Rais wa
Zambia, Edgar Lungu amewataka watendaji wa nchi yake na Tanzania, kuweka siasa
pembeni na kujikita kwenye biashara zitakazoinua uchumi wa nchi hizo mbili.
Akizungumza
jana jijini Dar es Salaam wakati wa kuhitimisha ziara yake ya siku tatu, Rais
Lungu aliyetembelea Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Shirika la Kusafirisha
na Kupokea Mizigo la Zambia (Zamcargo), alisema licha ya kuenzi mchango wa
waasisi wa mataifa hayo, Mwalimu Julius Nyerere na Kenneth Kaunda, watajikita
zaidi kwenye biashara.
“Changamoto mliyonayo ni kwenu uongozi na Bodi
ya TPA kwa watu wa Kusini au Mashariki au hata nje ya Afrika. Watu wa Zambia
wanasema muda wa siasa umekwisha, sasa ni muda wa maendeleo. Hatutawaunga mkono
kwa sababu niko karibu sana na Rais (John) Magufuli. Ni kweli niko karibu na
Rais Magufuli kama mlikuwa hamjui, lakini hatuwaungi mkono kwa sababu hiyo,
bali kwa ufanisi wenu,” alisema Rais Lungu.
Akizungumzia
miradi ya reli ya Tazara na bomba la mafuta la Tazama, Rais Lungu alisema nayo
inapaswa kufanya kazi kwa ufanisi.
“Ni kweli sisi ni ndugu lakini hatuangalii
hilo. Wazambia wanataka mbolea ifike haraka, shaba isafirishwe haraka kwenda
sokoni,” alisema.
Akiwa katika
ofisi za Zamcargo, Rais Lungu alirudia wito wake wa ufanisi wa biashara akisema
hatasita kuwawajibisha watendaji wa taasisi hiyo.
Awali,
Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Deusdedit Kakoko alisema Zambia imekuwa mteja namba moja katika usafirishaji
wa mizigo kupitia Bandari ya Dar es Salaam.
Kakoko
alisema mwaka 2014, Zambia ilichangia asilimia 36 ya mizigo ambayo ni sawa na
tani milioni 5.2 ikiwa ni mbali ya nchi nane zinazotumia bandari hiyo.
“Takwimu za
TPA zinaonyesha kuwa mizigo ya Zambia inayopitia hapa imekuwa ikiendelea kila
mwaka. Mwaka 2011, bandari ilipokea tani milioni 1.6 za mizigo inayotoka na
kuingia. Lakini mwaka 2014 Zambia ilipokea tani milioni 1.9 za mizigo ya
Zambia,” alisema Kakoko.
Alisema
kutokana na umuhimu huo, uongozi wa TPA umekuwa ukiboresha huduma ili kufanya
kazi kwa ufanisi.
“Kwa mfano,
muda wa kutoa mizigo bandarini umepunguzwa hadi siku kumi na moja mwisho wa
Oktoba kulinganisha na siku 32 zilizokuwa mwaka 2008. Bandari pia imeboresha
mfumo wa malipo ya mizigo kwa wateja wake kwa kutumia mfumo wa kielektroniki,”
alisema Kakoko.
Katika ziara
hiyo ya bandarini, Lungu aliambatana na Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa
Kimataifa na Kikanda, Balozi, Augustine Mahiga, Naibu Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani na katibu mkuu wa wizara hiyo, Dk
Leonard Chamuriho.
Mara baada
ya ziara hiyo Rais Magufuli aliwaongoza viongozi wengine wa Serikali kumsindikiza
mgeni wake huyo uwanja wa ndege na kurejea Zambia.
Viongozi
wengine waliofika uwanjani hapo ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa na viongozi wengine.
Rais Lungu
aliondoka uwanjani hapo saa 7: 40 mchana.
|
No comments:
Post a Comment