|
Siku mbili
baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kuahidi kufanyika maridhiano kati ya
uongozi wa Bunge na wabunge wa upinzani katika kikao kijacho kinachotarajiwa
kuanza Septemba 6, mwaka huu, Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson amesema hataki
kuwasikia wabunge wa upinzani wala kuwawaza.
Kauli hiyo
ya Naibu Spika huenda ikazidi kutonesha kidonda hasa baada ya Bunge la Bajeti
lililofanyika Mei mwaka huu kuacha majeraha kutokana na wabunge wa upinzani
wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kususia vikao vyote
vilivyoendeshwa na kiongozi huyo.
Juzi wakati
akihojiwa kupitia kipindi cha Funguka kinachorushwa na Kituo cha Luninga cha
Azam, Spika Ndugai, alisema anatafuta
mbinu ya kuweka sawa mambo hayo kwa kufanya maridhiano ikiwemo kushirisha maspika wastaafu.
Akizungumza
na gazeti la Mtanzania juzi katika mahojiano maalumu ofisini kwake jijini Dar
es Salaam, Dk. Tulia alisema hapendi kuwawazia wabunge hao wa upinzani.
“Kwa kuwa
Spika yeye kazungumza siwezi kucomment chochote kwa sababu sipendi kuwawazia wabunge
hao,”alisema.
Alipoulizwa
kwamba ni kwanini migogoro ilizidi wakati yeye akiwa anaendesha vikao, alisema
alichokuwa anafuata ni kanuni na kwamba malalamiko hayawezi kukosekana.
“Nashangaa
wengine wanasema kuendesha vikao ni mpaka uwe na uzoefu…unajua zile kanuni hata
ukipewa uendeshe wewe ukishazielewa hazihitaji uzoefu wowote. Kulalamika kuwa
nawapendelea ni jambo la kawaida.
“Kwa mfano
siku iliyotokea vurugu wakati wabunge wa upinzani wanadai kutorushwa matangazo
ya Bunge live, aliyekuwepo kwenye kiti alikuwa ni mwenyekiti ambaye ni mzoefu
wa siku nyingi na ni yeye aliyepeleka majina yao kwenye Kamati ya Maadili, sasa
sidhani kama hiyo ni hoja,”alisema Dk. Tulia
Alieleza
kushangazwa kwa kitendo cha wabunge wa upinzani katika barua yao waliyomwandikia
Spika kwamba hawana imani naye, huku akihusishwa na fedha zilizorejeshwa
serikalini.
“Katika ile
barua walieleza sababu nyingine kuwa hawana imani na mimi, wakanihusisha na
zile Shilingi bilioni 6 zilizorejeshwa serikalini wakati sheria na utaratibu
upo wazi kwa sababu Spika au Naibu Spika hauhisiki na masuala ya fedha bali
anayehusika ni Katibu wa Bunge.
“Kwa hiyo ni
jambo la kushangaza kwamba Naibu Spika karudisha fedha, mimi si mshika mafungu
lakini pia ni namna watu walivyopokea huwezi kuwazuia wanavyokuwazia,” alisema.
Akizungumzia
kauli ya Spika Ndugai kwamba kwa kuwa Bunge la 11 lina wabunge wapya wengi na
kwamba kuwaongoza kunahitaji uvumilivu mkubwa alisema: “Nisingependa kuongelea
kauli ya Spika…lakini uvumilivu wa mtu kutakiwa akae hadi mara 11 halafu
ameendelea kusimama ni uvumilivu gani huo?,” alihoji.
Pamoja na
mambo mengine alisema wakati wabunge wanawake wa Ukawa walipojitoa kwenye Chama cha Wabunge Wanawake (TWPG), alitukanwa
tusi kubwa lakini alinyamaza.
Mei 5, mwaka
huu wakati akichangia mjadala wa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya
Wizara ya Katiba na Sheria, Mbunge wa Ulanga Mashariki, Gudluck Mlinga (CCM),
alidai kuwa ili kuwa mbunge wa viti maalumu Chadema lazima uwe ‘baby’ wa mtu.
“Laiti
ungeona Hansard tusi walilonitukana siku ile, actually Mlinga hajatukana lakini
ulisikia nikilalamika mahali kwamba nimetukanwa? wao wanaongee vibaya…watukane,
mimi bado ni kiongozi wao na siwezi kuanza kuwakasirikia itakuwa sasa nashindwa
kuwaongoza mimi ni kama mzazi wao,” alisema Dk. Tulia.
Alisema
kitendo cha watu kudai kwamba anafanya upendeleo bungeni ni changamoto ya
kawaida, kwa sababu hata katika mabunge ya Jumuiya ya Madola malalamiko ya aina
hiyo yapo.
“Pale
bungeni wako wabunge 389, hawa ni wengi
sana wote hawawezi kupata nafasi ya kuongea. Kwa mfano uliomba nafasi jana
ukapewa ukaomba leo, hata ukisimama mara 11 katika hali ya kawaida huwezi
kupewa kwa sababu wako wengi ambao hawajachangia.
“Kama
kiongozi naona ni sehemu mojawapo ya kusimamia jamii ni changamoto na
itaendelea kuwepo kwa miaka mitano,”alisema Dk. Tulia.
|
No comments:
Post a Comment