|
Fedha za Mfuko wa
Barabara.
Magufuli alisema anazo
taarifa za baadhi ya wakurugenzi, walikuwa wakishirikiana na mameya, madiwani
na wenyeviti wa halmashauri kwa kupitisha na kuingia mikataba na kampuni zilizo
na uwezo chini ya viwango katika kutekeleza miradi ya barabara; na matokeo yake
miradi mingi haikuwa na mafanikio.
“Nawaambieni mkisimamia
maadili hakuna atakayewafukuza kazi. Msijipendekeze kwa mtu kwa sababu hakuna
aliyepenyeza majina yenu kwangu hadi mkachaguliwa. Kuna mmoja jina lake
lilipenyezwa nikalitupilia mbali,” alisema.
Fedha za elimu Bure.
Aliwataka kuwa makini
na kusimamia vyema Sh bilioni 18.77 zinazotolewa na serikali kila mwezi kwa
ajili ya elimu bure katika shule za msingi na sekondari kwa kuhakikisha
zinatumika vyema kwa lengo lililokusudiwa.
Alisema wapo
wakurugenzi waliokuwa wakizitumia vibaya fedha hizo kwa madai kuwa ni nyingi,
huku kukiwa na taarifa za baadhi ya walimu wakuu katika kufanya udanganyifu kwa
kuandika orodha ya uongo ya wanafunzi na kuongeza idadi ili wapate mgawo mkubwa
wa fedha hizo.
Matumizi ya EFDs
serikalini Pamoja na hayo, Rais Magufuli aliziagiza wizara zote nchini chini ya
makatibu wake wakuu na halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji na
taasisi zote za serikali, kuhakikisha wanaanza mara moja kukusanya mapato yake kwa
kutumia mashine za kielektroniki (EFDs).
“Haiwezekani
mfanyabiashara alazimishwe kutumia mashine hizi wakati sisi serikalini
tunakusanya mapato yetu bila kutumia mashine za EFDs. Ninawataka nyie
wakurugenzi mliopo hapa mkifika katika maeneo yenu mhakikishe halmashauri zenu
zinakusanya mapato yake kwa kutumia EFDs,” alisisitiza.
Aidha aliwaagiza
wakurugenzi hao kuhakikisha wanashiriki katika kutimiza ndoto ya Tanzania kuwa
taifa lenye kipato cha kati kupitia uchumi wa viwanda kwa kila mmoja
kuhakikisha katika eneo lake kunaanzishwa viwanda vidogo.
Kodi ndogo Ndogo.
Akizungumzia kero na
changamoto zinazowakabili wananchi, Dk Magufuli aliwataka wakurugenzi hao
kuhakikisha kipaumbele chao kikubwa kinakuwa ni kuondoa kero za wananchi hasa
wale wenye maisha ya chini.
Alisema watanzania
wamekuwa wakiteseka kwa muda mrefu na kuhangaishwa na kodi za ajabu hali
iliyochangia kurudisha maisha yao nyuma.
“Unakuta mtu analima
mpunga wake, akivuna na kuubeba kuupeleka nyumbani kwa matumizi anadaiwa kodi,
mbona wakati analima hamkudai kodi? “Nawaomba mhakikishe kodi za aina hii
mnazizuia kwani Serikali hii wakati ikiomba kura ya kuingia madarakani,
haikuahidi kutengeneza kero kwa wananchi bali kuziondoa kero hizo,” alisema.
Kutumbua Majipu.
Aliwaagiza wakurugenzi
hao watakapofika kwenye vituo vyao vya kazi, kuhakikisha wanachukulia hatua na
kuwaondoa mara moja watendaji walio kwenye mamlaka yao wasiowajibika na wale
wanaofanya kazi kwa kujifanya miungu watu.
“Nina taarifa wapo
watendaji kata ambao wanajifanya miungu watu, kazi yao kubwa ni kuichonganisha
Serikali na wananchi, tumieni madaraka yenu kuwaondoa ila msimuonee mtu. Nataka
mkawe mitume kwa niaba ya Serikali,” alisema.
Magufuli alisema
amewateua viongozi hao kwa kuwaamini na hatarajii itafika siku atajutia uteuzi
wake na kubaini kuwa aliwateua kimakosa.
Makamu wa Rais.
Kwa upande wake, Makamu
wa Rais, Samia Suluhu Hassan aliwataka Wakurugenzi hao kuhakikisha wanatimiza wajibu
wao kwa kuwa kuhudumia na kusimamia watumishi wa umma na wananchi; na si kuwa
watawala.
“Kila mtu ajiulize kwa
nini Tanzania kwenye watu takribani milioni 50, lakini ameteuliwa yeye. Someni
alama za nyakati na muwatumikie vyema wananchi. Someni pia mazingira ya kazi,
simamieni utendaji wenu kwa misingi ya sheria na katiba,” alisema Samia.
Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa alisema nafasi ya ukurugenzi katika halmashauri za wilaya, miji,
manispaa na majiji ni sawa na injini ya uwajibikaji, hivyo wanaoshika nafasi
hizo wanatakiwa kuwa wachapakazi, waadilifu na wenye kujituma ili serikali na
taifa kwa ujumla lifikie malengo yake.
“Nawataka mkifika
muanze kwanza kuwafahamu vyema washirika wenu kama vile mkuu wa mkoa, mkuu wa
wilaya, kamati ya ulinzi na usalama, sekretarieti ya mkoa, wakuu wa idara na
watumishi. Zijueni vyema ofisi zenu tambueni maeneo yenu ya kazi,” alisema
Majaliwa.
Aidha, alisema
halmashauri pamoja na kuendeshwa kwa fedha za serikali pia zina vyanzo vyake
vya ndani vya mapato na kuwataka viongozi hao kuwa mstari wa mbele katika
kusimamia vyema vyanzo hivyo na ukusanyaji wa mapato yake.
Aliwataka kuwa mstari
wa mbele kusimamia kikamilifu utekelezaji wa maagizo ya Rais likiwemo agizo
lake la hivi karibuni la kuhakikisha kila mwanafunzi wa shule za msingi na
sekondari ana dawati.
Ma-DC.
Pamoja na wakurugenzi
hao kuapa kiapo cha uadilifu, pia wakuu wa wilaya watatu ambao ni Mkuu wa
Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Nurdin Babu, Agnes Hokororo (Manyoni -
Singida) na Miraji Mtaturu (Ikungi – Singida) walikula kiapo hicho.
Ma-DC hao hawakula
kiapo cha uadilifu na wenzao hivi karibuni baada ya kubainika makosa katika
uteuzi wa wateule wa awali wa nafasi za wilaya hizo. Hokororo alichukua nafasi
ya aliyeteuliwa kuwa mkuu wa wilaya hiyo awali, Fatma Toufiq kutenguliwa kwa
kuwa tayari ana wadhifa wa ubunge Viti Maalumu.
Babu na Mtaturu
walichukua nafasi hizo baada ya wateule wa awali ambao ni Fikiri Avias Said na
Emile Ntakamulenga, kutenguliwa uteuzi wao baada ya kuteuliwa kimakosa.
Kwa upande wake,
Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Salome Kaganda
aliwataka viongozi hao kuhakikisha wanazisoma na kuzielewa sheria
zinazowaongoza ikiwemo Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Aidha, aliwataka
kuhakikisha wanatunza maadili yao kama viongozi wa umma na kutambua kuwa wao na
viongozi wa umma kwa saa 24 usiku na mchana hivyo wajiepushe na masuala
yatakayowavunjia heshima na kuwaaibisha mbele ya jamii.
“Lakini pia nawahimiza
mkumbuke kuwa nyie mtakuwa na siri nyingi za serikali haitopendeza kumkuta
mbunge ana nyaraka zilizoandikwa siri za serikali kutoka eneo lako. Moja kwa
moja utajibu,” alisema.
Jaji Kaganda alisema
amebaini kuwa wateule wengi wa nafasi hizo za wakurugenzi ni vijana na
kuwahimiza kuhakikisha hawaleweshwi na madaraka hayo na kujiingiza kwenye
matendo ya anasa na kujivunjia heshima.
|
No comments:
Post a Comment