|
Waandishi
wa habari kutoka redio mbalimbali zinazorusha kipindi cha Walinde Watoto
wakijadiliana mara baada ya mafunzo ya waandishi wa habari kuhusu zana ya
mawasiliano kuzuia ukatili dhidi ya watoto yaliyofanyika Morogoro.
Mambo 9 muhimu ya kufahamu kuhusu
Ukatili kwa watoto
Tatizo la Ukatili dhidi ya watoto,
linaongezeka siku hadi siku, na kuleta athari mbalimbali za kimwili, kiakili,
(kisaikologia) na kiafya kwa watoto.
Watoto wanaumizwa, kubakwa, kunajisiwa,
kutelekezwa, kusafirishwa kibiashara na kufanyishwa kazi za hatari zinazoathiri
afya zao. Matendo haya ya kikatili hayakubaliki kabisa.
Yafuatayo ni mambo 9 muhimu ya
kufahamu kuhusu ukatili kwa watoto:
1. Aina
za ukatili .
Ukatili dhidi ya watoto upo wa aina
nyingi. Ukatili wa Kijinsia, ni vitendo au maneno yanayoweza kusababisha
madhara kwa mtu au kundi la watu kutokana na maumbile yao. (Mf: kuguswa bila
ridhaa, jaribio la kubaka/kubaka, kulazimisha kufanya ngono n.k).
Ukatili
wa Kimwili ni kama kupigwa, kusukumwa, au kutishiwa kuuwawa kwa
silaha. (Mf: kuonyeshwa kwamba hutakiwi, vipigo vya mara kwa mara) na Ukatili
wa Kiakili/Kisaikolojia, kutelekezwa, kubaguliwa, kutishwa.
(Mf: kuitwa majina mabaya, kunyimwa huduma za msingi, kufanyishwa kazi ngumu
n.k)
2. Wahusika
wa Ukatili dhidi ya watoto .
Utafiti wa
Ukatili dhidi ya Watoto Tanzania ulifanyika mwaka 2009 na uliongozwa na Kikosi
Kazi kinachojumuisha Sekta mbalimbali za Serikali, Asasi za Kiraia na Wadau wa
Maendeleo.
Katika utafiti huo ilionekana kuwa
ndugu wa karibu kama mjomba, baba, walezi na walimu ndio wanaosababisha
ukatili dhidi ya watoto. Kwa kuona hivyo, Serikali kwa kushirikiana na
wadau wengine wakaona umuhimu wa kuanzisha mpango wa kuelimisha jamii kuzuia
ukatili dhidi ya watoto.
3. Nini
kifanyike kupunguza ukatili kwa watoto.
Wananchi wote kwa ujumla wana jukumu
la kuhakikisha kwamba wanawalinda watoto. Wazazi / walezi wanapaswa kujua
watoto wao walipo na wanachokifanya kila wakati na kuhakikisha usalama wa
mahali watoto wanapopenda kutembea mara kwa mara. Watoto wapewe moyo kuripoti
vitendo mbalimbali vya ukatili.
4. Umuhimu
wa kituo cha huduma ya simu kwa mtoto - namba 116.
Kituo
cha huduma ya simu kwa mtoto ni muhimu katika mifumo ya ulinzi wa mtoto nchini.
Ni sehemu pekee ambayo mtoto au Mzazi/Mlezi anaweza kupiga simu na kutoa
taarifa za ukatili kwa siri na kupata huduma ya ushauri nasaha na rufaa kwa
msaada zaidi kwa mujibu wa tatizo lolote linalohusu ukatili dhidi ya watoto.
PIGA SIMU BURE kwenda namba 116 kutoa taarifa za ukatili dhidi ya watoto.
5. Uchumi
na Familia.
Familia zikiwa na hali ngumu ya
kiuchumi husababisha ugomvi kati ya wanafamilia na hii huweza kupelekea
kutelekezwa kwa watoto au kuwatenga watoto na familia, jambo ambalo litaongeza
hatari ya ukatili na unyanyasaji wa watoto.
Vilevile ugumu wa maisha ni
kisababishi cha watoto wanaofanya kazi katika umri mdogo, kuchuuza /kufanya
biashara ya watoto, mimba zisizotarajiwa na ndoa za utotoni. Hivyo basi ni
muhimu wazazi/walezi kujishughulisha na kazi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwa
wanachama wa vikundi ili waweze kuzalisha mapato ya kusaidia mahitaji ya
familia.
6. Madhara
ya adhabu kwa watoto
Kuna madhara mengi sana ambayo
yanaweza kuwapata watoto kutokana na kupewa adhabu mbalimbali. Adhabu huleta
hasira na chuki ambayo haisaidii kuleta mabadiliko ya tabia.
Kadri adhabu
inapokuwa kali zaidi ndivyo inavyopelekea mtoto kuwa na matatizo ya
kutojithamini, kuwa mhalifu, kupata magonjwa ya akili na kuwa na tabia ya
ukatili.
Adhabu mara nyingi haitoi mchango chanya kwa maendeleo ya mtoto.
7. Ishara
ambazo huonyeshwa na watoto waliofanyiwa ukatili.
Ni muhimu kwa wazazi/ walezi
kutambua ishara mbalimbali zinazoonyeshwa na mtoto aliyefanyiwa ukatili.
Ishara
hizo ni kama vile mtoto kutojiamini hata kama anafanya kitu sahihi anakua na
hofu kwa sababu tu anahisi anaweza kupigwa.
Mtoto kukataa kwenda sehemu ambazo
amezoea mf. shule, ukifuatilia kwa ukaribu utakuta kuna mtu anamfanyia ukatili
huko au njiani.
8. Wasikilize
kwa makini.
Ni muhimu kujijengea mazingira ya
kumsikiliza mtoto kwa makini. Unapofanya hivyo ni muhimu ajue kuwa
unamsikiliza, aidha kwa kutumia ishara bila maneno; kama vile kuashiria kwa
kichwa. Mtazame mara kwa mara kwa mtazamo wa kirafiki. Unaweza pia
kurudia aliyokwambia kwa maneno mengine.
9. Umuhimu
wa vyombo vya habari kupambana na ukatili
Kwa mujibu wa mwongozo wa vyombo vya
habari wa kuandika habari za watoto uliochapishwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT), “Watoto wanahitaji
uangalizi maalum wa kuwajali na kuwalinda.
Wakati wa kuandika habari za watoto,
vyombo vya habari vinapaswa kujenga taswira sahihi kwa watoto ili kuwaepusha
katika hatari ya kuadhibiwa au kunyanyapaliwa. Watoto ni binadamu wanaohitaji
kutambuliwa, kupewa hadhi, utu, heshima na zaidi ya yote kulindwa.
Kutokana na
ukweli huo, uelewa, umakini na weledi wa uandishi wa habari zinazowahusu wao
kwa kuzingatia hali yao na mahitaji yao ni muhimu. Kimsingi vyombo vya habari
vinatakiwa kuboresha uandikaji wa habari za watoto na wakati huo huo kulinda
usalama wao kimwili na kihisia/jaziba. “
Mambo haya yameibuka katika mafunzo
ya waandishi wa habari kuhusu zana ya mawasiliano kuzuia ukatili dhidi ya
watoto yaliyofanyika Morogoro.
Mafunzo hayo ambayo yameandaliwa na
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na Watoto pamoja na shirika
la watoto duniani (UNICEF) na kampuni ya True Vision Production yamehudhuriwa
na waandishi wa habari kutoka redio mbalimbali zinazorusha kipindi cha Walinde
Watoto.
Redio hizo ni pamoja na Kitulo FM,
Radio Maria, Radio Faraja, Boma Hai Radio, Uplands FM, Radio Sauti ya Quran,
Kwizera FM na Country FM.
Nyingine ni Bomba FM, Zenji FM, ZBC,
Radio Huruma, Ice FM, Radio Jamii Kilosa, TBC Taifa, Dodoma FM, Fadeco Radio,
Radio Victoria na Best FM.
Waandishi wa habari wametakiwa
kushirikiana na serikali na wadau wengine kuhakikisha kuwa haki za watoto
zinatekelezwa hapa nchini.
Ni wajibu wa kila mwananchi
kuhakikisha kuwa anawalinda watoto na kuwasadia kukua na kufikia ndoto zao
katika jamii.
|
No comments:
Post a Comment