Maaskofu na
Mapadre wote nchini Tanzania wameombwa kuandaa Misa, Mikesha, Mafungo, Hija na Maombi
mbalimbali kwa ajili ya kuombea mvua kutokana na ukame uliopo.
Hayo
yalibainishwa jana,January 13, 2017 katika taarifa iliyotolewa na Baraza la
Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kupitia kwa Mwenyekiti wake, Askofu wa Jimbo
la Iringa, Tarcisius Ngalalekumtwa.
Alisema kuwa
hiki ni kipindi cha kilimo na mvua katika maeneo mengi nchini lakini hali sio
ile iliyozoeleka kwani mvua hazifiki kuruhusu watu kuendelea na shughuli zao za
kawaida.
“Kutokana na
hali hii yapo maeneo Tanzania ambayo tayari yamekumbwa na uhaba mkubwa wa
chakula. Ninaomba uwepo wa kasi ya sala kila mahali kuombea hali hii,” alisema
Askofu Ngalalekumtwa. Alisema pia kuwa kuadhimishwa kwa misa, hija, maombi na
mikesha kutasaidia kwa kuwa kila aombaye hupokea.
Alifafanua
kuwa kila mmoja anapaswa kuomba baraka za Mwenyezi Mungu kuhusu kazi za mikono
yake hususan kilimo ili akapate mazao ya nchi na kumtumikia Mungu kwa mioyo ya
utulivu na shukrani.
Hata hivyo,
akinukuu maandiko Matakatifu ya Biblia, Askofu Ngalalekumtwa alisema kuwa Mungu
aliyewatunza wana wa Israeli walipokuwa safarini wakielekea nchi ya Ahadi kwa
kipindi cha miaka 40, awaangalie kwa wema, upole na upendo.
|
No comments:
Post a Comment