Serikali
ya Tanzania, katika mwaka wa fedha 2016/2017 imepanga kuongeza ajira kwa Vijana ili
kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana wengi wa kitanzania
kwa kuongeza ajira na kuwezesha wengine kujiajiri kupitia mifuko ya uwezeshaji
toka Halmashauri za Wilaya nchini.
Akijibu
swali la Mhe.Mgumba Tebweta Omary ,Mbunge wa Morogoro Kusini (CCM) lenye sehemu A na B lililouliza Serikali itaanza lini kuwawezesha vijana wa Jimbo la
Morogoro Kusini Mashariki kifedha ili
waweze kujiajiri na kuondokana na tatizo la ajira na umaskini ,Naibu Waziri
Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe Suleiman Jafo amesema vijana katika
Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Kusini Mashariki wamekuwa wakiwezeshwa
kiuchumi kupitia fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ambapo kila Halmashauri
hupaswa kutenga asilimia 5 ya mapato yake ya ndani kila mwaka kwa ajili ya
vijana.
Mhe Suleiman Jafo ameongeza kuwa katika Bajeti ya
mwaka 2014/2015,Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro ilifanikiwa kutoa Shillingi
Millioni 10.3 kwa vikundi vya vijana 19 kwa ajili ya kutekeleza shughuli
mbalimbali za kiuchumi na katika Bajeti ya mwaka wa fedha 2015/2016 vikundi vya
vijana vilitengewa Shilllingi Millioni 87.5 ili kuviwezesha kiuchumi kwa
kujiajiri.
“Katika
kutatua changamoto zilizopo kwa vijana tunawawezesha kifedha ili kujiajiri ili kumekuwa na tatizo
la fedha kuchelewa kufika kwa walengwa ila Serikali kupitia Wizara yangu
tunalifanyia kazi ili fedha zifike kwa wakati na tumetenga Shillingi Millioni
50 kwa kila kijiji kwa ajili ya kuwezesha vijana walioko katika vikundi
mbalimbali mfano SACCOS ili waweze kujiajiri na kujikwamua kiuchumi kwa
kujiondoa katika hali ya umaskini”
“Napenda
kuwaomba wabunge tusaidiane sababu wao wanahusika katika kamati za fedha za
Halmashauri za Wilaya, waende wakasimamie hizo fedha kwa ajili ya kuwezesha
vijana zitoke na ziwasaidie walengwa”
Alisema Mhe Jafo.
Aidha
Mhe Suleiman Jafo amesema kuwa Serikali
imetenga Shillingi Billioni 233 kwa ajiri ya kuajiri vijana wapya takribani
71,408 kati ya hao watumishi wapya wa Afya wanatarajiwa kuwa takribani 10,871
na Waalimu 40,000 kwa nchi nzima ili kupunguza tatizo la ajira kwa vijana
wanaomaliza vyuo mbalimbali nchini.
Serikali
kupitia Halmashauri za Wilaya imejipanga katika kuwawezesha vijana katika
maeneo yao kujikwamua kiuchumi kwa kujiajiri na kwa mwaka wa fedha 2016/2017
Serikali itaboresha zaidi mifuko ya kuwezesha vijana katika Halmashauri za
Wilaya kwa kununua vifaa zaidi vya kujifunza stadi mbalimbali za kazi
zitakazowezesha vijana wengi zaidi kuwa na ujuzi utakaowasaidia kujipatia
kipato na kujikwamua kiuchumi.
Pata Picha, Habari
za Siasa, Kijamii, Biashara, Muziki na Michezo na Nyingine kwa
kujiunga na Mimi Hapa...FACEBOOK .. TWITTER .. INSTAGRAM … Pia Usisite kututumia tukio la Picha/Habari
kwa WhatsApp +255789925630-/+255756830214.
|
No comments:
Post a Comment