Wengine
walimlipa Sh milioni mbili, Sh milioni moja na wengine Sh 500,000, wakitarajia
angewasaidia. Walitembea usiku na mchana ndani ya pori hilo, wakipishana na
wanyama wakali kama simba na nyati, hivyo kuhatarisha usalama wa maisha yao na
watoto wao.
Hali ilizidi
kuwa mbaya zaidi, baada ya kutimia siku ya tano wakiwa ndani ya pori hilo, pale
walipoishiwa chakula na maji, hivyo kuwalazimu kuanza kuchinja ng’ombe na
kunywa damu kwaajili ya kukata kiu. Pia walikula kinyesi chao ili kupunguza
njaa. Yule mwenyeji wao aliwatelekeza baada ya kuona hali zao zimekuwa mbaya.
Alitokomea
kusikojulikana, akiwaacha wasijue pa kwenda, hivyo kulazimika kutelekeza mifugo
yao ili kunusuru kwanza maisha yao. Halikadhalika, wengine walilazimika kunywa
mikojo yao na mingine kuwanywesha watoto wao kunusuru maisha yao, hali
iliyowafanya kuathirika kiafya na kushindwa kuendelea na safari.
Wengine
walianguka na kupoteza fahamu. “Sisi tulikuwa tunataka turudi nyumbani kwetu
Morogoro. Huku tulikuja wakati wa operesheni ya Morogoro, huku tulikuja kununua
ng’ombe lakini miji yetu ipo kule Morogoro. Tukaambatana na huyo mwenyeji wetu
aliyejitambulisha kwa jina la Mzee Mzigua na mtoto wake.Lakini tunajua mpaka
nyumbani kwake”alisema Kiongozi wa msafara wa wafugaji hao, aliyejitambulisha
kwa jina la Lisesi Cherahani Bela na kuendelea;
“Zilitimia kama siku nne tukiwa hatujanywa
maji, jua lilikuwa linawaka, tukaanza kuanguka, tukaanza kuchinja ng’ombe na
kunywa damu, tulijaribisha kula kinyesi cha ng’ombe, tulikuwa tunakojoa mkojo
tunanywesha hata watoto. Mimi nilikunywa mkojo lita moja, ikaniathiri hapa kifuani,
kumbe mkojo ni kitu kibaya.”
|
Akizungumza
na waandishi wa habari waliofika katika eneo hilo, kiongozi huyo alisema baada
ya kuona hali inakuwa mbaya zaidi, alitafuta eneo ambalo lina mtandao wa simu
na kufanya mawasiliano na watu mbalimbali, ambapo alifanikiwa kuwasiliana na
watu wa Kigoma na kuomba msaada wao.
Alisema kuwa
watu hao, waliwasiliana na wahifadhi wa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi na
kuwasiliana na wahifadhi wa Pori hilo la Selous, ambao walianza kazi ya
kuwasaka na hatimaye kuwakuta katika eneo la Mlima Luhombelo, lililopo katikati
ya Pori hilo wakiwa tayari wameshadhoofika kiafya.
Askari hao
wa wanyamapori wa Pori hilo, waliwapatia uji na maji na kuwapa huduma ya kwanza
wale wengine ambao walikuwa na hali mbaya.
Baada ya
taarifa hizo za kupotea kwa wafugaji hao, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na
Utalii, Gaudence Milanzi alifika katika eneo hilo juzi, akiambatana na Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA), Martin Leibooki,
Meneja wa Pori la Akiba la Selous, Henock Msocha na maofisa wengine wa wizara
na pori hilo.
Milanzi alisema
Serikali inaangalia namna ya kuwasaidia wafugaji hao, kurejea katika hali zao
kiafya pamoja na kuwasaidia kutafuta mifugo yao ili waweze kurejea katika
makazi yao na kuendelea na shughuli zao.
“Kwa upande
wa Serikali kama Wizara hatuchukulii kama hawa wameingia kwenye hifadhi hapana,
muhimu kwanza ni kuokoa maisha ya binadamu, na hicho ndicho tunategemea
kukifanya sasa hivi, na baada ya hapo kutakuwa na masuala ya kutafuta hiyo
mifugo, kwa sababu wamepata hasara kubwa”alisema Katibu Mkuu huyo.
Aliutaka
uongozi wa wilaya ya Rufiji, kutoa ushirikiano na wizara ili kuwabaini
waliowadanganya wafugaji hao, kwa kuwaingiza kwenye pori hilo na kuwatapeli
kiasi hicho kikubwa cha fedha.
“Hawa
waliowadanganya na kupita huko ndani ya pori kwa kweli tutaendelea kuwatafuta
na tutaomba tuwe na ushirikiano na uongozi wa Wilaya kwa sababu inaelekea kuna
watu kazi yao ndo hiyo, ukiangalia pesa walizowapa ni nyingi sana, sasa watu
wamechukua pesa zote na wamewaacha katika hali kama hii, wengine wana watoto
wadogo, kwa hiyo tutahakikisha tunashirikiana kuwatafuta ili tukomeshe hili
tatizo moja kwa moja”alisema.
Katibu Mkuu
huyo alimpongeza Mkurugenzi Mkuu wa TAWA na Mhifadhi Selous kwa juhudi za
haraka walizochukua. Alisema wizara yake itaendelea kushirikiana na Mamlaka mbalimbali,
kutoa misaada ya haraka, endapo yatatokea tena matukio ya aina hiyo.
Kwa upande
wake, Leibooki alisema TAWA ambao ndiyo wamiliki wa hifadhi zote za wanyamapori
nchini, haitawachukulia hatua za kisheria wafugaji hao, kwa kuwa waliingia
ndani ya pori kwa kudanganywa na watu wenye nia mbaya.
Lakini,
alisisitiza kuwa mamlaka yake, itawashughulikia kisheria wawindaji haramu na
wafugaji wanaoingiza mifugo yao ndani ya hifadhi zilizo chini ya Mamlaka yake.
Pia alisema
Mamlaka yake, inaendelea na utaratibu wa kushirikiana na wananchi waishio
pembezeni mwa hifadhi zote, kwa kuwapa elimu ya ufugaji bora kwa kushirikiana
na wizara zinazohusika na kuendeleza miradi ya maendeleo, ikiwemo miundombinu
ya maji.
Katibu Mkuu
wa Chama cha Wafugaji chini (CCWT), Magembe Makoye aliwataka viongozi wa
Halmashauri mbalimbali nchini, kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji mahali
walipo, bila ya kuondoa watu wengine.
Alisema kuwa
wao kama chama, wamesikitishwa na tukio la kuondolewa kwa wafugaji hao katika
bonde hilo la Rufiji, kwa kuwaambia warudi walipotoka. Alisema tamko hilo
lilitolewa na uongozi wa Halmashauri hiyo na ndilo lililosababisha matatizo
hayo.
|
Makoye
alisema kufanya hivyo, hakuondoi migogoro ya wafugaji na wakulima, badala yake
ni kuendelea kuzalisha migogoro hiyo katika maeneo mengine, ambayo wafugaji
watahamia.
“Tunalaani
kweli vitendo hivi vya viongozi na watendaji wengine wa Halmashauri kuwafukuza
wafugaji, tena wakati mwingine kwa kuwatisha na matokeo yake wananchi hawa 50
wangepoteza maisha, kama isingekuwa bahati ya mtu mmoja kuwa na simu kati yao”
alisema Katibu Mkuu huyo.
“Kwa kweli
kwa niaba ya wafugaji wote wa Tanzania naishukuru sana Wizara ya Maliasili
kupitia kwa Katibu Mkuu, Gaudence Milanzi.” alisema Katibu huyo.
Alisema kuwa
kungeweza kutokea majanga makubwa zaidi kwa kuwa kuwa wafugaji hao walikuwa
wakisafiri na watoto wao wadogo katika mazingira hatarishi katikati ya pori
hilo, ambalo lina wanyama wakali.
“Kwa kweli
ni mazingira ya kusikitisha. Lakini niishukuru sana Serikali kwa maana ya
Wizara ya Maliasili na Utalii, wamefanya kazi yao kwa namna ambavyo mimi
ninawiwa kuwashukuru. Tangu jana tumewasiliana na Katibu Mkuu wa Wizara, leo
watu wote wameweza kupatikana, kumefanyika doria ya ndege, doria za magari,
doria kwa miguu, wamewatafuta hawa watu, wamewaokoa, wamewaleta kwenye huduma
za afya, wamewapa chakula, wamewahifadhi, hawajawadhuru” alisema.
Aliiomba
Serikali kuhakikisha tatizo la wafugaji nchini, linatafutiwa ufumbuzi wa
kudumu, kwani jamii haiwezi kuendelea kubaki na tatizo hilo kwa miaka yote.
Alitaka wafugaji watafutiwe maeneo ya kudumu ya kufugia, ikiwa ni pamoja na
kupimiwa maeneo yao, badala ya hali ilivyo sasa kuafukuza kila kukicha.
|
No comments:
Post a Comment