Bw. Abdon
Hamaro, Ofisa Kilimo kutoka TAHA na mwezeshaji wa mafunzo ya akinamama wa
kikundi cha ‘Green Voices Kinyerezi’,
akiendelea kuwaelekeza wanakikundi (hawapo pichani) namna ya kuendesha kilimo
hai cha nyanya. Mafunzo hayo yalifanyika hivi karibuni Kinyerezi, jijini Dar es
Salaam.
|
Mratibu wa mradi wa
Green Voices, Bi. Secelela Balisidya (kulia), akiwa makini kuangalia Bw. Hamaro
akiandaa mambo mbalimbali kwa ajili ya kuwaelekeza wanakikundi namna bora ya
kuendesha kilimo hai cha nyanya.
|
Wanakikundi cha Green
Vocies Kinyerezi wakifuatilia mafunzo hayo.
|
Christina Lwiza
(kushoto) akipokea pakiti ya mbegu ya nyanya kutoka kwa Dk. Sophia Mlote tayari
kwa kuwatika ili kuanzisha kilimo hai cha nyanya.
|
Bw. Hamaro akiandaa tray maalum kwa
ajili ya kuwapa wanakikundi kupandikiza mbegu kabla ya kupeleka kwenye vitalu
vyao. Hii ilikuwa ni sehemu ya mafunzo ya vitendo.
|
Wanakikundi wakijaza
udongo maalum kwenye tray kabla ya kuanza kupandikiza mbegu.
|
Bw. Hamaro akiwaelekeza kwa vitendo
wanakikundi namna ya kupandikiza mbegu hizo.
|
Hapa wanakikundi wakiendelea
kupandikiza mbegu kwenye tray.
|
Banda maalum ambalo ni shamba muhimu
kwa ajili ya kilimo hai (green house) ambamo ndani yake nyanya zimestawi.
|
Picha ya pamoja ya wanakikundi cha
Green Voices Kinyerezi.
Ndani ya banda kubwa lililoezekwa na
kuzungushiwa plastiki maalum katika Mtaa wa Kinyerezi Zimbili jijini Dar es
Salaam, Dk. Sophia Mlote akiwa ameongozana na mtaalamu wa kilimo, Bw. Abdon
Hamaro, anaonekana akipanga vizuri vifaa vya kilimo pembeni ya matuta
yaliyostawisha vizuri nyanya.
Pembeni ya banda hili lenye ukubwa
unaokadiriwa kuwa wa meta 8 kwa 12, akinamama kadhaa wamezunguka wakitazama
ustawi wa zao hilo huku Bw. Hamaro akiendelea kutoa maelekezo ya namna ya
kuendesha kilimo hai kinacholimwa katika
mabanda maalum yajulikanayo kama green houses ikiwa ni sehemu ya mafunzo ya vitendo
ya akinamama hao katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na
kuongeza kipato.
Tofauti na nyanya ambazo watu
wamezoea kuziona zikilimwa katika mashamba makubwa na bustani za wazi, nyanya
hizi zinalimwa ndani ya banda ambao ukubwa wake utategemea pia na eneo lililopo
pamoja na uwezo wa mhusika katika kulijenga banda hilo.
Hiki ni kilimo hifadhi ambacho
kinahimizwa kwa sasa ulimwenguni kote ili kukabiliana na mabadiliko ya
tabianchi pamoja na uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji.
“Mtu yeyote anaweza kuendesha kilimo cha mazao mbalimbali
kwa kutumia Green house hata katikati ya Jiji la Dar es Salaam kama tunavyoona,
ni rahisi na rafiki wa mazingira kwa sababu unaweza kuendesha hata kwenye uwa
wa nyumba yako kama hivi,” Bw. Hamaro anaendelea kuwaeleza akinamama
hao, ambao ni wanakikundi wa mradi wa
‘Green Voices’ unaofadhiliwa na taasisi ya Foundation for Women of
Africa yenye makao yake katika mji wa Madrid, nchini Hispania.
Mbali ya kutunza mazingira, Bw.
Hamaro kutoka Chama cha Wakulima wa Bustani Tanzania (TAHA) anasema, kilimo hai
kinasaidia kuzalisha vyakula visivyo na kemikali ambavyo ni rafiki wa afya ya
binadamu.
Katikati ya Jiji la Dar es Salaam
watu wamekuwa wakishuhudia kilimo cha mboga mboga kwenye mabonde ya mito midogo,
ambacho kinatumia umwagiliaji wa maji machafu na yenye kemikali za kutoka
viwandani, ambazo ni hatari kwa afya ya binadamu.
“Mbegu zinazotumika zimetengenezwa maalum na hazifanani za
zile GMO zinazopigiwa kelele, lakini pia unatakiwa kutumia mbolea za asili kama
mboji na samadi, kwa sababu ukitumia kemikali nyingi kwenye udongo, mimea
inanyonya na kemikali hizo zinabaki kwenye vyakula na hatimaye kuingia miilini
mwetu,” anafafanua Hamaro.
Vile vile, Hamaro anasema kilimo cha
Green house kinaweza kutumika hata kwa matunda na kwamba kinatumia maji kidogo
huku pia kikimpunguzia gharama mkulima hasa kwa kuepukana na magonjwa
mbalimbali ambayo yanasababishwa na wadudu.
“Kwa kuwa banda limefunikwa na kukingwa, hakuna wadudu
waenezao magonjwa ya mimea wanaoweza kuingia, lakini faida nyingine ni kwamba,
unaweza kudhibiti hali ya hewa kwa kupunguza ama kuongeza joto ili kuifanya
mimea kukua vizuri,” anaongeza
Dk. Mlote mwenyewe, ambaye ni Ofisa
Mwandamizi katika Wizara ya Kilimo, Chakula na Mifugo, ni mshiriki wa mradi wa
Green Voices ambaye baada ya mafunzo aliyoyapata, sasa anaieneza elimu hiyo kwa
wanawake wenzake majirani wa mtaa huo.
Yeyé ni miongoni mwa wanawake 15
waliopatiwa mafunzo ya kuongeza ujuzi wa jinsi ya kupambana na mabadiliko ya
tabianchi ambayo yaliendeshwa nchini Hispania chini ya ufadhili mkubwa wa
taasisi ya Foundation for Women of Africa inayojihusisha na maendeleo ya
wanawake wa Afrika, ambayo inaongozwa na Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania,
MarÃa Teresa Fernández de la Vega.
“Niliamua kuchagua mradi huu kwa sababu, kwanza ni rahisi
kuuendesha kwa kuwa shughuli zote zipo hapa nyumbani na hata kama nitarudi
usiku kutoka kazini, bado ninaweza kuingia humu shambani na kuhudumia mimea kwa
kuwa banda hili lina taa,” anaeleza.
Aidha, anasema, kwa kuwa anakaribia
kustaafu, na kwa elimu ya kilimo na uchumi aliyonayo pamoja na utaalamu
alioupata, ameona ni vyema aanzishe mradi ambao siyo tu utampatia kipato,
lakini pia utasaidia kutunza mazingira pamoja na kuwa msaada kwa jamii kutokana
na mazao yatakayovunwa.
“Niliamua kuwaelimisha wanawake wenzangu katika mtaa huu
na kuwashawishi waunde kikundi hiki na tayari wamekwishapata mafunzo ya kutosha
ambapo kila mmoja amekuja na wazo la kuanzisha bustani ndogo nyumbani kwake ya
mtindo huu kwa mazao ambayo anaona yanafaa,” anaongeza Dk. Mlote,
ambaye ameeleza kwamba, anakusudia kupanua kilimo hicho kwa kupanda hata miti
ya matunda.
Kikundi hicho cha ‘Green Voices Kinyerezi’ kinaundwa na
wanawake 10, ambapo mbali ya kujifunza kwa nadharia namna ya kuendesha kilimo
hai kwa njia ya green house, walipata fursa ya kufanya kwa vitendo kwa
kupandikiza mbegu za mazao mbalimbali ya mboga mboga kama nyanya, kabichi,
hoho, matango na matikiti maji kwenye bando hilo ambapo yatakapoota kila mmoja
atakwenda kupanda nyumbani kwake.
Christina Lwiza, mmoja wa wanakikundi
hicho ambaye anajishughulisha na biashara ya uuzaji vinywaji kwenye grocery
yake mwenyewe, anasema ameshawishika kuanzisha kilimo cha nyanya nyumbani kwake
ambacho kinaweza kumpatia mapato ya nyongeza pamoja na kukidhi mahitaji ya
nyumbani.
“Sijawahi kulima nyanya, lakini kwa mafunzo niliyoyapata,
hakika naweza kuendesha kilimo hicho bila shida,” anasema Christina.
Karibu wanakikundi wote wamehamasika,
ambapo kila mmoja ameamua kubuni zao ambalo linaweza kumfaa.
Mratibu wa mradi huo, Bi. Secelela
Balisidya, anasema mradi huo wa kilimo hai cha nyanya kwa kutumia green house
ni sehemu ya miradi 10 inayoendeshwa nchini Tanzania kupitia Green Voices
ambapo inaendeshwa katika mikoa sita ya Tanzania Bara.
Mikoa hiyo ni Dar es Salaam, Pwani,
Mwanza, Kigoma, Morogoro na Kilimanjaro ambapo inahusisha kilimo, usindikaji,
ufugaji na utafiti.
“Miradi hiyo ni kilimo cha miti ya matunda mkoani Kigoma,
kilimo cha viazi lishe visiwani Ukerewe mkoani Mwanza, Ufugaji Nyuki mkoani
Morogoro na Pwani, ukaushaji wa mbogamboga kwa kutumia nishati ya jua mkoani
Morogoro, usindikaji wa vyakula mbalimbali kutokana na muhogo mkoani Pwani,
kilimo hai cha mbogamboga, kilimo cha uyoga mkoani Dar es Salaam, mradi wa
majiko banifu mkoani Pwani na mradi wa utafiti wa jiko linalotumia nishati ya
jua mkoani Kilimanajro,” amefafanua Secelela Balisidya.
Aidha, amesema kwamba, lengo kubwa la
mradi wa Green Voices ni kupaza sauti za akinamama kueneza ujuzi wao wa
kupambana na mabadiliko ya tabianchi ili jamii nzima ya Kitanzania iweze
kujifunza zaidi na kuzitumia mbinu hizo katika kupambana na mabadiliko ya
tabianchi.
Mradi huo unatarajiwa kutelekezwa kwa
mwaka mmoja ili kutoa fursa kwa akinamama kutoa ujuzi wao wa kupambana na
mabadiliko ya tabianchi na sauti zao kusikika, kwa sababu kazi wanazozifanya
kila siku za kilimo na utunzaji wa familia zinahusiana moja kwa moja na
mazingira hivyo kuyaelewa zaidi mazingira na jinsi ya kupambana na mabadiliko
ya tabianchi.
Malengo ya dunia.
Kilimo hai kinaendana na masuala
mtambuka ya mazingira pamoja na kukabiliana na uhaba wa chakula na kupunguza
umaskini kama inavyoelezwa kwenye Malengo Endelevu ya Dunia yaliyopitishwa
mwaka 2015.
Kwa mujibu wa malengo hayo, mataifa
mbalimbali yamekubaliana kuhakikisha yanatokomeza umaskini kwa namna zote
pamoja na kukomesha njaa na kupata uhakika wa usalama wa chakula na kuboresha
lishe kwa kuhimiza kilimo endelevu.
“Kilimo hai ni endelevu kwa sababu
unaweza kulima wakati wowote hivyo kinaweza kukabiliana na njaa na uhakika wa
chakula ni mkubwa, lakini pia kitasaidia familia kuongeza kipato kwa kuuza
ziada ya chakula kitakachozalishwa,” anasema Hamaro.
Lakini pia kwa kutumia kilimo hai,
lengo namba sita la dunia linaweza kutimia, kwani ni kilimo ambacho kinatumia
maji kidogo, hivyo kuhakikisha utunzaji mzuri wa vyanzo vya maji na matumizi
sahihi ya maji yaliyopo.
Aidha, kilimo hai pia kinaweza
kukidhi lengo namba 13 la dunia linalohimiza kupambana na mabadiliko ya
tabianchi na athari zake.
Sera ya Kilimo.
Kilimo hai ni sehemu ya mapendekezo
yanayotajwa kwenye Sera ya Taifa ya Kilimo ya mwaka 2013 ambayo inaendana na
Dira ya Taifa ya Maendeleo kuelekea mwaka 2025 kwa kuhimiza kilimo chenye tija
pamoja na utumiaji mzuri wa rasilimali zilizopo, hususan ardhi na maji.
Kwa maana nyingine, kuhamasisha
kilimo hai ni sehemu ya utekelezaji wa malengo, dhima na dira ya sera hiyo hasa
katika kipindi hiki ambacho dunia inakabiliwa na changamoto ya uharibifu wa
mazingira na mabadiliko ya tabianchi, ambayo serikali pia imeainisha mikakati
yake katika Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2007.
|
No comments:
Post a Comment