Naibu Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Dkt. Hamisi
Kigwangalla akifurahi jambo na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Sokoine
ya Mkoa wa Lindi, Dkt. Evaristo Kasanga (kulia) wakati wa ziara ya
kushtukiza aliyofanya mwishoni mwa juma mkoa wa Lindi.(Picha zote na
Zainul Mzige wa Modewjiblog)
Na Mwandishi wetu, Mtwara.
Naibu
Waziri katika Wizari wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, Dk Hamisi Kigwangalla ameagiza kubadilishwa kwa mifumo ya
utawala, malipo na uendeshaji katika katika hospitali nchini ili kuleta
ufanisi na tija.
Akizungumza
katika ziara yake ya kujifunza kuona katika hali ya kawaida huwa
zinatolewaje katika hospitali za wilaya na mikoa alisema kukosekana kwa
mifumo bora ya malipo na motisha kumedumaza utumishi.
Ziara
yake hiyo ambayo aliifanya katika hospitali ya mkoa wa Lindi ya Sokoine
na Ile ya Mtwara ya Ligula ililenga kuona masuala mbalimbali
yanayohusiana na utoaji huduma ili kuwa na nafasi ya kutengeneza hali
bora zaidi kimkakati.
Alisema
tatizo la upungufu wa dawa na hata raslimali watu linasababishwa na
kukosekana kwa mfumo waukusanyaji mapato ulio sahihi na wenye salama
ambao utawezesha pia kutoa motisha mbalimbali kwa watumishi ili
kuwavutia kufanyakazi katika mikoa ya pembezoni.
Aidha
alisema malipo yanayofanyika katika hospitali hizo yanatakiwa kuwa ya
kielektroniki kwa kuwa imethibitishwa kila kunapokuwapo na mfumo wa
malipo kielektroniki unaboresha mapato na hatimaye kuboresha ufanisi
katika uendeshaji wa hospitali pamoja na kuwapo kwa huduma bora za dawa.
Pia
ameagiza kuharakishwa kwa mfumo wa malipo kielektroniki kwa wateja wa
Bima ili mchango wao usaidie kwa haraka utoaji wa huduma ndani ya
hospitali.
Hata
hivyo Naibu Waziri huyo alisema aliridhishwa na utendaji katika
hospitali ya Sokoine na Ligula na kusema ufanisi wao unatokana na kuwapo
kwa mipango inayowezesha kazi kufanywa.
Alisema
hospitali ya Sokoine imeanzisha utaratibu wa mawasiliano ambao
unawezesha daktari mahali popote pale kuitwa huku kila mmoja akijua
kwamba daktari ameitwa eneo Fulani.
Alitaka
hospitali nyingine nchini hasa za rufaa kuangalia mfumo wa mawasiliano
ya ndani wa Hospitali ya Sokoine ili kuleta ufanisi katika utoaji wa
huduma kwa wananchi.
Pia
alipongeza utendaji wa hospitali ya Ligula na kusema kwamba kutokana na
ufanisi wao na huduma nzuri ndio maana hata wananchi wa nchi jirani
wanafika katika hospitali hiyo kupata huduma.
Alisema kama kusingelikuwa na huduma bora wananchi hao wasingelivuka kuja kutafuta huduma Ligula.
Hata
hivyo Naibu Waziri huyo alitaka kuwapo na utaratibu wa kudhibiti hali
hiyo na kusema kwamba ni matumaini yake kuwa wataalamu wataketi pamoja
na kutafuta namna ya kufanya katika mazingira hayo ya pia kuhudumia raia
wa nchi jirani.
Naye
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Ligula ya mkoa wa Mtwara, Dkt. Shaibu
Maarifa, alisema kwamba pamoja na huduma wanazotoa wanakabiliwa na
changamoto kadha hasa wodi ya wanawake na wajawazito.
Alisema
kutokana na ongezeko la watu katika mji wa Mtwara kutokana na kuwapo
kwa fursa kubwa za uchumi wa gesi na kiwanda cha saruji cha Dangote,
wafanyakazi wamekuwa wakifika na familia zao na hivyo kwa sasa wodi hiyo
haitoshi.
Hata hivyo alisema hali ingekuwa mbaya zaidi kama kituo cha afya cha Lipombe kisingesaidiana na hospitali hiyo.
Alisema
wodi ya watoto kwa sasa inafanyiwa ukarabati na benki ya Eco na wana
mkakati mwingine wa kuomba msaada wa kuondoa ufinyu wa wodi ya wanawake.
Alisema
anashukuru Katibu Tawala wa mkoa wa Mtwara, Alfred Luwanda na Mkuu wa
mkoa wameshafika katika hospitali hiyo na wameahidi kufanya kila
linalowezekana kuhakikisha kwamba matatizo yake yanatatuliwa na kukidhi
hospitali ya rufaa.
Kuhusu
upatikanaji wa dawa alisema kwamba hospitali hiyo wa sasa ina akiba ya
kutosha baada ya serikali kuipelekea sh milioni 80 na tayari
wameshazilipa kwa Bohari ya Dawa (MSD).
Aidha
alisema dawa za bima afya zipo na kwamba hawatarajii tatizo kwa kuwa
wamekubaliana na mamlaka husika kukitokea upungufu watatumia hata fedha
za bima kwa ajili ya kupunguza upungufu wa dawa.
Hata hivyo alisema kwamba wanakabiliwa na uhaba wa madaktari bingwa kwani kwa sasa wana dakatri bingwa wa mifupa na wanawake.
Naibu Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Dkt. Hamisi
Kigwangalla akipewa maelezo na Kaimu Muuguzi Mkuu wa Hospitali ya
Sokoine ya Mkoa wa Lindi, Damasiana Msalla alipotembelea wodi
ya wazazi na kuridhishwa na huduma za hospitalini hiyo wakati wa ziara
ya kushtukiza aliyoifanya mwishoni mwa juma mkoani Lindi.
Mganga
Mfawidhi wa Hospitali ya Sokoine ya Mkoa wa Lindi, Dkt. Evaristo
Kasanga akizungumza jambo na Eleuteri Mangi, Afisa kutoka Idara ya
Habari -MAELEZO jijini Dar es Salaam.
Hospitali ya Sokoine ya Mkoa wa Lindi imetwaa kombe la mshindi wa pili kwa utoaji wa huduma bora Tanzania kwa mwaka 2015.
Jedwali linaloonesha baadhi ya gharama za matibabu katika huduma zinazotolewa hospitali ya Sokoine ya Mkoa wa Lindi.
Ujumbe wa watoa huduma kwa wateja wanaofika kupata huduma hospitali ya Sokoine ya Mkoa wa Lindi.
Naibu Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Dkt. Hamisi
Kigwangalla (katikati) akiongozana na Mganga Mkuu wa Hospitali ya Ligula
ya mkoa wa Mtwara, Dkt. Shaibu Maarifa (kushoto) pamoja na Daktari wa
zamu kitengo cha dharura hospitalini hapo, Dkt. Ester Tumwanga kuelekea
wodi za wagonjwa wakati wa ziara ya kushtukiza aliyofanya mwishoni mwa
juma mkoani humo.
Naibu Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Dkt. Hamisi
Kigwangalla akiwa kwenye chumba cha dharura katika Hospitali ya Ligula
ya mkoa wa Mtwara. Kushoto ni Daktari wa zamu kitengo cha dharura
hospitalini hapo, Dkt. Ester Tumwanga.
Naibu Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Dkt. Hamisi
Kigwangalla akitoka kwenye wodi ya wazazi Hospitali ya Ligula ya mkoa wa
Mtwara wakati wa ziara ya kushtukiza aliyofanya mwishoni mwa juma
mkoani humo. Aliefuatana nae ni Mganga Mkuu wa Hospitali ya Ligula ya
mkoa wa Mtwara, Dkt. Shaibu Maarifa.
No comments:
Post a Comment