Wanafunzi
wapatao 21 wanaosoma Shule ya Msingi Kilambo cha Mkolechi, Kata ya Kala mwambao
mwa Ziwa Tanganyika wilayani Nkasi, wamefukuzwa shule kwa muda usiojulikana kwa
kuvaa viatu maarufu yeboyebo.
Imeelezwa
kwamba yeboyebo hizo zilikusanywa na kuchomwa kwa kile kilichoelezwa kwamba ni
kunatokana na waraka uliotolewa na Ofisa Elimu Halmashauri ya Nkasi (Msingi)
ukipiga marufuku wanafunzi kuvaa aina hiyo ya viatu shuleni.
Hata
hivyo,jana Ofisa Elimu Halmashauri ya
Wilaya ya Nkasi (Msingi), Misana Kwangula, alikanusha kutoa waraka huo kwa
shule hiyo.
“Sina taarifa
rasmi ila jana jioni (Jumatatu) alinipigia simu mkazi mmoja akinitaarifu kwamba
kuna mwalimu wa shule ya msingi Kilambo cha Mkolechi amechoma moto viatu vya
wanafunzi kwa madai kuwa ofisa elimu (msingi) ametoa waraka kwamba wanafunzi
hawatakiwi kuvaa yeboyebo shuleni…
“Hakuna
waraka wala marufuku yoyote iliyotolewa, isitoshe sio sahihi hata kidogo wala
sio kitu kizuri kuchoma vifaa walivyonavyo wanafunzi…. Sasa kama amewachomea
wanafunzi hao viatu hivyo vya yeboyebo basi awanunulie viatu vya ngozi,” alisema
Kwangula.
Mkasa huo wa
wanafunzi hao kufukuzwa shule na kuchomewa yeboyebo walizovaa ulitokea juzi
wakati wanafunzi hao walipofika shuleni wakiwa wamevaa viatu hivyo.
Inaelezwa
kwamba mwalimu wa zamu, Baraka Mwakasege aliwazuia kuingia darasani, badala
yake akawaamuru wavue viatu vyao.
Taarifa
kutoka shuleni hapo zinaeleza kuwa, baada ya hatua hiyo, mwalimu huyo wa zamu
alizikusanya yeboyebo na kuzitia kiberiti kisha akawafukuza wanafunzi hao kwa
muda usiojulikana hadi wazazi na walezi watakapowanunulia viatu vya ngozi.
Mwalimu Mkuu
wa shule hiyo, Posian Ally alikanusha kumtuma mwalimu wa zamu kuwafukuza
wanafunzi hao shule kwa muda usiojulikana wala kuteketeza kwa moto yeboyebo
zao.
Alisema ataitisha kikao ili kujadili suala
hilo na kwamba mwalimu huyo akibainika kutenda kosa hilo ataamriwa kuwanunulia
watoto hao viatu vingine.
Pata Picha, Habari za Siasa, Kijamii, Biashara, Muziki na Michezo na Nyingine kwa kujiunga na Mimi Hapa...FACEBOOK .. TWITTER .. INSTAGRAM … Pia Usisite kututumia tukio la Picha/Habari kwa WhatsApp +255789925630 Or +255756830214.
|
No comments:
Post a Comment