Wabunge wa UKAWA wamemtaka Rais John
Magufuli kutoa tamko juu ya uvunjifu wa haki za binadamu Zanzibar na kwamba
wana mpango wa kumpeleka katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) wakidai
yanayotokea visiwani humo yana baraka zake.
Katika mkutano wao na wanahabari jana,June 28,2016, Wabunge hao wamemtaka Waziri wa Mambo ya
Ndani, Mwigulu Nchemba kwenda Zanzibar kujionea hali halisi badala ya kupata
taarifa kutoka kwa wasaidizi wake.
Hata hivyo, CCM imesema kuwa inalaani
tamko hilo na kuwa kama UKAWA wanaona kuna masuala yanayohitaji kurekebishwa na
kuhitaji hatua za haraka za Serikali watumie vyombo vinavyotambulika kisheria
kama Bunge badala ya kuishia kulalamika “vichochoroni”.
Akitoa tamko la Wabunge hao jana, Mbunge
wa Vunjo (NCCR-Mageuzi) alieleza kuwa hali ya kiusalama inazidi kuwa mbaya
Pemba na Unguja baada ya uchaguzi wa marudio wa Machi 20,2016 kutokana na baadhi ya
wananchi kupigwa na vikosi alivyodai ni vya usalama.
Mbatia alisema kuwa vikosi vya ulinzi
hususani jeshi la polisi vimekuwa vikishiriki katika vitendo vya ukiukwaji wa
haki za raia Pemba kwa zaidi ya miezi miwili kwa polisi kupiga mabomu ya
machozi, kuwakamata ovyo wananchi, kuwapiga na kuwatesa na kisha kuwafungulia
mashtaka bandia.
Kutokana na vitendo hivyo, Mbatia
alisema wabunge wa Ukawa wanapenda kusikia kauli ya wazi ya Dk Magufuli juu ya
uonevu huo uliodumu kwa muda mrefu dhidi ya Wazanzibari na kutoheshimiwa haki
za binadamu zikiwamo za kutoa maoni na kujikusanya.
Mbatia, ambaye ni Mwenyekiti Mwenza
wa UKAWA, alisema Rais anapaswa kutimiza wajibu wake kuhakikisha usalama wa
raia kama anavyotakiwa kikatiba na kuhakikisha polisi wanawalinda wananchi na
siyo kuwaonea.
“Ukawa inasema wazi kuwa inaendelea
kukusanya taarifa za vitendo vya ubakaji wa demokrasia na haki za binadamu ili
kupata ushahidi wa kutosha wa kumfikisha Dk Magufuli ICC akajibu makosa hayo,” alisema Mbatia.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na Wabunge 66 waliosaini tamko hilo, Mbatia alisema Ukawa inamtaka Mkuu wa Jeshi
la Polisi, IGP Ernest Mangu kuitoa amri ya kusitishwa kwa matendo hayo na
achukue hatua dhidi ya askari wake ambao huwatesa raia ili kurudisha imani kwa
wananchi.
Alisema wananchi wa Pemba na Unguja
waendelee kuikataa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa amani na pia wadumishe
utaratibu wa kuheshimu sheria na kujizuia kufanya vitendo vya kukinzana na
sheria.
Lakini alipotakiwa kuzungumzia tamko
hilo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alitupa lawama zote kwa
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad.
Alisema kuwa ndiye adui mkubwa wa
UKAWA baada ya kususia uchaguzi wa marudio na kuhamasisha wananchi wasiitambue
Serikali na sasa wafuasi hao wanatekeleza maagizo hayo kwa kukata mazao na
kuleta fujo kwa wananchi wenzao.
“Kazi ya dola ni kuhakikisha mtu
havunji amani. Watu wanaofanya vitendo hivyo washughulikiwe ipasavyo na vyombo
vya dola,” alisema Vuai.
Alisema hakuna sababu ya kumpeleka
Rais Magufuli katika mahakama ya ICC kwa kuwa anafanya kazi nzuri ya kuongoza
nchi na kwamba kauli zilizotolewa na Ukawa ni za kitoto.
Alivisihi vyombo vya dola kuendelea
kuimarisha usalama visiwani humo ili watu wenye nia mbaya wasizoroteshe amani
kutokana na matakwa ya viongozi wao.
Awali katika mkutano huo, Mbunge wa Malindi (CUF), Ally Saleh alisema wameamua
kutoa tamko hilo kutokana na hali kuzidi kuzorota Pemba na kwamba ni lazima
Serikali itekeleze wajibu wake kuzuia machafuko zaidi.
Kuhusu mipango yao ya kumshtaki Rais,
alisema kesi hiyo haina haraka kwa kuwa hata wajukuu zao wanaweza kuifungua kwa
kuwa makosa ya jinai hayafi.
“Baada ya kukusanya ushahidi wa kutosha na kujiridhisha kufanya hivyo,
tutafanya. Tanzania siyo kisiwa ulimwengu mzima unaangalia nini kinaendelea
Zanzibar, hivyo tusipowajibika, dunia itatuwajibisha,”alisema Saleh.
Mbunge wa Chambani (CUF), Yusuph
Salim Hussein alisema vyombo vya usalama vimekuwa vikiwatuhumu wafuasi wa CUF
kufanya vurugu hizo lakini tangu zianze tuhuma hizo hakuna mtu hata mmoja
aliyewahi kushtakiwa kwa uharibifu mali au fujo.
“Tangu mwaka 1992 hizo tuhuma kuwa
sasa hakuna mtu aliyewahi kushtakiwa mahakamani na kutiwa hatiani. Ni wao
(Serikali) ndiyo wanawaonea wananchi,” alisema.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi, Hamad Yusuph Masauni alisema ni jambo la kusikitisha kuona viongozi
wanawalinda wahalifu badala ya kuhimiza amani na usalama.
Masauni alisema baada ya uchaguzi
wafuasi wetu ndiyo wanafanya fujo hadi Machi 20 hali ilikuwa shwari Pemba laki
ni viongozi wa CUF ndiyo chanzo cha matukio ya uhalifu unaoendelea Pemba baada
ya Maalim Seif kwenda visiwani huko na kuwataka wasiitambue Serikali.
“Hivi kabla ya tamko la Maalim Seif
vikosi vya ulinzi na usalama havikuwapo ili vikakate mikarafuu na kuchoma
nyumba za watu? Askari wetu wamefunzwa vizuri, wamekula kiapo kulinda usalama
wa raia wote bila kujali chama,”
Alisema nchi haiwezi kuendeshwa kwa
kuacha watu wavunje amani na kwamba vyombo vya usalama vitamshughulikia mtu
yeyote atakayekiuka sheria bila kujali chama.
|
No comments:
Post a Comment