|
Waziri wa
Fedha na Mipango wa Tanzania (PICHANI), Dk. Philip Mpango, amewasilisha Kiwango
na Ukomo wa Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2016/2017, akisema itakuwa Sh.
trilion 29.53.
Kati ya
fedha hizo, mapato ya ndani ni Sh. trilioni 17.79 ambazo kati ya hizo, Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA) inatarajiwa kukusanya Sh. trilioni 15.1 na mapato
yasiyo ya kodi yakiwa Sh. trilioni 2.69.
Hata hivyo,
bajeti hiyo kubwa katika historia ya Tanzania na yenye kuleta matumaini,
inaelezwa na wachambuzi wa masuala ya uchumi na kodi kuwa, itawalazimu
Watanzania kuvuja jasho jingi na kukamuliwa katika nyanja ya kodi ili kuongeza
mapato ya serikali iweze kutekelezeka kwa ufanisi.
Wachambuzi
hao wanaeleza kuwa, ili serikali iweze kufikia kiwango cha bajeti hiyo,
inapaswa kufanya jitihada kubwa na kuja na ubunifu wa kubuni vyanzo vipya vya
mapato, hali ambayo kwa kiasi kikubwa itabebwa na wananchi ambao watalazimika
kulipa kodi nyingi na baadhi ya bidhaa kuongezewa kodi ili kuziba nakisi ya
wastani wa Sh. trilioni 2 itakayokuwapo kutokana na mamlaka hiyo kwa sasa
kukusanya wastani wa Sh. trilioni 1.1 kwa mwezi.
Kiwango
hicho cha makusanyo ya mwezi ambacho kwa uhai wa bajeti hiyo wa mwaka mmoja
wenye miezi 12, hakiwezi kufikisha Sh. trilioni 29.53 zinazopangwa kutumika
katika kipindi chote cha mwaka mzima, hivyo kuhitaji jitihada za ziada katika
ukusanyaji mapato.
WAHISANI
WAONGEZA UGUMU.
Marekani
imeshatangaza kuifuta Tanzania kwenye nchi wanachama wa Shirika la Changamoto
za Milennia (MCC) ,hivyo nchi kukosa Sh. trilioni 1.03 ilizokuwa ipewe na mfuko
huo kusaidia ujenzi wa barabara za pembezoni na kusambaza umeme vijijini.
Umoja wa
Ulaya EU na ipo kwenye hatihati ya kutoa Sh. trilioni 1.56, ukiendelea kusubiri
hatma ya mazungumzo na hali ya Zanzibar.
Pia baadhi
ya mawaziri wa Uingereza nao wanaishauri serikali ya nchi yao kuifutia Tanzania
msaada wa Sh. bilioni 622, kutokana hali ya Zanzibar.
Wizara ya
Fedha na Uchumi pia imeshatangaza wahisani 10 kati 14 wanaosaidia bajeti kuu ya
serikali kujitoa, ambapo Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk. Servacius Likwelile,
alisema waliobaki ni Benki ya Dunia (WB), Umoja wa Nchi za Ulaya (EU), Dernmark
na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB).
Hatua hiyo
ya wahisani ni pigo kubwa kwa bajeti ya serikali ya mwaka huu, kwani mchango
wao katika bajeti hiyo utakuwa umepungua.
Hata hivyo,
Rais Magufuli inaonekana ameliona hilo na mara kadhaa amekuwa akiisisitiza TRA
kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato, kubana mianya ya ukwepaji kodi na
kukuwajibisha wanaotumia vibaya fedha za umma ili nchi iweze kujitegemea
kimapato.
Aidha, Dk.
Mpango alinukuliwa na vyombo vya habari akisema walishaona dalili ya wahisadi
kutotoa fedha na kwamba serikali imeandaa bajeti bila ya kutegemea fedha hizo.
Wahisani
wengine ambao wamekuwa wakisaidia bajeti kuu ya serikali ni Uingereza, Canada,
Finland, Ujerumani, Ireland, Japan, Norway na Sweden.
Itakumbukwa
kuwa, kwenye bajeti ya serikali ya 2014/15 wahisani walitarajiwa kuchangia Sh.
trilioni 1.09, lakini wengi walikataa kutoa fedha kutokana na kashfa ya akaunti
ya Tegeta Escrow.
MCHANGANUO
WA BAJETI.
Dk. Mpango
akisoma hotuba yake mbele ya wabunge wote jijini Dar es Salaam jana, alisema
makusanyo yasiyo ya kodi yanatarajiwa kuwa Sh. trilioni 2.69, huku makusanyo ya
halmashauri zote yakiwa Sh. bilioni 665.41.
Alisema
serikali inatarajia kupata Sh. trilioni 3.6, ikiwa ni misaada ya wahisani
kwenye bajeti kuu ya serikali na miradi mbalimbali wanayoifadhili moja kwa
moja.
Kwa upande
wa mikopo ya masharti ya kibiashara, Dk Mpango alisema serikali inatarajia
kukopa Sh. trilioni 2.1 kutoka vyanzo vya nje na Sh. trilioni 5.37 kutoka
vyanzo vya ndani.
DENI LA
TAIFA
Dk. Mpango
alisema mpaka kufikia Februari, mwaka huu, deni la taifa lilikuwa ni dola za
Marekani bilioni 19.93 ambazo ni sawa na Sh. trilioni 43.5.
AKIBA FEDHA
ZA KIGENI.
Kwa upande
wa akiba ya fedha za kigeni, alisema mpaka sasa ni dola za Marekani bilioni
4.09 ambazo ni sawa na Sh. trilioni 8.936, kiasi ambacho kin awe za kununua
vitu kutoka nje ya nchi kwa miezi minne.
Kwa upande
wa thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani, alisema imeendelea kupungua
kutoka Januari 2015, ambapo dola moja ilikuwa Sh. 1,754.7 mpaka Februari, 2016
ambapo imekuwa Sh. 2,189.1.
MATUMAINI.
Hata hivyo,
pamoja na hali hiyo, bajeti hiyo ambayo imejikita kwenye kuendeleza viwanda vya
kati na vikubwa, licha ya kuleta hofu ya kuwabana zaidi wananchi, inaweza kuwa
faraja kwao kwani kwa mara ya kwanza fedha za maendeleo zitakuwa asilimia 40 ya
bajeti yote.
Bajeti hiyo
ambayo itakuwa ya kwanza kwa serikali ya Rais Magufuli, inazidi ile ya mwisho
ya Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, iliyokuwa ya Sh. trilioni 22.5, ambayo hata
hivyo utekelezaji wake ulikuwa hafifu kutokana na kiasi kikubwa cha fedha za
maendeleo kutowasilishwa licha ya kuwa umebaki mwezi mmoja kukamilika kwa mwaka
wa fedha wa 2015/2015.
Mbali na bajeti hiyo ya mwisho ya Rais Kikwete ambayo
ilijikita zaidi kufanikisha uchaguzi mkuu wa Oktoba 25,2015, bajeti ya mwaka 2014/2015
ilikuwa Sh. trilioni 19.85 na ya mwaka 2013/2014 ilikuwa Sh. trilioni 18.2.
|
No comments:
Post a Comment