Wabunge wa Vyama vya Upinzani leo,May 31,2016,
wametoka nje kwa mara nyingine kupinga Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson kuendesha
vikao vya Bunge na kumwachia Bunge yeye na Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM).
Taarifa kutoka Bungeni zinaeleza kuwa,
wabunge wote wa upinzani wametoka nje kususia kikao cha Bunge ikiwa ni
kutekeleza azimio lao la kutokuwa na imani na Dk Tulia.
Baada tu ya kusomwa dua ya kufungua
Bunge asubuhi wabunge hao wametoka nje na kumwacha Dk. Tulia akiwa na wabunge
wa CCM pekee.
Hata hivyo Dk. Tulia ameanza kupaniwa
na wapinzani tangu jana. Ni kwa madai kuwa wapinzani hawamwamini tena.
Wameeleza kuwa, namna anavyoliongoza
Bunge, kauli zake na kuyumba kwake katika kusimamia haki kwa wabunge wa Ukawa
na wale wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumechochea kuonekana kuwa, nafasi
aliyonayo haimstahili.
Kutokana na hali hiyo, Freeman Mbowe
ambaye ni Kiongozi Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni jana aliahidi
kuanzisha mgomo dhidi ya Dk. Tulia.
Mbowe aliwaambia hayo wabunge wenzake
mjini Dodoma kwenye kikao cha dharura alichoitisha na kushirikisha waandishi wa
habari.
Alisema, Dk. Tulia ndio tatizo kuu la
Bunge la Kumi na Moja na kwamba, kiongozi huyo wa Bunge kila anapokuwa kwenye
kiti na kuongoza Bunge, mtafaruku hutokea.
“Nitapendekeza kuwa kila kikao cha
Bunge kinachoongozwa na Tulia Ackson, sote tutoke nje ili kuonesha kwamba
hatuna imani naye katika kuendesha shuguli za bunge,” Mbowe alisema jana.
Utekelezwaji wa kauli ya Mbowe
umeanza leo ambapo sasa Dk. Tulia amebaki na wabunge wa CCM pekee.
|
No comments:
Post a Comment