Naibu Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi),
Kassim Majaliwa.
Jumla ya
wanafunzi 18,751 kati ya 73,754 (asilimia 74.58) waliofanya mitihani ya kidato
cha nne mwaka jana 2014 wamekosa nafasi za masomo za kujiunga kidato cha tano
na vyuo vya ufundi mwaka huu 2015 kutokana na sababu mbalimbali.
Miongoni wa
sababu hizo ni ufinyu wa nafasi za shule, kushindwa kupata ufaulu wa masomo
waliyochagua, umri mkubwa wa watahiniwa wa kujitegemea pamoja na kukosa sifa za
kuchaguliwa, huku muhula wa kwanza wa kujiunga kidato cha tano ukitarajiwa
kuanza Julai 18, mwaka huu.
Aidha,
wanafunzi 479 wakiwamo wavulana 332 na wasichana 147 wamechaguliwa kujiunga na
vyuo vya ufundi mwaka huu, huku idadi ya wanafunzi hao ikiongezeka kutoka 472
mwaka 2014 hadi 479 mwaka huu.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Kassim
Majaliwa, alisema ufaulu umeongezeka na kwamba idadi ya wanafunzi wa kike
waliochaguliwa kujiunga na vyuo vya ufundi imeongezeka kutoka wanafunzi 117
mwaka 2014 hadi 147 mwaka 2015 sawa na ongezeko la asilimia 25.64.
Alisema kati
ya wanafunzi ambao hawakuchaguliwa, wavulana ni 13,216 na wasichana ni 3,219.
Hata hivyo,
alisema wanafunzi hao watadahiliwa na Baraza la Taifa la Ufundi (Nacte) kwenye
fani mbalimbali zikiwamo za ualimu, afya, maendeleo ya jamii na kilimo.
Majaliwa
alisema kati wanafunzi 55,003 waliochaguliwa kujiunga kidato cha tano na
mafunzo ya ufundi mwaka huu, wavulana ni 31,700 na wasishana ni 23,303 ambalo
ni ongezeko la wanafunzi 918 ikilinganishwa na wanafunzi 54,085 waliochaguliwa
mwaka jana.
Alisema
wanafunzi hao wamechaguliwa kujiunga kidato cha tano katika shule 277 zikiwamo
29 zilizopangiwa wanafunzi kwa mara ya kwanza mwaka huu.
Alisema
wanafunzi 29,744 wamechaguliwa kujiunga na masomo ya sayansi na hisabati
wakiwamo wavulana 18,294 na wasichana
11,450 sawa na asilimia 54.08.
Pia, alisema
wanafunzi 25,259 wakiwamo wavulana 13,406 na wasichana 11,853(45.92)
wamechaguliwa kujiunga na masomo ya sanaa na biashara.
Naibu Waziri
huyo alisema ufaulu wa watahiniwa wa mwaka 2014 kwa kuzingatia madaraja yaani
GPA ya 5.0 hadi 1.6 ni watahiniwa 73,754 sawa na asilimia 37.48 ya wanafunzi
waliofanya mtihani huo mwaka jana.
Alisema kuna
ongezeko la ufaulu wa asilimia 17.17 ikilinganishwa na matokeo ya mwaka 2013
ambayo watahiniwa walifaulu kuanzia daraja la kwanza hadi la tatu, huku idadi
ikiwa 71,527 sawa na asilimia 20.28 ya watahiniwa waliofanya mtihani huo.
Majaliwa alisema
muhula wa kwanza kwa masomo ya kidato cha tano mwaka huu utaanza Julai 18 na
kwamba wanafunzi wote wamepangwa katika shule zenye miundombinu na walimu wa
masomo husika.
Aliwataka
wanafunzi waliochaguliwa kuripoti katika shule walizopangiwa kwa wakati na
kuonya watakaoshindwa kuripoti shuleni zaidi ya siku 14 nafasi zao
zitachukuliwa na wanafunzi ambao wamekosa nafasi.
Alieleza
kuwa, uchaguzi wa wanafunzi wanaojiunga kidato cha tano na vyuo vya ufundi
umefanyika kwa kutumia mfumo wa kompyuta na kwa kuzingatia machaguo ya
wanafunzi, ufaulu wa nafasi zilizopo katika shule husika na kusistiza
hakutakuwa na fursa ya kufanya mabadiliko yoyote ya shule.
Mwaka juzi
wanafunzi 54,085 (asilimia 75.61) kati ya 404,083 (asilimia 94.48) waliofanya
mtihani wa kumaliza kidato cha nne Tanzania Bara walichaguliwa kujiunga na
kidato cha tano katika shule za sekondari za serikali na vyuo vya ufundi, huku
16,800 wenye sifa zinazotakiwa wakikosa kuchaguliwa kwa sababu mbalimbali
ikiwamo ufinyu wa nafasi.
Source:-
NIPASHE.
Pata Picha, Habari za Kisiasa, Kijamii, Kiuchumi na Michezo kila stori inayonifikia wakati wowote ukijiunga na mimi kwa kubonyeza…..FACEBOOK , TWITTER , INSTAGRAM , Pia tutumie tukio la Picha kwa WhatsApp +255789925630.
|
No comments:
Post a Comment