Kauli ya Rais wa Tanzania ya Kuzuia
Vyama vya Siasa Kufanya Shughuli za Siasa kwa Miaka Mitano ni Tangazo la Vita
dhidi ya Demokrasia na Mfumo wa Vyama vingi Nchini
Tumepokea kwa MSHTUKO
na masikitiko makubwa kauli ya Rais kwamba vyama vya siasa havipaswi kufanya siasa
isipokuwa wakati wa Kampeni na kupitia bungeni.
Kimsingi kauli ya Rais
ni kauli yenye nia ya kuvunja Sheria ya Vyama vya siasa inayolinda uwepo wa
mfumo wa vyama vingi na kuhimiza vyama vya siasa kufanya shughuli za siasa
katika msimu wote ili kuthibitisha uhai wao.
Tunaichukulia kauli ya
Rais kama tangazo la vita dhidi ya demokrasia na uhai wa vyama vingi nchini.
Chama chetu kitaitisha vikao vya dharura kujadili hali ya siasa nchini na namna
ya kukabiliana na mashambulizi yanayoendelea dhidi ya demokrasia nchini mwetu.
Tunatoa wito kwa vyama
vyote vya siasa vinavyoamini katika misingi ya demokrasia nchini kukutana
haraka na kujadili namna ya kuunganisha nguvu pamoja katika kupigana vita mpya
ya kulinda demokrasia nchini mwetu.
Aidha, tunatoa wito kwa
wananchi wote na taasisi za kiraia kusimama imara katika kulinda demokrasia.
Tunasisitiza kuwa ushahidi wa kisayansi duniani kote unaonyesha kuwa huwezi
kuua demokrasia bila kuua juhudi za maendeleo. Tusiruhusu mtu yeyote mwenye
mamlaka kuua demokrasia nchini mwetu.
Hatua zozote za kuua
demokrasia ni kuua Umoja, Amani na Mshikamano wa wananchi na Taifa, ambayo
ndiyo misingi ya maendeleo ya nchi yetu kijamii, kisiasa na kiuchumi.
Tunatoa wito kwa
wananchi wote kushikamana na kusimama imara katika kipindi hiki kigumu ili
kulinda demokrasia.
Zitto Kabwe, MB
Kiongozi wa Chama, ACT Wazalendo
Alhamisi, 23 Juni 2016.
|
No comments:
Post a Comment