|
Mwenyekiti
wa Chadema, Freeman Mbowe ametoa mwelekeo wa upangaji wa uongozi wa Kambi Rasmi
ya Upinzani bungeni na baraza kivuli la mawaziri, huku akionyesha kambi hiyo
kuwa tayari kushirikiana na Mbunge wa Kigoma Mjini kwa tiketi ya ACT-Wazalendo,
Zitto Kabwe.
Akizungumza
jana mjini Dodoma Mbowe alisema idadi ya wizara hizo itafanana na ya wizara za
Serikali ya Awamu ya Tano ambazo zipo 19.
“Tutatangaza
baraza kivuli kabla ya kumalizika kwa mkutano wa Bunge Ijumaa wiki hii na
baraza hili litashirikisha vyama vyote vinavyounda Ukawa,” alisema Mbowe.
Alisema
kigezo cha kwanza kitakuwa uzoefu na taaluma za wabunge kikifuatiwa na mgawanyo
wa nafasi kwa kuzingatia kipaumbele hicho kwanza.
“Tutazipanga
kulingana na muundo wa Muungano kwa sababu kuna wizara ambazo ni sehemu ya
Muungano. Nne tutazingatia jinsia kadri iwezekanavyo na tano tutazingatia
uteuzi kulingana na mikoa, yaani mawaziri vivuli watateuliwa kulingana na mikoa
wanayotoka kadri itakavyowezekana.”
Alisema
miaka yote, upinzani ulikuwa ukiitaka Serikali kupunguza ukubwa wa Baraza la
Mawaziri, hivyo uamuzi wa Rais John Magufuli kupunguza idadi ya wizara ni jambo
zuri na wao watafanya hivyo katika uteuzi wa baraza hilo kivuli.
Kuhusu Zitto
alisema: “Katika siasa na ushirikiano wa vyama hakuna mazingira ya kudumu.
Jambo lolote linawezekana lakini kuna taratibu zake na muda ndiyo huwa
unaongea.”
Alisema
Chadema na NCCR vimewahi kuwa na wabunge ambao kwa sasa ni makada wa CCM, huku
akitolea mfano jinsi Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa alivyohama CCM na
kujiunga na Chadema na kugombea urais.
“Hatujawahi
kama kambi ya upinzani kumtenga Zitto kwenye kila jambo, yapo mambo tunaweza
kulazimika kutengeneza ushirikiano na wabunge hata wa CCM ili kufanya jambo
fulani kutekelezeka.
“Kushirikiana
na Zitto si jambo la ajabu kama ambavyo umeona tukilifanya. Yapo majeraha mengi
ambayo tumeyapitia pande zote (Chadema na Zitto) ambayo huwezi kuyatibu kwa
siku moja.
"Yapo
ambayo yatapona kulingana na muda. Unaweza kumfanyia mtu kitu kibaya, lakini
baadaye ukatambua kuwa umekosea. Chochote katika siasa kinawezekana,” alisema
Mbowe.
Zitto
alifukuzwa Chadema na kujiunga na ACT Wazalendo Machi 21, 2015 chama ambacho
hakina ushirikiano na vyama vinavyounda Ukawa lakini katika siku za karibuni
ameonekana kuwa karibu na umoja huo wa wananchi, ikiwa ni pamoja na
kushirikiana kuibua hoja mbalimbali katika mkutano wa Bunge unaoendelea mjini
Dodoma.
Pata Picha, Habari
za Siasa, Kijamii, Biashara, Muziki na Michezo na Nyingine kwa
kujiunga na Mimi Hapa...FACEBOOK .. TWITTER .. INSTAGRAM … Pia Usisite kututumia tukio la Picha/Habari
kwa WhatsApp +255789925630-/+255756830214.
|
No comments:
Post a Comment