![]() |
|
HOTUBA YA MHE. KASSIM MAJALIWA MAJALIWA (MB),
WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA KUHITIMISHA
SHUGHULI ZA MKUTANO WA PILI WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
TAREHE 05 FEBRUARI, 2016.
I: UTANGULIZI
(a) Masuala ya Jumla
Mheshimiwa Naibu Spika,
1. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mungu kwa
kutujalia afya njema na uwezo katika kutenda yote yaliyo mema. Tumekuwepo hapa
kwa takriban siku 11 katika shughuli za Mkutano wa Pili wa Bunge lako Tukufu.
Ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa Rehema kwa kutufikisha
salama siku ya leo.
2. Tumekutana hapa tukiwa tumeshuhudia uundwaji
wa Serikali unaoendelea ambapo Mheshimiwa Dkt John Pombe Magufuli, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amefanya uteuzi wa Baraza jipya la Mawaziri
ambao ni Waheshimiwa Wabunge wenzetu. Niruhusu nitumie nafasi hii ya awali
kuwapongeza Mawaziri na Naibu Mawaziri wote ambao wameteuliwa kushika nyadhifa
mbalimbali katika Serikali ya Awamu ya Tano.
(b) Chaguzi Mbalimbali
Mheshimiwa Naibu Spika,
3. Katika Mkutano huu, tumeweza kufanya Chaguzi
za Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge. Vilevile,
tumefanya chaguzi za Wenyeviti wa Bunge letu na Wajumbe wa kutuwakilisha katika
Taasisi mbalimbali za Kitaifa na Kimataifa. Kwa vile orodha ni ndefu, napenda
nitumie nafasi hii kuwapongeza kwa dhati kabisa na kwa ujumla wao wote
waliogombea nafasi hizo na kushinda. Ni matarajio yangu kwamba tutatumia nafasi
hizo vizuri katika kuleta ushirikiano, mshikamano na kufanya kazi pamoja kama
Wawakilishi wa Wananchi na kutekeleza majukumu yetu kama Wabunge ndani ya Bunge
hili.
(c) Maafa na
Ajali
Mheshimiwa Naibu Spika,
4. Tarehe 27 Januari, 2016 wakati Bunge lako
Tukufu likiendelea na Vikao, Waheshimiwa Wabunge walipewa taarifa ya
kusikitisha ya kuzama kwa Kivuko cha Kilombero, ambapo katika tukio hilo watu
walipoteza maisha na wengine kujeruhiwa. Aidha, mali za abiria zimepotea.
Wakati huo huo, mvua zinazoendelea kunyesha nchini katika baadhi ya maeneo
zimesababisha mafuriko, vifo, uharibifu wa mali ikiwemo mazao na miundombinu.
Katika baadhi ya maeneo, mvua hizi zimesababisha njaa na athari nyingine kwa
jamii.
5. Pamoja na maafa ya mvua na mafuriko, wapo
wananchi waliofariki na wengine kupata ulemavu katika ajali mbalimbali za
vyombo vya usafiri. Nitumie fursa hii kuwapa pole wote waliopoteza ndugu, jamaa
na marafiki katika matukio yote hayo. Aidha, napenda kuwatakia afya njema wote
waliopata majeraha. Kwa wale wote waliopoteza maisha tunawaombea Roho zao
zilale mahali pema peponi - Amina.
6. Kuhusu uharibifu wa miundombinu, tunazo
taarifa za uharibifu mkubwa wa Miundombinu katika maeneo kadhaa. Napenda
kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba Serikali itafanya kila liwezekanalo
kurekebisha miundo mbinu ya barabara iliyoharibika. Tunatambua gharama kubwa
inayohitajika, lakini ni wajibu wetu kama Serikali kuhakikisha Wananchi
wanapata huduma muhimu hasa za mawasiliano kati ya eneo moja na jingine.
(d) Maswali
Mheshimiwa Naibu Spika,
7. Leo tunahitimisha Mkutano wetu wa Pili wa
Bunge tukiwa tumefanya shughuli mbalimbali ndani ya Bunge letu. Katika Mkutano
wetu, Waheshimiwa Wabunge wamepata fursa ya kuuliza maswali ya kawaida na yale
ya papo papo kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu. Jumla ya maswali115 ya
msingi na 307 ya nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na
Serikali.
(e) Mjadala wa Hotuba ya Rais
Mheshimiwa Naibu Spika,
8. Katika Mkutano huu moja ya agenda iliyochukua
nafasi kubwa ni Hoja ya Serikali ya kujadili Hotuba ya Mheshimiwa Dkt. John
Pombe Maufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hoja hiyo
tuliihitimisha vizuri na kwa mafanikio makubwa. Kazi kubwa iliyoko mbele yetu
ni kutekeleza yale tuliyokusudia kama wajibu wetu. Napenda kuwapongeza tena
Waheshimiwa Wabunge wote kwa kushiriki katika mjadala wa Hotuba hiyo vizuri.
Nichukue tena nafasi hii kuliahidi Bunge lako Tukufu kwamba michango ya
Waheshimiwa Wabunge na maoni yao yatazingatiwa kwa utekelezaji.
II: MPANGO WA TAIFA WA MAENDELEO
Mheshimiwa Naibu Spika,
9. Katika Mkutano huu wa Bunge, Waheshimiwa
Wabunge wamepata fursa ya kujadili na kuidhinisha Mapendekezo ya Mpango wa
Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali katika mwaka wa Fedha 2016/2017.
Vilevile, Bunge limejadili na kutoa maoni na ushauri katika mwongozo wa kuandaa
Mpango na Bajeti ya Serikali katika mwaka wa Fedha, 2016/2017. Kipekee, naomba
nimshukuru Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Isdor Mpango(Mb) na Naibu
wake Dkt. Ashatu Kachwamba Kijaji (Mb.) pamoja na Waheshimiwa Mawaziri wa
Wizara za Kisekta kwa ufafanuzi mzuri walioutoa wakati wa kuhitimisha hoja hii.
Aidha, napenda kutumia fursa hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa
michango yao mizuri, maoni na ushauri ambao Serikali itauzingatia katika
kukamilisha maandalizi ya Mpango na Bajeti ya mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika,
10. Naomba nami uniruhusu nitoe maelezo mafupi ya
msisitizo katika maeneo machache yaliyopata michango mingi kutoka kwa
Waheshimiwa Wabunge waliochangia hoja ya Serikali ya mapendekezo ya Mpango wa
Taifa wa Maendeleo. Waheshimiwa Wabunge wengi wamesisitiza kuhusu umuhimu wa
Serikali kuongeza uwajibikaji katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali na
kuimarisha udhibiti wa matumizi ya Serikali. Aidha, Waheshimiwa Wabunge
wameishauri pia Serikali kuweka kipaumbele cha ujenzi wa Reli mpya ya Kati,
kujenga uchumi wa Viwanda, kuanza na kusimamia ujenzi na Mitambo ya kuchakata
gesi asilia (LNG) na Kiwanda cha Mbolea Mkoani Lindi, kuongeza kasi ya
usambazaji wa umeme Vijijini, ujenzi wa Bandari Mtwara, kutatua changamoto
zinazowakabili Wakulima na Wafugaji pamoja na Wachimbaji Madini.
Vilevile, kuweka mikakati thabiti ya utekelezaji wa Miradi ya
Sekta za Elimu, Afya, Maji na huduma kwa wenye Ulemavu na pia kuzingatia
utawala bora. Serikali inatambua kuwa maeneo haya ni muhimu sana katika kujenga
uchumi imara na endelevu na pia kuondoa umasikini. Hivyo, itazingatia sana
ushauri huu mzuri uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Naibu Spika,
11. Naomba nitumie fursa hii kumpongoeza
Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa umahiri mkubwa na umakini
aliouonesha ikiwa ni mwanzo mzuri wa kuongoza Serikali ya Awamu ya Tano.
Mheshimiwa Rais ameonesha kasi kubwa na dhamira ya dhati ya kuwatumikia
Watanzania katika kujenga uchumi imara, unaokuwa na endelevu. Waheshimiwa
Wabunge wengi watakubaliana nami kwamba Serikali ya Awamu ya Tano katika
kipindi chake cha mwanzo cha siku 100, imeonesha dhahiri nia ya dhati ya
kuhakikisha kwamba makusanyo ya mapato yetu yanaongezeka. Jitihada hizo za
kuongeza makusanyo ya mapato ya Serikali zimefafanuliwa vizuri kwenye Hotuba ya
Waziri wa Fedha na Mipango. Serikali itaendelea na mikakati yake ya kuongeza
Mapato yake na kudhibiti mianya ya kukwepa kodi. Ni matumaini yangu kuwa
Waheshimiwa Wabunge, Wafanyabiashara na Wananchi wote wataunga mkono dhamira
hiyo njema ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika,
12. Kuhusu matumizi, tayari Serikali imeanza
kuchukua hatua thabiti za kudhibiti matumizi yasiyo na tija katika Wizara,
Idara za Serikali zinazojitegemea na Taasisi zote za Umma pamoja Mikoa na
Mamlaka za Serikali za Mitaa. Lengo la hatua zinazochukuliwa ni kuhakikisha
kwamba Serikali inasimamia kwa umakini matumizi ya fedha za Umma ili zitumike
ipasavyo kwa malengo yaliyokusudiwa. Hatua hizi zitaimarishwa zaidi katika mwaka
ujao wa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika,
13. Kama nilivyoeleza awali hoja nyingi za msingi
zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge kuhusu Mpango wa Taifa, zimefafanuliwa
vizuri na Waheshimiwa Mawaziri wa Kisekta na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango.
Naomba niwaahidi kuwa tutazizingatia katika mchakato wa maandalizi ya Mpango na
Bajeti ya Serikali ya mwaka 2016/2017, kwa kadri itakavyowezekana. Waheshimiwa
Wabunge watashirikishwa kikamilifu katika mchakato huo kupitia Kamati
mbalimbali za Bunge. Serikali itafarijika sana kupata maoni na ushauri zaidi
ili tuweze kuboresha mipango yetu ya muda mfupi na muda mrefu.
III: SEKTA YA KILIMO
Uzalishaji wa Mazao ya Chakula 2014/2015 na
Upatikaji wa Chakula 2015/2016
Mheshimiwa Naibu Spika,
14. Hali ya chakula kwa mwaka
2015/2016 katika maeneo mengi ya nchi imeendelea kuwa ya kuridhisha kufuatia
mavuno mazuri yaliyopatikana msimu wa kilimo wa 2014/2015. Takwimu za Wizara ya
Kilimo, Mifugo na Uvuvi zinaonesha kuwa albaki kutoka msimu uliopita nchi ilikuwa
na ziada ya chakula licha ya kuwepo kwa maeneo machache ambayo hayakuwa na
chakula.
Mheshimiwa Naibu Spika,
14. Kutokana na uzalishaji wa mazao
ya chakula kwa msimu wa 2014/2015 kuwa Tani milioni 15.5 na mahitaji ya chakula
kwa mwaka 2015/2016 kuwa Tani milioni 12.9 hivyo nchi
imejitosheleza kwa chakula kwa ziada ya Tani milioni 2.5 sawa
na asilimia 120. Napenda kuwahakikishia Watanzania kuwa Serikali
itaendelea kuhudumia maeneo yote yenye uhaba wa chakula.
Mheshimiwa Naibu Spika,
15. Pamoja na Taifa kuwa na ziada
ya asilimia 120 ya chakula, tathmini ya hali ya chakula nchini
inaonesha kuwa kuna Halmashauri 69 katika mikoa 18 nchini
yenye maeneo yenye dalili za upungufu wa chakula. Maeneo hayo yapo katika Mikoa
ya Dodoma, Shinyanga,
Lindi, Singida, Tabora, Arusha, Geita, Kilimanjaro, Manyara, Mara, Tanga,
Simiyu, Mwanza, Morogoro, Iringa, Njombe, Mtwara, na Pwani.
Mheshimiwa Naibu Spika,
16. Ili kukabiliana na hali ya
uhaba wa chakula katika maeneo hayo, Serikali inaendelea kutoa chakula katika
maeneo hayo ambapo jumla ya Tani 23,871.6 za chakula
zilitengwa kwa ajili hiyo. Hadi kufikia tarehe 17 Januari, 2016, jumla ya Tani
11,860.8 zilikuwa zimechukuliwa toka Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya
Chakula (NFRA) kwenda kwenye Halmashauri za Wilaya zenye upungufu wa chakula
kwa ajili ya usambazaji. Natoa wito kwa Halmashauri ambazo hazijachukua mgao
wao kufanya hivyo mara moja ili Wananchi katika maeneo hayo wasizidi
kuathirika.
Mheshimiwa Naibu Spika,
17. Sambamba na utoaji wa chakula cha msaada, Serikali kupitia
Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) inaendelea kutoa mahindi katika
maghala ya Songea na Sumbawanga kwa ajili ya kuuzwa kwa wafanyabishara wa
nafaka walioidhinishwa na mikoa yenye uhaba wa Chakula. Lengo ni kuongeza
upatikanaji wa chakula na kukabiliana na kasi ya kupanda kwa bei ya vyakula
katika maeneo hayo. Chini ya utaratibu huo, vibali vimeshatolewa kwa
wafanyabiashara wa Mikoa 17, vya kununua jumla ya Tani
77,166. Hadi kufikia tarehe 18 Januari, 2016 jumla ya Tani
56,817.5 kati ya Tani 64,817.3 zilizokuwa zimelipiwa kutoka NFRA
tayari zilikuwa zimechukuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika,
18. Ili kuongeza na kuimarisha uhakika na usalama wa chakula
hapa nchini, Serikali imelenga kujenga maghala 275kwa awamu katika
sehemu zenye uzalishaji mkubwa wa zao la mahindi ambapo hadi sasa jumla ya
maghala 125yanaendelea kujengwa na kukarabatiwa katika maeneo hayo.
Aidha, Serikali kwa kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA)
inaendelea kujenga maghala ya kimkakati kwa ajili ya kuhifadhi akiba ya Taifa.
Kwa sasa ghala moja lenye uwezo wa kuhifadhi Tani 5,000 limeshajengwa Wilayani Mbozi Mkoani Mbeya. Aidha, Serikali
imepata mkopo wenye masharti nafuu kutoka Serikali ya Poland ambao utawezesha
kujenga vihenge vya kisasa (silos) vyenye uwezo wa kuhifadhi Tani
160,000 na maghala yenye uwezo wa kuhifadhi Tani 90,000.
Mheshimiwa Naibu Spika,
19. Pamoja na hatua zinazochukuliwa
na Serikali, ninawataka viongozi wa Mikoa, Wilaya na atendaji katika
Halmashauri zote Nchini kuwahamasisha Wananchi kutumia vizuri mvua zinazonyesha
nchini kote kulima kwa bidii ili kuweza kuvuna na kujiwekea akiba ya chakula
cha kutosha kwa ajili ya kaya zao wakati wote wa mwaka. Aidha, wawahamasishe
wafanyabiashara na wadau wengine kusaidia Serikali kuchukua chakula kutoka
maeneo yenye ziada na kupeleka katika maeneo yenye upungufu. Ni imani yangu
kwamba tukizingatia maelekezo haya pamoja na juhudi za Serikali zilizooneshwa,
tatizo la uhaba wa chakula nchini litapungua, kama siyo kumalizika kabisa.
IV: MIFUGO:
Hatua zilizochukulwa na Serikali katika
Kushughulikia Migogoro ya Wakulima na Wafugaji;
Mheshimiwa Naibu
Spika,
20. Migogoro ya ardhi hapa nchini ina sura nne;
migogoro kati ya Wakulima na Wafugaji, mgogoro kati ya Wananchi na Wawekezaji;
migogoro kati ya Wananchi na Serikali na migogoro kati ya Mamlaka moja na
Mamlaka nyingine ndani ya Serikali. Migogoro hii imeenea nchi nzima kutokana na
sababu mbalimbali ikiwepo kuongezeka kwa matumizi ya rasilimali ya ardhi.
21. Serikali kwa kushirikiana na
Mamlaka za Serikali za Mitaa na Tume ya Taifa ya Matumizi ya Ardhi kwa kutumia
Sheria ya Ardhi ya Vijiji Na. 5 ya mwaka 1999 na Sheria
ya matumizi ya Ardhi Na. 6 ya mwaka 2007, hadi kufikia mwezi Juni 2015 jumla ya
Vijiji 620 katika Wilaya 81 kwenye
Mikoa 22 zimeweza kutenga Hekta Milioni 1.9 kwa
ajili ya Wafugaji. Wito wangu kwa Wananchi na Wadau wa Kilimo na Ufugaji
nawaomba kutunza na kuendeleza maeneo haya ili yaweze kutumika kwa mujibu wa
malengo yaliyopangwa.
Mheshimiwa Naibu Spika,
22. Nitumie fursa hii pia
kulijulisha Bunge lako Tukufu kuhusu hatua ambazo Serikali imechukua
kukabiliana na migogoro ya Wakulima na Wafugaji iliyotokea katika Mikoa ya
Morogoro (Wilaya za Mvomero na Kilombero) na Manyara (Wilaya ya Kiteto). Katika
kushughulikia tatizo hili, Jumla ya Vijiji 53 vimeainisha
maeneo kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo Kilimo na Ufugaji. Aidha, jumla
ya Mashamba Pori Manane (8) yameanishwa na orodha yake imewasilishwa kwa
Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hatua za kufutiwa hati
miliki na hatimaye kufanya utaratibu wa kuyatumia kwa ufugaji. Ni matarajio
yangu kuwa maeneo haya yatapunguza sana kwa kiasi kikubwa matatizo ya uhaba wa
malisho hapa Nchini. Wito wangu niwatake Viongozi wa Vijiji kusimamia vizuri
matumizi ya maeneo yatakayotolewa kwa ajili ya malisho ili tatizo hili la
kukosa maeneo ya malisho lisijirudie tena.
Mheshimiwa Naibu Spika,
23. Bado kuna mgogoro wa Wafugaji
na Wakulima katika Bonde Oevu la Kilombero ambao umetafutiwa ufumbuzi kwa
kuweka alama (branding) mifugo yote katika eneo hili ambapo jumla ya
Mifugo 52,780 ilipata usajili wa Wilaya. Aidha, jumla ya
Mifugo 24,586 imeondolewa katika eneo la Bonde la Kilombero.
Kwa kuzingatia hatua zilizochukuliwa na Serikali Wananchi wanapaswa kufuata
Sheria na kuhakikisha Mifugo hairudi tena katika maeneo yaliyokatazwa na kwamba
maeneo haya yanahifadhiwa kwa mujibu wa Sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika,
24. Mgogoro wa Wafugaji na Wakulima
katika maeneo ya Kiteto ni wa muda mrefu na kwa bahati mbaya sana umeleta
madhara makubwa kwa maisha ya Wanadamu na uharibifu wa mali. Napenda
kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba Tume iliyoundwa na aliyekuwa Waziri Mkuu
(Mstaafu) Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda ikiongozwa na Askofu Amos Mhagachi
imekamilisha hatua muhimu ya kuleta maelewanao na maridhiano katika pande
zilizoathirika na mgogoro huo. Kwa sasa hali imeendelea kuimarika na
tunaendelea kufuatilia kuhakikisha inakuwa shwari kwa muda wote.
25. Vilevile tarehe 29 Januari 2016
nimekutana na Viongozi wa Serikali, Halmashauri ya Wilaya na Chama kutoka
Wilaya ya Kiteto hapa Dodoma ambapo nilipata fursa ya kupokea taarifa ya Tume
niliyoitaja hivi punde. Nimeiagiza Tume kuendelea na hatua iliyobakia ili
kurejesha utulivu na amani kwa wananchi wa Kiteto. Hata hivyo, nimepanga
kufanya ziara Wilayani Kiteto katika siku chanche zijazo ili niweze kukutana na
Wananchi walioathirika na mgogoro huu na ikiwa ni pamoja na kujionea hali
halisi Wilayani Kiteto ili tuweze kutatua migogoro yote. Wito wangu kwa ndugu
zangu wa Kiteto ni kuwaomba waendelee kuvumilia wakati jitihada za Serikali
katika kutatua migogoro hiyo inaendelea.
V: UTEKELEZAJI WA ELIMU MSINGI BILA
MALIPO
Mheshimiwa Naibu Spika,
26. Tangu Mheshimiwa Rais Dkt. John
Pombe Magufuli atoe maaelezo ya utekelezaji wa elimu ya msingi bila malipo,
kumekuwa na umuhimu wa kutoa elimu na ufafanuzi zaidi juu ya utekelezaji wa
agizo la elemu bila malipo kwa Watanzania kuanzia darasa la awali hadi Kidato
cha Nne katika Shule za Umma. Hii ni hatua ya Serikali katika kuhakikisha uwepo
wa fursa ya elimu bora kwa wote kwa kuwapunguzia mzigo wazazi na walezi
kugharamia au kuchangia upatikanaji wa elimumsingi.
Katika mpango huu, Serikali imedhamiria kuhakikisha kuwa
mwanafunzi atasoma kuanzia darasa la awali hadi kidato cha Nne bila ya wazazi
na walezi kulipa ada ya shule, gharama za mitihani na michango mbalimbali. Hata
hivyo, yapo majukumu ambayo yataendelea kutekelezwa na wazazi na walezi wote
ambayo ni pamoja na kununua sare za shule na michezo, madaftari, kalamu na
chakula kwa wanafunzi wa shule za kutwa zilizojiwekea utaratibu huo. Maeneo
mengine ni kulipia nauli ya kwenda na kurudi shule, na mahitaji mengine kama
kununua godoro, shuka na vifaa vya usafi binafsi. Mzazi au mlezi anao wajibu wa
kugharamia matibabu ya mtoto wake.
Mheshimiwa Naibu Spika,
27. Napenda nitumie nafasi hii
kuwaomba Waheshimiwa Wabunge wote tushirikiane katika juhudi za kuunga mkono uamuzi
wa Serikali kuhusu elimu bila malipo. Aidha, nawaomba wote kwa ujumla wetu
kushirikiana kuwaelimisha Wananchi wetu kuhusu utaratibu huu na wajibu wa kila
mmoja wetu kama Mzazi/Mlezi, Serikali na jamii kuhusu utekelezaji wa zoezi
hili. Nia yetu ni kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata fursa ya kupata elimu
bora kwa mtoto mwenye umri wa kwenda Shule na wote walioko katika Shule za
Msingi na Sekondari. Napenda pia kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba kama
tulivyokwisha sema suala la ada elekezi inafanyiwa kazi na ikikamilika Wananchi
watajulishwa kuhusu utaratibu huo. Vikao vya pamoja baina ya Serikali na wadau
vitaanza hivi karibuni.
Mheshimiwa Naibu Spika;
28. Katika kutekeleza mpango huu,
Serikali imetenga fedha shilingi Bilioni 131.4 kuanzia mwezi
Disemba 2015 hadi Juni, 2016, kuhudumia wanafunzi wa bweni kwa chakula, kufidia
gharama za ada za mitihani, ada ya shule na kutoa fedha za uendeshaji wa shule
(Capitation Grants). Aidha, kupitia Waraka wa Elimu Na. 5 wa
mwaka 2015, Serikaliimefuta michango yote iliyokuwa inachangishwa shuleni kwa
idhini ya Kamati na Bodi za Shule.
Mheshimiwa Naibu Spika,
29. Tunatambua katika utekelezaji
wa zoezi hili zipo changamoto zilizojitokeza. Kwa mfano, baadhi ya shule zenye
wanafunzi wachache kupata fedha kidogo sana kwa kuwa ugawaji wa fedha
unazingatia idadi ya wanafunzi. Lakini pia zipo changamoto katika kutoa chakula
cha mchana kwa wanafunzi wa kutwa na uendeshaji wa Hosteli ambazo wazazi na
walezi au jamii walikuwa wanachangia fedha za chakula. Serikali inaendelea kuzifanyia
kazi changamoto hizo zilizojitokeza katika utekelezaji wa mpango huu ikiwemo
uelewa wa jamii na wadau kuhusu mpango mzima kwa ujumla wake.
VI: HUDUMA YA MIKOPO KWA WANAFUNZI WA ELIMU YA
JUU
Mheshimiwa Naibu Spika,
30. Serikali imeendelea kutoa
huduma ya mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa mwaka wa masomo 2015/2016
kwa kuzingatia Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Namba 9 ya
mwaka 2004 (Kama ilivyorekebishwa), Kanuni za Utoaji Mikopo za mwaka 2008, na
Mwongozo wa utoaji Mikopo na Ruzuku kwa mwaka wa masomo 2015/2016. Hadi kufikia
mwishoni mwa Januari 2016, Serikali ilikuwa imetoa mikopo yenye thamani ya
ShilingiBilioni 207.9 kwa wanafunzi 122,786 wa
elimu ya juu, wakiwemo wanafunzi wa mwaka wa kwanza 53,850 ambao
ni asilimia 98.9 ya wanafunzi 55,254 walioomba
mikopo hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika,
31. Ili Taifa liendelee kuwa na
wataalamu wa kutosha katika nyanja muhimu, Serikali itaendelea kutoa kipaumbele
cha kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu wanaodahiliwa katika programu za kipaumbele
ikiwemo Sayansi za Tiba,
Ualimu wa Sayansi na Hesabu, Uhandisi wa Mafuta na Gesi, Uhandisi Umwagiliaji,
Sayansi za Kilimo, Wanyama na Ardhi. Aidha, Serikali inaendelea kufanyia kazi
mikakati ya kuimarisha urejeshaji wa mikopo pamoja na kuwa na vyanzo endelevu
vya kupata fedha za kumudu ongezeko la wanafunzi wenye mahitaji ya mikopo.
VII: HALI YA USALAMA NCHINI
Mheshimiwa Naibu Spika,
32. Hali ya usalama katika Nchi yetu kwa ujumla ni
shwari. Hata hivyo, katika kipindi hiki nchi yetu imekuwa
ikikabiliana na changamoto ya ongezeko kubwa la Wakimbizi hususan katika Mkoa
wa Kigoma. Kambi zetu zilizoko mikoa ya Kigoma, Katavi, Tabora na Tanga
zinahifadhi wakimbizi wapatao 218,895 kutoka mataifa ya Burundi
(wakimbizi 156,377), Congo-DRC (wakimbizi 62,176),
Somalia (wakimbizi 150) na Mataifa Mchanganyiko (wakimbizi192)
kutoka nchi za Rwanda, Uganda, Sudan ya Kusini na Ethiopia. Kwa ujumla, katika
kipindi hiki wamepokelewa wakimbizi zaidi ya 122,267 kutoka
Burundi. Aidha, hadi kufikia tarehe 31
Desemba, 2015 kambi mpya ya wakimbizi ya
Nduta imepokea wakimbizi 38,994 wengi kati
yao wamehamishiwa kutoka Kambi ya Nyarugusu na wachache wakiwa wameingia moja
kwa moja kutokea Burundi.
Mheshimiwa Naibu Spika,
33. Kufuatia ujio wa wimbi kubwa la
wakimbizi toka Burundi kumejitokeza matukio ya uhalifu wa kutumia silaha za
moto ndani na nje ya kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu. Aidha,
kutokana na upekuzi na ukaguzi kwa
wakimbizi unaofanywa kwa pamoja na vyombo vya dola sanjari na taarifa za
ki-intelijensia imebainika kuwepo kwa askari waasi waliokimbia pamoja na raia
wa kawaida ambao wanajaribu kuwashawishi vijana kujisajili ili kujiunga na
vikundi vya waasi. Nitoe wito kwa wananchi na wakimbizi kushirikiana na vyombo
vyetu vya usalama kwa kutoa taarifa za uhalifu, hususan umiliki haramu wa
silaha za moto kwenye makambi na katika maeneo mbalimbali.
VIII: MPANGO ENDELEVU WA USAFI WA
MAZINGIRA NCHNI
Mheshimiwa Naibu Spika,
34. Mtakumbuka kuwa Mheshimiwa Rais
Dkt. John Pombe Magufuli, aliamua maadhimisho ya miaka 54 ya Uhuru ya terehe 9
Desemba, 2015 yafanyike kwa kufanya usafi wa mazingira katika maeneo ya Umma na
maeneo yanayowazunguka. Kwa ujumla Wananchi, Taasisi za Umma na Binafsi
ziliitikia agizo hilo na kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo. Nichukue fursa
hii kuwapongeza kwa dhati wananchi, taasisi za umma na binafsi wote kwa
kushiriki katika zoezi hilo kikamilifu. Mlionesha moyo wa uzalendo na ari kwa
nchi yenu. Nawapongeza sana!
Mheshimiwa Naibu Spika,
35. Usafi ni dhana muhimu katika
kulinda afya za binadamu na kudhibiti magonjwa mbalimbali ya mlipuko ikiwemo
kipindupindu. Ili kufanikisha lengo hili, kunahitajika juhudi za makusudi na za
pamoja katika usimamizi wa sheria, kanuni na taratibu tulizojiwekea. Hivyo,
Serikali imeamua kulifanya zoezi la usafi wa mazingira kuwa endelevu. Kupitia
Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Serikali imetoa Waraka unaoelekeza kuwa kila Jumamosi
ya mwisho wa mwezi iwe Siku Maalum ya kufanya Usafi wa Mazingira.
Mheshimiwa Naibu Spika,
36. Napenda kuendelea kusisitiza
katika kila ngazi yaani Viongozi na Wananchi kutimiza wajibu wao kwa
kuhakikisha zoezi hili linakuwa endelevu. Aidha, napenda kuwahimiza Viongozi wa
Mkoa, Wilaya na Halmashauri kusimamia usafi wa mazingira katika maeneo yao ya
utawala zoezi ambalo litakuwa linafanyika kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi.
Kila Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya nchini awe na mikakati ya kudumu ya
usafi ikiwa ni pamoja kuhakikisha kuwa kuna sheria ndogo za usafi wa mazingira
na zinatekelezwa ipasavyo. Aidha, Halmashauri zote nchini zihakikishe kuwa
uchafu uliokusanywa katika maeneo mbalimbali unazolewa na kupelekwa katika
maeneo mahususi ya dampo. Simamieni kikamilifu wakandarasi waliopewa zabuni
hizo na kuona wanatimiza wajibu wao kikamilifu.
Mheshimiwa Naibu Spika,
37. Kama tulivyoona Usafi wa
mazingira ni jukumu la kila Mwananchi na linapaswa kuwa endelevu. Rai yangu kwa
Watanzania wote ni kujenga tabia ya kuhakikisha kuwa mahali pa kazi na
mazingira yanayowazunguka yanakuwa safi wakati wote. Kufanya hivyo, kutasaidia
kuimarisha usafi wa mazingira na kuboresha afya. Hali kadhalika kupunguza
mlipuko wa magonjwa yakiwemo kipindupindu.
38. Wito wangu kwa Wananchi ni
kuona kuwa zoezi la usafi ni la kila mmoja wetu na kuepuka kuchafua mazingira
kwa makusudi ikiwemo kuepuka tabia za kutupa taka hovyo wanapokuwa katika
vyombo vya usafiri na pia kutofanya biashara katika maeneo yasiyoruhusiwa ili
kuzuia kutupwa taka hovyo. Wamiliki wa mabasi yanayofanya safari ndefu
wanatakiwa waweke vifaa vya takataka. Yeyote atakayebainika kutupa takataka
dirishani, atachukuliwa hatua za kinidhamu ikiwa ni pamoja na mmiliki wa basi
hilo.
Watendaji wa Mitaa na Kata na Vijiji kutimiza wajibu wao wa
kuhakikisha maeneo wanayoyasimamia yanakuwa katika hali ya usafi. Nitumie fursa
hii kuwahimiza Wananchi, Taasisi na Jumuiya zote kuhakikisha wanaweka mazingira
katika hali ya usafi na pia kushiriki katika siku ya usafi kama iliyopangwa na
Serikali.
IX: UHUSIANO WA KIMATAIFA
Mheshimiwa Naibu Spika,
39. Nchi yetu imeendelea kuwa
kivutio kikubwa katika mahusiano baina ya Nchi na Nchi, Jumuiya za Kikanda na
Kimataifa. Hii inatokana na Viongozi wetu ambao wamekuwa katika mstari wa mbele
kudumisha mahusiano yetu katika Medani za Kimataifa. Yapo mambo mengi
yaliyofanyika na yanayo endelea kufanyika kama mwendelezo wa kudumisha
ushirikiano katika Jumuia hizi za Kikanda na Kimataifa.
Mheshimiwa Naibu Spika,
40. Kutokana na juhudi za Viongozi
wetu kutangaza Nchi yetu Kimataifa, ni hivi karibuni tu Mheshimiwa Dkt. Jakaya
Mrisho Kikwete, Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania aliteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bwana Ban Ki-moon
kuwa mmoja wa Wenyeviti wa jopo la ushauri la ngazi ya juu kuhusu Afya ya Mama
na Mtoto Duniani (Every Woman, Every Child). Hii ni heshima kubwa kwa
nchi yetu kwa kuwa itaiweka Tanzania kuwa miongoni mwa mataifa yenye
kuheshimika duniani. Aidha, uteuzi huu ni chachu ambayo inaleta matumaini mapya
katika kukabiliana na changamoto za afya ya mama na mtoto, hususan katika nchi
zinazoendelea kama Tanzania. Nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt.
Jakaya Mrisho Kikwete kwa uteuzi huo. Tunamuombea heri na baraka tele katika
kutekeleza jukumu hilo kubwa la Kimataifa kwa maendeleo ya watu wetu.
X: KUIMARISHA UTENDAJI SERIKALINI
NA MAADILI
Mheshimiwa Naibu Spika,
41. Serikali ya Awamu ya Tano
inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi imedhamiria kurejesha nidhamu na maadili ya
Watendaji wa Serikali na Watumishi wa Umma katika kutoa huduma mbalimbali kwa
Wananchi kwenye maeneo mbalimbali. Katika kuhakikisha Watumishi wa Umma na
Watanzania wote wanafanya kazi, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekuja na kauli mbiu ya “Hapa Kazi Tu”. Tafsiri
ya falsafa hii ni kuwataka Watanzania wote katika nafasi mbalimbali walizopo
kufanya kazi kwa bidii na kujiepusha na vitendo vya uzembe, urasimu na kutenda
kazi kwa mazoea.
42. Aidha, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ya mwaka 1977 chini ya Ibara ya 22 inaainisha kuwa,
kilaMtu anayo haki ya kufanya kazi. Vilevile, Ibara ya 25 inafafanua
kuwa kufanya kazi ndiyo njia pekee ya kumwezesha Mtanzania kupata utajiri na
ndilo chimbuko la ustawi wa wananchi na ni kipimo cha utu.
Wakati akihutubia Mkutano wa kwanza wa Bunge lako Tukufu,
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kwa maneno yake alisema, napenda kunukuu:-
“Serikali nitakayounda, nataka iwe
inawahudumia Wananchi kwa haraka na sio kuwasumbua sumbua na kuwazungusha.
Natoa rai kwa Watumishi wa Serikali, hasa ambao ni wazembe na wavivu,
kujiandaa. Wamevumiliwa kwa muda mrefu sasa basi. Kwa sababu Watumishi wa aina
hiyo hawatavumiliwa katika Serikali nitakayoiongoza. Lugha za “Hiyo ni
changamoto tutaishughulikia” au “Mchakato unaendelea”hazitavumiliwa
katika Serikali ya Awamu ya Tano. Mimi nataka watu wa Kazi tu.
Hatuwezi kulea watu ambao wanalipwa mishahara lakini hawafanyi kazi
wanazotakiwa kufanya, au wamegeuza Ofisi za Umma kuwa ni mahala pa kuchuma bila
kufanya kazi.”mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa Naibu
Spika,
43. Ili kutekeleza
maneno ya Mheshimiwa Rais na kuhimiza matakwa ya Kikatiba, kila Mtanzania
anapaswa kushiriki na kujituma kwa uaminifu katika kazi halali za uzalishaji
mali. Aidha, kila Mwananchi anapaswa kuwa na nidhamu ya kazi na kuhakikisha
anafikia malengo yaliyowekwa. Nitumie fursa hii pia kuwakumbusha Watumishi wa
Umma kuwa wamepewa dhamana ya kuwahudumia Wananchi kwa niaba ya Serikali. Hivyo
wanawajibika kuhakikisha wanawahudumia Wananchi kwa haki, weledi, uadilifu na
kwa taaluma zao. Ni lazima wahakikishe kuwa wanatatua kero za Wananchi. Sio
sahihi wananchi kuwasilisha kero zao kwa viongozi wa ngazi za kitaifa hasa
wakati wa ziara ilhali viongozi wa mikoa na wilaya wapo katika maeneo hayo kwa
wakati wote.
44. Tunatambua kuwa wapo
Watumishi wanaotekeleza vyema majukumu yao. Lakini pia wapo Watumishi ambao
hawazingatii maadili ya kazi zao na pia wanafanya kazi kwa uzembe. Serikali
haitaacha kuchukua hatua za nidhamu kwa watumishi wote wasiozingatia kikamilifu
sheria, kanuni na taratibu katika Utumishi wa Umma. Aidha, kwa kuzingatia maelekezo ya Mheshimiwa Rais,
Viongozi na Watumishi wote wa Umma lazima tufanye kazi kwa kuzingatia weledi na
kujiamini. Kila mtu anapaswa kujitathmini kama dhamana aliyopewa
anaitendea haki.
Mheshimiwa Naibu
Spika,
45. Huu sasa ni wakati wa kufanya mabadiliko ya
dhati katika utendaji na uadilifu. Kwa maana hiyo napenda kusisitiza mambo
yafuatayo kwamba:-
(i) Kila Kiongozi na Mamlaka ya
nidhamu ni lazima kuwajibika kusimamia Utendaji na Maadili ya Kazi. Hatua za
kinidhamu zichukuliwe kwa wakati na kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu
za utumishi. TUSIONE HAYA HATA MARA MOJA, CHUKUENI HATUA.
(ii) Wananchi wahudumiwe ipasavyo na
kwa weledi, haki, uadilifu na heshima. Mambo haya yakizingatiwa hakuna
mwananchi atakayesafiri kutoka kijijini, wilayani au mkoani kutafuta huduma
Makao Makuu ya Wizara, Ofisi ya Waziri Mkuu au IKULU.
(iii) Madawati ya malalamiko yawepo
katika Ofisi za Umma. Aidha, tayari maelekezo yametolewa ya Watumishi wa Umma
wazingatie utaratibu wa kuvaa vitambulisho vyenye majina yao kwa urahisi wa
wananchi kuwatambua wanapowahudumia. AGIZO HILI LITEKELEZWE.
Mheshimiwa Naibu
Spika,
46. Ni kweli kwamba, Mheshimiwa Rais ametumia
dhana ya “kutumbua jipu” kama dawa ya kusimamia uwajibikaji
hasa katika wale wenye dalili ya kukosa maadili ya Utumishi wa Umma. Tafsiri ya
dhana hii ya “Kutumbua jipu”inalenga katika kuwarejesha Watumishi
wa Umma na walioko Serikalini katika mstari mzuri wa utendaji. Nitoe wito kwa
Waheshimiwa Wabunge wote kama tulivyo na kwa umoja wetu, tumuunge mkono
Mheshimiwa Rais katika vita hii kubwa ya “Kutumbua Majipu”. Tukiwa
pamoja na kwa kushirikiana tutaweza kuibadilisha nchi yetu kuwa nchi ya maadili
na yenye sifa ya juu katika utendaji wa Utumishi wa Umma.
Mheshimiwa Naibu
Spika,
47. Aidha,
naomba nisisitize kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe
Magufuli inaongozwa na Katiba, Sheria, Kanuni na Taratibu za Nchi. Vilevile
inaheshimu na kuthamini haki za Watumishi wa Umma wa ngazi zote na inatambua
mchango mkubwa unaotolewa na Watumishi wa Umma katika kuchangia ukuaji wa
uchumi wa Taifa. Kamwe, Serikali haitamwonea mtumishi yeyote wala kumnyanyasa
endapo tu atakuwa anatenda yale yanayopasa. Lakini pia haitamvumilia mtumishi
mzembe na asiyetimiza wajibu wake. Serikali itaendelea kuchukua hatua za
kurejesha nidhamu kwa Watumishi wa Umma ili kuwezesha Nchi yetu kuwa na
Utumishi wenye kuzingatia uadilifu na uliotukuka.
XI: HITIMISHO.
Mheshimiwa Naibu Spika,
48. Uzoefu nilioupata katika muda mfupi tuliokaa
pamoja hapa Bungeni, nimegundua kuwa tuna Waheshimiwa Wabunge mahiri waliobobea
katika nyanja mbalimbali. Wapo wasomi wa ngazi zote, wazee kwa vijana ambao
wana uzoefu na utaalam mkubwa. Ni imani yangu kuwa tutatumia utaalam na uwezo
mkubwa tulionao katika kuijenga nchi yetu na kuwasaidia Watanzania kutoka hapa
tulipo hadi hatua ya mbele katika kuleta maendeleo. Wananchi waliotuchagua
wanatutegemea. Nawaomba tutangulize uzalendo katika kila jambo tufanyalo kwa
manufaa ya Taifa letu na watu wake. Tufike mahali ambapo kwa elimu, busara na
hekima tulizonazo kuacha kabisa ushabiki wa kisiasa badala yake tutizame mbele
katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika,
49. Napenda kuhitimisha Hotuba yangu kwa kurejea
tena nilivyosema hapo awali kwamba, baada ya kukamilika kwa Uchaguzi Mkuu kwa
mafanikio makubwa, kazi kubwa iliyo mbele yetu ni kuijenga nchi yetu kwa umoja
na mshikamano. Nawaomba tuweke maslahi ya Watanzania na Taifa letu mbele.
Tudumishe amani na utulivu. Tupuuze sera zozote za kudhoofisha utaifa wetu kama
Watanzania na kutugawa kwa misingi yoyote ile, iwe ya kikabila, imani za dini,
rangi au kwa itikadi za kisiasa. Dhamira yetu sote iwe ni kukuza uchumi wa nchi
yetu na kuondoa umaskini ili kuwaletea wananchi wetu maendeleo na maisha
mazuri.
50. Ni jukumu la kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa
Tanzania inapiga hatua mbele. Tufanye kazi kwa bidii kuunga mkono kaulimbiu
yetu ya “Hapa ni Kazi Tu”. Aidha tutumie juhudi, maarifa na ubunifu
zaidi katika kila jambo. Mimi naamini kuwa kwa ushirikiano katika Bunge hili na
wananchi kwa ujumla, tutaweza kutimiza matarajio ya wananchi waliotuchagua na
matarajio ya Watanzania wote.
Mheshimiwa Naibu Spika,
51. Naomba nitumie nafasi hii tena
kuwashukuru wote waliosaidia kufanikisha mkutano huu. Nikushukuru wewe Naibu
Spika, na Mheshimiwa Spika kwa kutuongoza vizuri na kwa weledi mkubwa. Kipekee
niwashukuru Wenyeviti wa Bunge ambao wamekalia kiti kwa mara ya kwanza lakini
kwa weledi mkubwa, Hongereni sana!!.
Mheshimiwa Naibu Spika,
52. Nitumie nafasi hii kumshukuru Katibu wa Bunge
na Wasaidizi wake wote kwa kazi nzuri ya kuhakikisha mkutano huu unakamilisha
shughuli zake kama ilivyopangwa. Niwashukuru Wataalam wote wakiwemo Waandishi
wa Habari kwa kazi nzuri waliyofanya kufanikisha Mkutano huu.
Mheshimiwa Naibu Spika,
53. Nimalizie kwa kuwatakia wote safari njema
mnaporejea kwenye maeneo yenu ya kazi na katika majimbo yenu.Ninaamini
kwamba, Mwenyezi Mungu atatulinda na kutuweka salama sote kama tulivyo hadi
kukutana tena katika Mkutano ujao.
Mheshimiwa Naibu Spika,
54. Baada ya kusema hayo, naomba sasa kutoa Hoja
kwamba, Bunge lako Tukufu liahirishwe hadi tarehe 19
Aprili, 2016 saa 3:00 asubuhi litakapokutana
katika Mkutano wa Tatu kwenye Ukumbi huu hapa Dodoma.
Mheshimiwa Naibu Spika,
55. Naomba kutoa Hoja.
|
Saturday, February 06, 2016
Home
SIASA
KUAHIRISHA MKUTANO WA PILI WA BUNGE:-Soma Hatuba ya Mhe. Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa Bungeni Dodoma February 05,2016.
KUAHIRISHA MKUTANO WA PILI WA BUNGE:-Soma Hatuba ya Mhe. Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa Bungeni Dodoma February 05,2016.
Tags
# SIASA
Sambaza Hii
Chief Editor | Mhariri
SIASA
Labels:
SIASA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Kuhusu Mwandishi
Journalist / Chief Editor / Tanzanian Blogger
Simu: 0756830214 / 0620197747 / 0789925630.






No comments:
Post a Comment