hadi sasa ni Kampuni 30 zimefanya uwekezaji wenye
thamani ya Dola za Kimarekani milioni 305.08 na zinatarajiwa kutengeneza ajira
2,959.
Imetolewa
na:
Kitengo cha
Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dar es Salaam
20 Januari,
2017.
|
No comments:
Post a Comment