Mwanamke wa
umri wa miaka 72 amejifungua mtoto wa kiume katika hospitali moja nchini India.
Mwanamke
huyo alipachikwa mimba kupitia njia ya kitaalamu ya IVF ambapo yai la mwanamke
hutolewa kutoka kwenye ovari, kutungishwa mbegu ya kiume na kisha kurejeshwa kwenye
mji wa mimba.
Yai hilo linaweza kutolewa kwa mwanamke mwingine.
Njia hiyo
hutumiwa kuwawezesha wanawake tasa kupata watoto.Daljinder Kaur alijifungua
mtoto wake baada ya kupokea matibabu kwa miaka miwili katika hospitali iliyoko
jimbo la Haryana.
Matabibu
walifanikiwa kumtungisha mimba kupitia IVF mara yao ya tatu.
Mumewe Kaur ana
umri wa miaka 79.
Kisa hicho
kimezua mjadala mkali kuhusu kutumiwa kwa teknolojia hiyo ya IVF na umri ambao
wanawake wanaweza kuruhusiwa kuitumia kupata watoto.
Dkt Kanad
Nayar, katibu mkuu wa chama cha upachikaji mimba nchini India anasema sheria ya
kuamua umri wa juu ambao mwanamke anaweza kuruhusiwa kutumia teknolojia hiyo
itatungwa karibuni.
Umri huo
utakuwa karibu miaka 55.Daktari huyo anasema jambo la kuzingatiwa zaidi ni
uwezo wa mwanamke kumlea mtoto hadi akomae.
"Ukimzaa
mtoto lazima uweze kumlea mtoto kwa karibu miaka 20 hivi. Huwezi kujifungua
mtoto kisha uwaache watu wengine wakimlea,” amesema Dkt Nayar.
Ni mara ya
pili kwa mwanamke mkongwe kujifungua mtoto India. Awali, mwanamke wa miaka 70
alijaliwa mtoto nchini humo.
Lakini
mwanamke huyo alifariki miaka miwili baadaye na sasa mtoto huyo anatuzwa na
jamaa zake.
Credit: BBC
|
No comments:
Post a Comment