Naibu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamis
Kigwangala akiwasili katika Hospitali ya rufaa ya Amana iliyopo Ilala,
Dar es Salaam alipofanya ziara ya kushtukiza baada ya sherehe za
kuapishwa.(Picha zote na Zainul Mzige wa Modewjiblog).
Na Rabi Hume, Modewjiblog.
Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu
amefanya ziara ya kushtukiza katika hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala
ikiwa ni masaa machache tangu kutoka kuapishwa na Rais wa Tanzania, Dkt.
John Pombe Magufuli kuwa Waziri wa Wizara hiyo.
Mhe.
Ummy aliwasili katika hospitali ya Mwananyamala, majira ya saa 8 mchana
na kuanza kuzungumza na wananchi mbalimbali waliokuwa wamekaa eneo la
hospitali hiyo kuhusu matatizo yanayowakabili pindi wanapofika hospitali
hapo kupatiwa huduma ambao wengi wao walionekana kutoridhishwa na
huduma wanazopatiwa wanazozihitaji.
Mmoja
wa wananchi ambao alielezea kwa masikitiko yaliyomkuta pindi alipofika
hospitalini hapo ni, Bi. Khadija Meso ambaye alisema kuwa walikuwa na
siku tatu tangu wamefika hospitalini hapo ambapo walikuwa wamempeleka
mtoto wao ambae alikuwa anaumwa lakini alikuwa hapatiwi huduma hali
imeyopelekea kupoteza maisha kwa mtoto huyo.
Mwingine
aliyezungumza aliyejitambulisha kwa jina la Mama Madohoro alisema kuwa
anashangazwa na hospitali ya rufaa kuwatoza wazee pesa licha ya sera ya
afya kusema wazee na watoto chini ya miaka 5 kupatiwa bure huduma za
kiafya.
Alisema
kuwa alimpeleka hospitalini hapo ndugu yake mwenye umri wa miaka 90
ambae alikuwa akihitajika kulipia vipimo vilivyo na gharama kubwa huku
vya gharama ndogo akipatiwa bure na kutokana na uwezo mdogo wa kifedha
alionao ukapelekea kupoteza maisha yake kwa mgonjwa huyo.
Nae
Othaman Rwambo alimuomba Mhe. Waziri kuwa ajaribu kuzungumza na wauguzi
wa hospitali hiyo kutokana na kutoa majibu machafu kwa wagonjwa
wanaofika katika hospitali hiyo kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Naibu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamis
Kigwangala akikagua vyumba vya madaktari baada ya kuona mlundikano wa
wagonjwa wakisubiri huduma.
Alisema
kuwa kasi ya rais wa awamu ya tano ni kufanya kazi na wao kama
watumishi wa umma wanapaswa kufanya kazi kwa bidii ili kuwahudumia
watanzania na kuwataka watumishi hao kuweka uzalendo mbele kuliko
maslahi binafsi.
Akiwajibu
wananchi hao pamoja na kuelezea sababu ya ziara yake, Mhe. Ummy Mwalimu
alisema kuwa amefika hospitalini hapo ili kujua changamoto
zinazowakabili wananchi lakini pia kujifunza ni kitu gani ambacho
wananchi wanahitaji kuboreshewa katika sekta ya afya.
Alisema
kuwa matatizo aliyoyakuta ni changamoto kwake na wizara yake na watakaa
kama wizara kuona ni jinsi gani wanaweza kutatua matatizo
yanayojitokeza katika hospitali hiyo na kuutaka uongozi wa hospitali
hiyo kumaliza matatizo yaliyo ndani ya uwezo wao ndani ya siku 3.
“Mambo
ambayo nimeyakuta hapa ni kujifunza na kuona ni hali gani wanakumbana
nayo wananchi wanapokuja kupata huduma za kiafya lakini pia kwangu ni
changamoto lakini kwa kasi aliyonayo rais wetu wa awamu ya tano hatuna
budi na sisi kuwa na kasi hiyo na mimi napenda kuwaambia wananchi
wanaopata huduma katika hospitali hii tutatatua matatizo yanayowakabili,
“Nimeupa
uongozi wa hospitali kazi ya kumaliza matatizo yaliyopo wanayoweza
kuyamaliza kama neti kwenye wodi kama ile ya wajawazito, na hata mambo
ya feni kwenye wodi za wanaume na mengine tutakaa kama wizara kuyajadili
tuone jinsi gani tutayamaliza,” alisema Mhe. Ummy.
Mh. Naibu Waziri, Dkt. Hamis Kigwangala akiingia katika chumba cha X-Ray kuangalia utendaji wa kazi unavyoendelea.
Aidha
Mhe. Waziri alisema siku ya Jumatano wanatarajia kutambulisha namba
ambayo wananchi watakuwa wanaitumia kutoa taarifa wizarani kuhusu kero
wanazokutana nazo hospitalini wanapokwenda kupata huduma za matibabu.
Nae
Naibu Waziri wa Wizara hiyo ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto, Dkt. Hamis Kigwangala amefanya ziara ya kushtukiza katika
hospitali ya rufaa ya Amana na kukuta baadhi ya huduma za afya katika
hospitali hiyo zikiwa zimesimama kwa sababu mbalimbali.
Baadhi
ya matatizo ambayo amekutana nayo hospitalini hapo ni pamoja na
kutokuwepo kwa mtoa huduma katika chumba cha Utra Sound, Ubovu wa
mashine ya kuchunguza matatizo yaliyopo mwilini (MS4S) na kubakia moja
ikifanya kazi ambayo inachukua muda mrefu kutoa majibu.
Matatizo
mengine ambayo amekutana nayo ni uchache wa vitanda, kutokupatikana kwa
dawa katika duka la hospitali huku maduka ya nje ya hospitali
zikipatikana na kutokuwepo kwa baadhi ya watumishi ofisini kukiwa ni
muda wa kazi.
Naibu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamis
Kigwangala akizungumza na mtoa huduma katika chumba cha X-Ray ambapo
aliridhishwa na utoaji huduma wa mtumishi huyo.
Akizungumzia
matatizo hayo alisema kuwa kuna uzembe umekuwa ukifanyika kwa baadhi ya
watumishi hali inayofanya hospitali hiyo kuwa na wagonjwa wengi bila
kupatiwa huduma na badala yake wanawapa rufaa kwenda Hospitali ya Taifa
ya Muhimbili.
“Tunachotaka
ni kuona wananchi wanapata huduma, nimefika hapa nakuta hata chumba cha
Utra Sound anaehusika hayupo na hata wagonjwa wakija hawatapata huduma
na kinachofata hapo wanampeleka Muhimbili ndiyo maana Muhimbili imejaa
wagonjwa kumbe sababu ni uzembe uliopo huku kwenye hospitali za rufaa,”
alisema Dkt. Kingwangala.
Aidha
Mhe. Naibu Waziri ameuagiza uongozi wa hospitali hiyo kufika wizarani
siku ya jumatatu saa 10 jioni ili kupewa maelekezo jinsi ya kufanya kazi
ya kuwahudumia wananchi na kwenda sawa na kasi ya rais Dkt. John Pombe
Magufuli ambaye anahitaji kuona serikali yake ikifanya kazi kwa
kuhudumia wananchi.
Naibu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamis
Kigwangala akizungumza na baadhi ya wananchi kuhusu upatikanaji wa
huduma wanazopata hospitalini hapo ambao wengi wao hawajaridhishwa na
utendaji wa wahudumu wa zamu wa siku hiyo.
Naibu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamis
Kigwangala akizungumza na mmoja wa Daktari (ambaye hakutaka sura yake
iyonekane) kuhusu utaratibu wa utoaji huduma kwa wagonjwa wanaosubiri
huduma hizo.
Naibu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamis
Kigwangala akimuulizia Kiongozi wa zamu katika ofisi za mapokezi ya
hospitali hiyo.
Muuguzi
Kiongozi wa Hospitali ya rufaa ya Amana, Bupe Mwakalenge akijibu
maswali ya Mheshimiwa Naibu Waziri kuhusu kutokuwepo kwa baadhi ya
Madaktari katika baadhi ya vitengo.
Naibu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamis
Kigwangala akitazama moja ya cheti cha mgonjwa aliyekuwa akilalamika
kusubiri kwa muda mrefu bila kupatiwa huduma.
Mwanasayansi
wa Maabara ya Hospitali ya rufaa ya Amana, Jabir Mukhsin (kulia) akitoa
maelezo kwa Naibu Waziri Dkt. Hamis Kigwangala kuhusu ubovu wa mashine
inayotumika kufanya vipimo mbalimbali (MS4S) ikiwemo mzunguko wa damu
mwilini ambayo kwa sasa imeharibika na kubakiwa na mashine moja ambayo
ufanyaji wake wa kazi unachukua muda mrefu kutoa majibu sahihi.
MS4S Mashine ambayo imeharibika.
Mmoja
wa wagonjwa waliokuwepo wakisubiri huduma ya kipimo cha MS4S
akimwelezea Mh. Naibu Waziri kuhusu kutokufanyika kwa kipimo hicho licha
ya kuwa hospitali wamepokea malipo yake ya kufanyiwa kipimo hicho.
Naibu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamis
Kigwangala akionekana kushangwazwa na jambo fulani wakati akiendelea na
ziara yake hospitalini hapo. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya
Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara hiyo, Gideon Malabeja.
Naibu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamis
Kigwangala akiwa nje ya chumba cha Ultra-sound ambacho kimefungwa
kufuli licha ya maelezo ya Muuguzi Kiongozi wa Hospitali hiyo Bi.
Mwakalenge kuwa mashine hiyo ni nzima na haina tatizo lolote.
Muuguzi
Kiongozi wa wagonjwa wa nje, Francis Itima akimwelezea Mheshimiwa
kuhusu changamoto ya upungufu wa vitanda katika wodi ya wakina mama
waliojifungua.
Naibu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamis
Kigwangala akikagua wodi ya watoto ambayo aliridhishwa na hali iliyopo
katika wodi hiyo.
Mfamasia
wa zamu katika hospitali ya Amana, Anna Kajiru akimpa maelezo Naibu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamis
Kigwangala kuhusu upungufu wa dawa uliopo katika duka hilo la dawa
hospitalini hapo.
Baadhi ya wananchi wakipatiwa huduma ya dawa katika duka la dawa lililopo hospitalini hapo.
Pichani
juu na chini ni Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto, Dkt. Hamis Kigwangala akitoa mrejesho kwa waandishi wa
habari kuhusu ziara yake ya kushtukiza, matatizo yanayoikabili hospitali
hiyo na hatua ambayo wizara itachukua.
Papo kwa Papo >>>> Pata Picha, Habari za Siasa, Kijamii, Biashara, Muziki na Michezo na Nyingine kwa kujiunga na mimi hapa…..FACEBOOK , TWITTER , INSTAGRAM , Pia tutumie tukio la Picha kwa WhatsApp . |
No comments:
Post a Comment