Baadhi ya
wananchi wa mitaa ya Kata za Lwanima na
Kishili wilayani Nyamagana mkoani Mwanza wanachangia maji ya visima vya asili na fisi, ng’ombe na mbweha kutokana na kukosa huduma kutoka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira
Mwanza (MWAUWASA).
Kitendo
hicho kimeonekana kuleta hofu kwa wakazi hao wakidai kupatwa na magonjwa kwa
sababu wamekuwa wakikuta vinyesi katika
visima vya maji.
Mbali
ya magonjwa, wanawake wengi wa mitaa
hiyo wamekuwa wakiamka kati ya saa 11.00
na 12.00 ri na kuacha watoto ndani kwa ajili
kuwahi kuchota maji na wengine wamekuwa wakikutana na fisi wakiwa
visimani, jambo ambalo ni hatari kwa usalama wao.
Mpaka sasa
tayari familia moja ya Mwarabu Benard
imepatwa na athari ya mtoto wao, Profipeli Mwarabu (miezi minane), kufariki
dunia hivi karibuni baada ya kuungua
moto saa 12.00 asubuhi akiwa ndani ya nyumba wakati mama yake, Honatha
Timatheo, akiwa amekwenda kuchota maji katika
visima hivyo.
Tukio hilo
lilisababisha Mbunge wa Nyamagana,
Stanslaus Mabula (CCM) na Mkurugenzi wa
Mwauwasa, Antony Sanga kwenda katika familia hiyo na kutoa mkono wa pole pamoja na kutembelea mitaa yenye ukosefu wa
maji na wakaahidi kupeleka huduma hiyo
haraka.
Mwandishi alitembelea
baadhi ya visima vya asili katika mitaa
mbalimbali ya kata hizo pamoja na bonde la linalotenganisha Kata ya
Lwanima na Kishili kwa nyakati tofauti
na kushuhudia jinsi wanawake
wanavyohangaika kugombania maji.
Kisima
kimoja cha asili maarufu kinachojulikana kwa jina la Kibundululu ambacho
kinatumiwa na wakazi wa Bushitu, Kakebe, Majengomapya na Kilimo, kimekuwa
msaada mkubwa kwa wananchi hao lakini ng’ombe wa maeneo hayo wamekuwa wakinywa maji mchana na kujisaidia humo.
Faustina
Christopher ambaye ni miongoni mwa wanawake ambao huwahi kuchota maji hayo, alisema analazimika kuwahi alfajiri ili kupata maji
masafi.
Alisema
wakati mwingine amekuwa akikutana na fisi maeneo hayo.
Edna
Samweli, alisema kutokana na kuwa na biashara yake ya mhagawa amekuwa akiwahi
kwenda kisimani alfajiri kabla ya ng’ombe
kuyachafua kwa vile maji hayo wakati wa
mchana yamekuwa yakinuka kinyesi cha mifugo.
Hata hivyo
visima vingine vilivyopo bonde linalotenganisha kata za Lwanima na Kishili
vimekuwa na idadi kubwa ya wananchi wanaochota maji, huku wafugaji nao wakitegemea kunywesha hapo.
Wakazi hao
wameiomba Serikali hususan Mwauwasa, kuwapatia huduma ya maji ikizingatiwa
wamekuwa wakiteseka kwa kiasi kikubwa wakati wa kiangazi, kama ilivyo sasa.
Akizungumza
na Mwandishi, Mkurugenzi wa Mwauwasa,
Sanga alisema mamlaka
imetenga fedha kwa ajili ya kununua
mabomba ya kusambaza maji.
“Tunaomba
wananchi watuvumilie kwa kuwa tayari watalaamu wametembelea maeneo hayo na
kuchukua takwimu za bomba zinazotakiwa kusambazwa.
“Tutaunganisha
maji kutoka Mahina, kupitia Kakebe na kuelekea Majengomapya , Kilimo hadi
Kanindo, kazi hii itaanza kufanyika ndani ya mwezi huu,”alisema.
|
No comments:
Post a Comment