|
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amefanya ziara yake ya
kwanza nje ya nchi leo tarehe 06 April, 2016 kwa kutembelea nchi jirani ya
Rwanda, ambapo yeye na Mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Rwanda Mheshimiwa Paul
Kagame wamefungua Kituo cha Pamoja cha Utoaji wa Huduma za Mpakani (One Stop
Border Post) na Daraja la Kimataifa la Mto Rusumo katika Mpaka wa Tanzania na
Rwanda.
Rais
Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli, ameingia nchini
Rwanda kwa usafiri wa magari akitokea nyumbani kwake Lubambangwe, katika kijiji
cha Mlimani, Wilaya ya Chato Mkoani Geita ambako alikuwa mapumziko tangu tarehe 29 Machi, 2016.
Katika eneo
la Rusumo, Rais Magufuli na Rais Kagame kwanza wamefungua majengo ya Kituo cha
Pamoja cha Utoaji wa Huduma za Mpakani kilichopo upande wa Tanzania,kisha
wakafungua daraja la mto Rusumo, na baadaye wakafungua Majengo ya Kituo cha
Pamoja cha Utoaji wa Huduma za Mpakani kilichopo upande wa Rwanda.
Mradi huu wa
ujenzi wa Kituo cha Pamoja cha utoaji wa Huduma za Mpakani cha Rusumo,
umehusisha ujenzi wa majengo ya mamlaka ya Mapato katika pande zote mbili na
daraja lenye urefu wa mita 80 na upana wa mita 9.5, na umegharimu shilingi
Bilioni 61.4 zilizotolewa kwa ufadhili wa serikali ya Japan kupitia shirika
lake la JICA.
Akizungumza
katika sherehe ya ufunguzi wa mradi huo Rais Magufuli ameishukuru Japan kwa kutoa fedha za kuwezesha
utekelezaji wa mradi huo na ametoa wito kwa wafanyabiashara wa Rwanda kupitisha
mizigo yao Tanzania kupitia mpaka huo, pamoja na kuitumia bandari ya Dar es
salaam.
Dkt.
Magufuli amewasihi wananchi wa Rwanda na wanajumuiya ya Afrika Mashariki kwa
ujumla, kushirikiana kibiashara kwa kutumia fursa zilizopo huku akibainisha
kuwa Tanzania imeanza juhudi za kuimarisha miundombinu yake ya barabara na
kujenga reli ya kati, ambayo tayari washirika 13 wameonesha nia ya kufanikisha
ujenzi huo.
Aidha, Rais
Magufuli amewaonya maafisa forodha na vituo vya ukaguzi kuacha mara moja tabia
ya ucheleweshaji wa upitishaji wa mizigo, na amesema serikali imeshaamua kuwa
barabara ya Rusumo hadi Dar es salaam itakuwa na vituo vitatu ambavyo ni
Rusahunga, Singida na Vigwaza ili magari yatumie muda wa siku 3 badala ya
kutumia siku zaidi ya 10.
Kwa upande
wake Rais Paul Kagame wa Rwanda ambaye ameongozana na mkewe Mama Janeth Kagame,
pamoja na kuishukuru Japan kwa kufadhili mradi huo amesema Tanzania na Rwanda
zina kila sababu ya kushirikiana kiuchumi na ameongeza kuwa ni matumaini yake
kujengwa kituo hicho kutaongeza biashara na idadi ya watu wanaovuka daraja
kutoka 2,000 wa sasa hadi watu zaidi ya 15,000 kwa siku.
Akiwa Rwanda
Rais, Magufuli amefanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Paul Kagame na hapo
Kesho, Rais Magufuli atashiriki maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 22 ya mauaji
wa Kimbari yaliyotokea mwaka 1994 ambapo watu takribani milioni 1,000,000
waliuawa.
Gerson
Msigwa
Kaimu
Mkurugenzi wa Mawasiliano,
IKULU
Kigali
06 April,
2016. |
No comments:
Post a Comment