Hapa ndipo
nyumbani alipozaliwa na alipokuwa
akiishi aliyekuwa waziri
wa fedha na mbunge wa jimbo la
Kalenga mkoani Iringa,Dr Wiliam Mgimwa na ndipo atazikwa hapa.
|
Hii ndio
nyumba ya waziri wa fedha Dr Wiliam Mgimwa iliyopo jimboni Kalenga ambako ndipo
alipozaliwa ikiwa na bendera
ikipepea nusu mlingoti.
|
Wanachama wa
CCM wakibadilisha bendera nyumbani kwa aliyekuwa waziri wa fedha Dr Mgimwa. Picha na Francis Godwin.
|
Rais wa
Tanzania Jakaya Kikwete amepokea kwa
mshituko na huzuni kubwa taarifa za kifo cha Waziri wa Fedha, William Mgimwa,
aliyekuwa pia Mbunge wa Kalenga kupitia CCM.
Rais katika
taarifa ya Ikulu jana(Januari 02,2014), alisema Taifa limepoteza Waziri huyo
katika kipindi lilipokuwa linamhitaji zaidi kutokana na mchango wake mkubwa,
ambao amekuwa akiutoa kupitia nafasi zake za Waziri wa Serikali na mwakilishi
wa wananchi wa Kalenga.
Picha ya
Maktaba Waziri wa Fedha,
marehemu Dk William Mgimwa .
|
Kifo cha Mgimwa
kilitangazwa (Januari 01,2014)na Katibu Mkuu Kiongozi (KMK), Balozi Ombeni
Sefue kwa niaba ya Serikali.
Katika
tangazo lake, Balozi Sefue alisema Waziri Mgimwa aliaga dunia jana saa 5.20
(Saa za Afrika ya Kati) katika Hospitali ya Kloof Medi- Clinic, Pretoria, Afrika
Kusini ambako alilazwa kwa muda kidogo.
Balozi Sefue
alisema maandalizi ya kurudisha nyumbani mwili wa marehemu yanafanywa na
Serikali kwa kushirikiana na familia yake na taarifa zaidi zitatolewa baadaye
kwa kadri zinavyopatikana na maandalizi yanavyoendelea.
Katika
salamu zake kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na familia ya Mgimwa, Rais Kikwete
alisema: “Sina maneno ya kutosha kuelezea mshituko na huzuni yangu kubwa
kutokana na taarifa za kifo cha Mgimwa.
“Binafsi
nilimtembelea mara mbili hospitalini alikokuwa amelazwa na mara ya mwisho hali
yake ilikuwa imeimarika. Tulizungumza kwa kiasi cha dakika 10 hivi akanielezea
nia na tamaa yake ya kurejea nyumbani kwa sababu hali yake ilikuwa nzuri.”
Rais Kikwete
aliongeza: “Sote tunajua mchango wake katika Serikali. Sote tulitamani
kuendelea kuwa naye, lakini haya ni mapenzi ya Mungu. “Napenda kutoa pole
nyingi na rambirambi zangu za dhati kwa wanafamilia wote kwa kuondokewa na
mhimili wao. Naungana nanyi katika kuomboleza msiba huo mkubwa. Napenda mjue
kuwa msiba huu ni wangu pia. Machungu yenu ni majonzi yangu,” alisema Rais
Kikwete.
Rais pia aliwatumia rambirambi wananchi wa Kalenga akisema wamempoteza
mwakilishi na mtetezi mahiri wa maslahi yao.
Kifo cha
Mgimwa kinafanya wizara tano sasa kukosa mawaziri baada ya wengine wanne
kuondoka, kutokana na sakata la ujangili kwa utekelezaji wa Operesheni Tokomeza
Ujangili, kukiuka haki za binadamu kwa baadhi ya raia kuuawa na wengine kupata
ulemavu huku mifugo pia ikiuawa.
Wakati
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamisi Kagasheki alijiuzulu, mawaziri
wengine watatu walitenguliwa vyeo vyao, ambao ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi Dk Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi
Vuai Nahodha na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David
Mathayo.
![]() |
Picha ya
Maktaba ikimwonyesha Waziri wa Fedha, marehemu Dk William Mgimwa akisoma bajeti
ya wizara yake Bungeni mjini Dodoma.
|
Wasifu wake
Mgimwa alizaliwa
Kalenga Januari 20, 1950 na kupata elimu ya msingi katika Shule ya Wasa kati ya
mwaka 1961 na 1967 kabla ya kujiunga na Seminari ya Tosa kati ya mwaka 1966 na
1967.
Baada ya
hapo alijiunga na Seminari ya Tosamaganga kati ya mwaka 1968 na 1969 kisha
Seminari ya Mafinga kati ya mwaka 1970 na 1971.
Mwaka 1975
alijiunga na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) hadi mwaka 1978 ambapo alipata
Stashahada ya Juu katika masuala ya benki.
Alirudi IFM
mwaka 1983 na kusoma hadi mwaka 1984 na kutoka na Stashahada ya Uzamili katika
fedha na mwaka 1989 alijiunga na Chuo cha Uongozi Mzumbe kusomea Shahada ya
Uzamili katika fedha, ambayo aliipata mwaka 1991.
Kuhusu
ajira, Mgimwa alifanya kazi Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kati ya mwaka 1980
hadi mwaka 2000, akishika nafasi za Mhasibu mwaka 1980 hadi 1981; mwaka 1981
hadi 1989 alikuwa mhadhiri katika Chuo cha NBC na mwaka 1996 hadi 1997 alikuwa
Meneja katika benki hiyo.
Kuanzia
mwaka 1997 hadi 2000 alikuwa Mkurugenzi wa NBC kabla ya kuwa Mkuu wa Chuo cha
Benki Mwanza kati ya mwaka 2000 na 2010, alipochaguliwa kuwa Mbunge wa Kalenga,
akichukua nafasi ya Stephen Galinoma.
Mei 7 mwaka
juzi aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Waziri wa Fedha, akichukua nafasi
ya Mustafa Mkulo.
Ndani ya CCM
Mgimwa kati ya mwaka 2008 na 2010 alikuwa Mlezi wa Kata ya Wasa, mwaka 1994
hadi 1995 alikuwa Kamanda Msaidizi wa Vijana wa CCM wakati mwaka 1991 hadi 1994
alipata kuwa Diwani wa Kata ya Gangilonga. Katika uhai wake aliandika
machapisho mengi kuhusu masuala ya benki na fedha.
Wakati huo
huo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimemtumia Rais Jakaya Kikwete
salaam za rambirambi, kutokana na kifo hicho cha Waziri Mgimwa.
Aidha,
kimetuma salaam kwa familia na uongozi wa CCM, kutokana na msiba huo wa
kuondokewa na mmoja wa wanachama na mbunge.
Taarifa
iliyotolewa jana, ilisema chama hicho kimepokea kwa mshituko na majonzi makubwa
taarifa za kifo hicho.
“Kwa
masikitiko makubwa, CHADEMA kinatuma salaam za pole kwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete kwa kuondokewa na msaidizi wake wa karibu
na mtumishi mwenzake serikalini,” ilisema taarifa ya chama.
No comments:
Post a Comment