Soma Taarifa ya Mkoa wa Kagera kuhusu Janga la tetemeko la Ardhi la Septemba 10,2016. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Tuesday, September 13, 2016

Soma Taarifa ya Mkoa wa Kagera kuhusu Janga la tetemeko la Ardhi la Septemba 10,2016.

TAARIFA YA MKUU WA MKOA WA KAGERA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU HATUA ZINAZOCHUKULIWA NA SERIKALI JUU YA JANGA LA TETEMEKO LA ADHI
 
TAREHE 13 SEPTEMBA, 2O16

Ndugu Waandishi wa Habari, Naendelea kuwapa wananchi pole na janga la tetemeko lililotupata katika Mkoa wetu wa Kagera tarehe 10.09.2016, aidha natumia fursa hii kuwapa taarifa za maendeleo ya hatua za Serikali inazoendelea nazo kuhusu janga hilo pamoja na juhudi mbalimbali za wataalam wa masuala ya majanga ili kuhakikisha wananchi waliopatwa na maafa kujua ni hatua gani zimechukuliwa na Serikali.

Ndugu Waandishi wa Habari, Napenda kuwafahamisha kuwa baada ya tetemeko kubwa lililotokea tarehe 10.09.2016 majira ya alasiri lililokuwa na ukubwa 5.7 katika vipimo vya Richter lilisababisha vifo vya wananchi 17, majeruhi 253, nyumba za makazi zilizoanguka ni 840, nyumba zilizopata nyufa ni 1,264 na majengo ya taasisi yaliyoripotiwa kuanguka ama kupata nyufa ni 44 kwa takwimu ambazo tunazo hadi tarehe 13.09.2016

Ndugu Waandishi wa Habari, Baada ya tetemeko la kwanza la tarehe 10.09.2016 lilitokea tetemeko lingine dogo ambalo lilitokea usiku wa tarehe 11.09.2016 majira ya saa 4:15 usiku na halikusababisha madhara yoyote ukiacha yale yaliyokuwa yamesababishwa na tetemeko la kwanza katika Wilaya zote za Mkoa wa Kagera.

Isipokuwa, wananchi watatu walipata mshituko katika Manispaa ya Bukoba na kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa na kulazwa ambapo wanaendelea vizuri na matibabu.

Aidha, kilitokea kifo kimoja tarehe 12.09.2016 katika Wilaya ya Missenyi na kufikisha idadi ya watu 17 waliokufa kutokana na tetemeko la ardhi Mkoani Kagera.
Ndugu Waandishi wa Habari, Katika Hospitali yetu ya Rufaa ya Mkoa wagonjwa waliokuwa wamelazwa toka siku ya janga lilipotokea walikuwa 150 hadi kufikia leo tarehe 13.09.2016 wagonjwa walioruhusiwa ni 76 na wagonjwa 74 wanaendelea na matibabu.

Aidha, katika hali isiyo kuwa ya kawaida lilitokea tukio lingine la kusikitisha tarehe 12.09.2016 saa 5:00 asubuhi katika Wilaya ya Missenyi eneo la Mtukula katika machinjio ya ng’ombe ambapo wananchi wawili Abdul Amadi (47) na Shafi Saidi (37) walipigwa radi na kufa palepale.

Ndugu Waandishi wa Habari, (Hatua Zinazochukuliwa na Serikali) baada ya tetemeko kutokea Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kurudisha hali ya wananchi katika maisha ya kawaida na hatua hizo ni kama ifuatavyo;

Kamati ya maafa ya Mkoa na Kamati ya maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Mhe. Jenister Muhagama tulifanya tathimini ya haraka ya pamoja na kubainisha mahitaji yote ya haraka yanayohitajika kwa ajili ya wananchi waliopatwa na janga la tetemeko.

Ndugu Waandishi wa Habari, Natoa wito kwa wananchi, taasisi, idara, na mashirika ya umma na yasiyokuwa ya umma, marafiki na wananchi wote walioguswa na janga la tetemeko katika mkoa wa Kagera wanaweza kuchangia michango yao kupitia Akaunti ya Maafa iliyopo Benki ya CRDB yenye jina “KAMATI YA MAAFA KAGERA CRDB BUKOBA” Akaunti Namba 0152225617300.(Kwa walio nje ya nchi Swift code: CORUtztz).

Ndugu Waandishi wa Habari, Mahitaji mengine ambayo wadau mbalimbali wanaweza kuchangia ni pamoja na Madawa, Tiba pamoja na vifaa tiba kwa upande wa afya. 

Aidha, vinahitajika vifaa vya ujenzi ambavyo ni Mabati 90,000 yenye gharama ya Tshs.1,710,000,000/= Sementi mifuko 9,000 yenye thamani ya Tsh.162,000,000/= Mbao zenye gharama ya Tsh.450,000,000/= na Misumari yenye gharama ya Tsh. 12,000,000/=. Jumla ya gharama zote ni Tsh.2,334,000,000/= .

Ndugu Waandishi wa Habari, Katika hatua nyingine Serikali imeamua kufunga shule za Sekondari Nyakato na Ihungo baada ya kutokea uharibifu mkubwa katika miundombinu ya shule hizo ambayo ni madarasa, mabweni na vyoo na kuonekana havifai kutumika tena kwa kuanguka kuta au kupata nyufa kubwa.
Aidha, wanafunzi waliruhusiwa kuondoka kurudi katika familia zao baada ya kuonekana kuwa wameathirika kisaikolojia na tetemeko hilo. 

Kamati ya maafa inajenga madarasa, mabweni na vyoo vya muda katika muda wa wiki mbili ili wanafunzi warejee shuleni kuendelea na masomo.

Pia Serikali imefanya juhudi za kuleta wataalam wa afya ambao ni Madaktari Bingwa sita kutoka Hospitali ya Bugando ili kuja kutoa huduma kwa wagonjwa ambao watahitaji msaada zaidi wa kitabibu. Aidha, ubalozi wa China umeleta waganga wa kusaidia matibabu kwa wahanga.

Ndugu Waandishi wa Habari, Katika uchunguzi uliofanywa na Wataalam kutoka Wakala wa Jiolojia Tanzania kuhusu tetemeko lililotokea Mkoani Kagera walibainisha sababu za tetemeko kuwa kitovu cha tetemeko hilo kuwa kiko chini sana ya ardhi kwa kutafasiri umbile la mawimbi ya tetemeko hilo yaliyonakiliwa na vituo vya kupimia matetemeko ya ardhi (Picka Namba 5) inaonekana kuwa tetemeko hilo limetokana na misuguano ya mapande makubwa ya ardhi iliyopasuliwa na mipasuko ya ardhi mithili ya mipasuko kwenye bonde la ufa.

Ndugu Waandishi wa Habari, Serikali ya mkoa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali hasa Wataalam kutoka Wakala wa Jiolojia Tanzania inaandaa vituo mbalimbali katika mkoa ili kutoa elimu jinsi ya kufanya mazoezi ya kuchukua tahadhari kabla ya tetemeko, wakati wa tetemeko na baada ya tetemeko kutokea ili kujizoesha kwani mara nyingi wakati wa matukio ya majanga kama hayo watu huchelewa kuchukua uamuzi wa haraka kujinusuru na kujiuliza kwamba wafanye nini. Hivyo mazoezi ya mara kwa mara ya jinsi ya kuchukua tahadhari humfanya mtu kufanya uamuzi wa haraka pindi tukio linapotokea.

Ndugu Waandishi wa Habari, Napenda kuchukua fursa hii kuwaomba wale wote ambao watawiwa kutoa masaada wowote wa kifedha au vifaa wawasiliane na ofisi yangu (Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera) kwa maelekezo zaidi au watumie Akaunti ya Benki iliyotajwa hapo juu na siyo mahala pengine popote. 

Aidha, mimi kama Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa ya Mkoa ningependa misaada yote ipite katika ofisi yangu ili iwafikie walengwa kwa utaratibu maalum na mzuri tuliojiwekea kama mkoa.( Iwapo utahitajika ufafanuzi zaidi wadau wanaweza kuwasiliana na Ofisi ya Waziri Mkuu idara ya Maafa.)

Ndugu Waandishi wa Habari, Mwisho napenda kusema kwamba tutaendelea kutoa taarifa hizi kadri tunavyozidi kuzipokea na nawashukuru sana waandishi wa habari na vyombo vya habari kwa ushirikiano wenu na tuzidi kushirikiana kuwajulisha Watanzania kila hatua tunayoichukua kuhusu janga hili la tetemeko katika Mkoa wa Kagera.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad