|
Aliyewahi kuwa kocha wa Simba James
Aggrey Siang’a amefariki leo alfajiri
nchini kwake Bungoma nchini Kenya baada ya kuugua kwa muda mrefu. Siang’a
alikuwa ni miongoni mwa makocha walioheshimika sana Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa afisa wa Chama cha
Kefoca, Bob Oyugi, Siang’a ambaye aliwahi kuchezea Gor Mahia, Luo Union na timu
ya taifa Kenya Harambee Stars kama kipa, pia aliwahi kuwa kocha wa klabu za
Simba, Moro United na Express ya Uganda.
Siang’a aliidakia Kenya katika
Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 1972 na pia alikuwa kocha wa
Harambee Stars mwaka 1999 na 2000, kabla ya kuhamia Tanzania kufundisha Simba,
Mtibwa Sugar, Moro United na timu ya taifa ya Bara kwa muda mfupi mwaka 2002.
Mashabiki wa Simba SC watamkumbuka
zaidi Sianga baada ya kuipa timu taji la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati
visiwani Zanzibar mwaka 2002, kabla ya kuunda kikosi imara cha vijana wadogo
kilichokuwa tishio katika soka ya Tanzania muongo wote huo.
Akiwa na Moro United Oktoba 2004
Siang’a aliombwa kuinoa Taifa Stars lakini alikataa. Siang’a pia aliinoa Mtibwa
Sugar kabla ya kurejea Kenya kuifundisha timu ya Gor Mahia.
Siang’a ndiye aliyeiwezeha Simba SC
kuitoa Zamalek ya Misri waliokuwa mabingwa wa Afrika katika hatua ya 16 Bora na
kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Tumempoteza mtu wetu sana, Siang’a.
Mchezaji wa zamani wa kimataifa amefariki ijumaa usiku kwa mujibu wa familia
yake. Tunasubiri taarifa zaidi kutoka kwao ili kuendelea na hatua nyingine.
Mwili wake upumzishwe kwa amani,” alisema Oyugi.
Kikosi hicho kilikuwa kikiundwa na
vijana kama Said Swedi, Ramazani Wasso, Boniface Pawasa, Victor Costa, Lubigisa
Madata, Suleiman Matola, Primus Kasonzo, Christopher Alex, Shekhan Rashid,
Ulimboka Mwakingwe, Emmanuel Gabriel na Athumani Machuppa.
Sianga alizitoa BDF XI ya Botswana,
Santos ya Afrika Kusini kabla ya Zamalek. Santos aliitoa kwa penalti 9-8 baada
ya sare ya jumla 0-0 na Zamalek pia aliitoa kwa penaliti 3-2, baada ya sare ya
jumla ya 1-1 kila timu ikishinda 1-0 nyumbani kwake.
Simba ikapangwa Kundi A pamoja na
Ismailia ya Misri, Enyimba ya Nigeria na ASEC ya Ivory Coast na ikafanikiwa
kushinda mchi mbili na kutoa sare moja.
Ilishinda 1-0 dhidi ya ASEC, 2-1
dhidi ya Enyimba na sare ya 0-0 na Ismailia katika mechi za nyumbani Uwanja wa
Taifa, (sasa Uhuru), Dar es Salaam.
Katika mechi za ugenini, Simba SC
ilifungwa 3-0 na Enyimba, 2-1 na Ismaili na 4-3 na ASEC.
Kituko kikubwa cha
kukumbukwa cha Siang’a ni pale alipompiga kichwa aliyekuwa kocha wa SC Villa,
Mserbia Milutin Sredejevic ‘Micho’ kwenye fainali ya Kombe la Klabu Bingwa
Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame Simba SC ikilala 1-0 Uwanja wa
Mandela, Namboole, Kampala, Uganda.
Micho alikwenda kwenye benchi la
Simba kumsalimia Siang’a aliyekuwa ana hasira za kipigo na kukosa Kombe na pia
akilalamikia bao la Mkenya mwenzake, Vincent Tendwa aliyemalizia krosi ya
kiungo Mtanzania, Shaaban Kisiga ‘Malone’ lilikuwa la kuotea – lakini
akaambulia ‘ndoo’.
Kabla ya Micho kujibu, wawili hao
wakatenganishwa na sherehe za ubingwa zikachukua nafasi yake Namboole.
Baada ya kuondoka Simba alifichua
mpango wa kufuatwa na kiongozi mmoja wa klabu wakati huo kumshawishi wapokee
hongo ya Zamalek timu ifungwe mwaka 2003.
Siang’a alidai alikataa na akaiongoza
Simba kuitoa Zamalek, lakini kilichofuatwa ni kufukuzwa kwenye timu kwa chuki
za kiongozi huyo mwenye asili ya Kiasia.
Mungu ampumzishe kwa amani gwiji huyo
wa soka Kenya.
|
No comments:
Post a Comment