|
Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki
amesema serikali imelazimika kusitisha ajira mpya za watumishi 71,496
serikalini, mwaka huu hadi pale tatizo la watumishi hewa litakapopatiwa
ufumbuzi.
Akifungua mafunzo
kuhusu maadili ya viongozi wa umma kwa Wakurugenzi watendaji wa halmashauri za
wilaya, miji, manispaa na majiji Ikulu Dar es Salaam jana,Julai 12,2016, Kairuki alisema
tangu oparesheni ya kutafuta watumishi hewa ianze hadi sasa watumishi 12,246
wameshaondolewa.
Kairuki alisema tatizo
la watumishi hewa nchini bado ni kubwa kwani uzoefu unaonesha kuwa nchi nyingi
zilizokumbwa na tatizo hilo, ni asilimia ndogo tu ya watendaji ndio iliyokuwa
inawajibika.
Alisema kwa sasa Serikali imelazimika kusimamisha masuala mengi ya utumishi wa umma ili ipate
taarifa kamili ya aina ya watumishi waliopo, na kwamba ma-DED hao kuhakikisha
wanasimamia vyema oparesheni hiyo kwani hadi sasa watumishi hewa waliobainika,
takribani asilimia 90 wanatokea katika Serikali za Mitaa.
Aidha, Kairuki alisema
pamoja na kugundulika kuwa tatizo la watumishi hewa ni kubwa nchini, pia
serikali imebaini kuwepo kwa watumishi watoro wasiotimiza wajibu wao.
“Nawataka mkahakikishe
mnawabana hawa maofisa utumishi, haiwezekani kuwepo na tatizo la watumishi hewa
kubwa kiasi hiki huku pia kukiwa na tatizo la watumishi watoro, hawa maofisa
kwani walikuwa na majukumu gani?” Alihoji Kairuki.
Alisema endapo serikali
itabaini kuwa maofisa utumishi hao wamehusika katika matatizo hayo ya watumishi
hewa na utoro, wataondolewa mara moja.
“Serikali haina mchezo kila ofisa katika eneo
lake, awe ofisa elimu, afya na kilimo wafanye kazi zao,” alisema.
|
No comments:
Post a Comment