Haruna Niyonzima.
Klaubu ya Yanga imetangaza kuvunja
mkataba na kiungo wake wa kimataifa kutoka nchini Rwanda Haruna Niyonzima
kutokana na utovu wa nidhamu ikiwemo kuchelewa kuripoti kambini na kutoipa
kipaumbele klabu yake.
Nahodha huyo wa Rwanda alichelewa
kurejea kwenye klabu yake mara baada ya kumalizika kwa fainali za michuano ya
Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati (CEFAFA Challenge Cup) iliyofanyika nchini
Ethiopia.
Afisa Habari wa Yanga, Jerry Muro
amewaambia Waandishi wa Habari katika Mkutano uliofanyika makao makuu ya klabu,
Jangwani, Dar es Salaam kwamba Haruna pia anatakiwa kuilipa klabu.
Jerry Muro amesema uamuzi huo
umefikiwa na kikao cha Kamati ya Nidhamu ya klabu, baada ya kulichunguza kwa
umakini suala la mchezaji huyo na historia yake ya nidhamu pia ndani ya klabu
tangu asajiliwe miaka minne iliyopita.
Sakata la sasa la Niyonzima
linaanzia mwezi uliopita baada ya mchezaji huyo kuruhusiwa kwenda kuichezea
Rwanda katika Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki, CECAFA Challenge nchini
Ethiopia na akachelewa kurejea baada ya mashindano.
Kufuatia hali hiyo, klabu
ilimsimamisha kwa muda usiojulikana Niyonzima kabla ya suala lake kupelekwa
Kamati ya Nidhamu, ambayo hatimaye imekuja na maamuzi magumu.
Pamoja na Niyonzima kuwasilisha
vielelezo vyote vya kumsafisha, lakini uchunguzi wa Kamati ya Nidhamu
ulijiaminisha kiungo huyo amedanganya ili kukwepa hatua za kinidhamu.
Ulibaini plasta gumu (PoP) alilofunga baada ya kurejea akiwa amechelewa ilikuwa
ni ‘geresha’ na vielelezo vingine alivyowasilisha vilikuwa ‘feki’ pia.
Na ikamnasa kwenye picha za video
siku za karibuni ‘akijirusha’ sehemu mbalimbali za starehe ikiwemo kwenye
onyesho la mwanamuziki Ali Kiba.
Niyonzima ambaye alikuwa
akikitumikia kikosi cha timu yake ya taifa aliwasili Dar es Salaam December 16
mwaka huu wakati michuano ya Challenge Cup ilimalizika December 6.
Baada ya kuwasili Niyonzima alitoa
utetezi wake kwamba alikuwa akisumbuliwa na majeraha aliyoyapata kwenye
michuano ya Challenge kwani alikuwa amefungwa bandage ngumu mguuni. Lakini
Yanga ilihitaji uthibitisho wa ripoti ya daktari wake wa timu ya taifa.
December 17, Yanga ilitoa adhabu ya
kumsimamisha mchezaji huyo kwa muda usiojulikana huku akiendelea kupokea nusu
mshahara kwa muda wote huo aliosimamishwa kwa kipindi kisichojulikana.
Adhabu hiyo ilitangazwa na Katibu
Mkuu wa Yanga Dkt. Jonas Tiboroha baada ya kamati ya mashindano kuazimia adhabu
hiyo iwe ni ya awali wakati ikiendelea kujadili ni adhabu gani stahiki itolewe
kwa Niyonzima ambaye amejijengea umaarufu mkubwa kwenye soka la Tanzania na
Afrika Mashariki kwa ujumla.
Leo Jerry Muro ametangaza
uamuzi uliofikiwa na klabu ya Yanga wa kuvunja mkataba na Niyonzima huku
ikimtaka Niyonzima ailipe klabu hiyo zaidi ya dola za kimarekani 71,175 kama
fidia inayotokana na mkataba mpya unaomalizika mwaka 2017.
Haruna aliyezaliwa Februari 5, mwaka
1990 Gisenyi nchini Rwanda, alijiunga na Yanga SC mwaka 2011 akitokea APR ya
kwao, ambako aliwasili mwaka 2007 akitokea Rayon aliyoichezea kwa misimu miwili
baada ya kujiunga nayo akitokea Etincelles iliyomuibua mwaka 2005.
|
No comments:
Post a Comment