Moja ya mambo ambayo Nape
amezungumzia, ni kuhusu Kamati Kuu hiyo kuwahoji Mawaziri saba, kujibu kero au
mambo kadhaa ambayo yaliibuliwa wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa CCM,
Abdulrahman Kinana iliyomalizika hivi karibuni katika mikoa ya Mtwara, Ruvuma,
Mbeya na Njombe.
Nape alisema,
Kamati Kuu iliwahoji mmoja baada ya mwingine, kuanzia saa tano asubuhi hadi
jioni, baada ya kila mmoja kufika akiwa ameandaa majibu ya tuhuma au hoja
alizokuwa ametakiwa kujibu mbele ya Kamati Kuu hiyo.
"Kwa kuwa mawaziri
hao tulikuwa tumeshawapelekea hoja zinazowahusu ambazo tulizipisha kwa kiranja
wao Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, wengi wao walifika wakiwa na mafaili yenye
majibu, ambapo waliingia na kujieleza mmoja baada ya mwingine, na baada ya maelezo
ya kila mmoja wajumbe walitoa mapendekezo kwa Mwenyekiti, Rais Jakaya
Kikwete", alisema Nape.
Hata hivyo Nape alisema,
si vema kueleza kwenye vyombo vya habari kuhusu mapendekezo ambayo Kamati Kuu
ilimshauri Mwenyekiti kuchukua, akisema kufanya hivyo itakuwa sawa na
kumshinikiza kiongozi huyo kutekeleza mapendekezo yao kwa lazima na hivyo
kuharibu maana nzima ya ushauri.
"Sisi tulichofanya
ni kumpa mapendekezo, naye kwa mujibu na namna atakavyoona inafaa, atachukua
hatua, ambavyo si lazima kumfukuza Waziri Kama wengi wanavyotaka iwe, bali
anaweza kuchukua hatua yoyote ili mradi yeye mwenyewe kwa mamlaka aliyo nayo
ataona ina manufaa yatakayotoa majibu ya kero zilizosaababisha kila mmoja wa
mawaziri hao kuitwa mbele ya Kamati Kuu", alisema Nape.
IFUATAYO NI TAARIFA YOTE
KAMA ALIVYOITOA NAPE LEO DESEMBA 14,2013.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA
HABARI.
Kamati Kuu ya Halmashauri
Kuu ya Taifa ya CCM imekutana mjini Dodoma kwa kikao chake cha kawaida tarehe
13/12/2013. Kikao hicho kiliongozwa na Mwenyekiti wa Taifa wa CCM Ndg. Jakaya
Mrisho Kikwete.
Pamoja na mambo mengine
Kamati Kuu ilipokea taarifa ya ziara ya Katibu Mkuu wa CCM Ndg. Abdulrahman
Kinana na baadhi ya wajumbe wa Sekretarieti kwenye baadhi ya mikoa nchini.
Kamati Kuu imepongeza
ziara hizo kwa kuwa na mafanikio makubwa na kwa jinsi zilivyoongeza uhai wa
Chama na zilivyojishughulisha na mambo na mahitaji ya wanachi.
Aidha Kamati Kuu
imeipongeza sana Serikali kwa utekelezaji mzuri wa Ilani ya uchaguzi ya CCM
kwenye maeneo yote ambayo Katibu Mkuu ametembea.
Maeneo yaliyopongezwa ni
pamoja na Miundombinu hasa barabara, hatua kubwa kwenye fursa na ubora wa
elimu, maeneo ya afya na umeme vijijini.
Kamati Kuu iliwaita
mawaziri saba kuja kutoa maelezo ya mambo mbalimbali yaliyoibuliwa kwenye ziara
hizo za Katibu Mkuu wa CCM. Mawaziri hao ni;-
i). Ndg. Christopher
Chiza- Waziri wa Kilimo,Chakula na Ushirika
ii). Ndg. Shukuru
Kawambwa- Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi
iii). Ndg. Celina Kombani
- Waziri wa Utumishi
iv). Ndg. Hawa Ghasia
-Waziri wa TAMISEMI
v). Ndg. Abdallah Kigoda-
Waziri wa Viwanda na Biashara
vi). Ndg. Mathayo David
Mathayo- Waziri wa Mifugo na Uvuvi
vii). Ndg. Saada Mkuya-
Naibu Waziri wa Fedha( kwa niaba ya Waziri wa Fedha).
Baada ya maelezo ya
kutosha kutoka kwa mawaziri husika, Kamati Kuu iliagiza yafuatayo kwa
Serikali;-
1.Kuhusu wakulima wa
Pamba
(i). Serikali iangalie
upya upatikanaji wa pembejeo za ruzuku kwa wakulima wa Pamba nchini.
(ii). Uwepo wa mbegu bora
ni muhimu lakini ni vizuri pakawa na ushindani unaozingatia ubora ili kuondoa
ukiritimba wa mtengenezaji mmoja, hivyo kusaidia bei kuwa nzuri kwa wakulima.
Hata hivyo Chama kimeiagiza serikali kutowalazimisha wakulima kutumia mbegu ya
Quiton badala yake elimu itumike zaidi badala ya nguvu.
Serikali imetakiwa
kuangalia upya utaratibu wa kutoza bei ya mbegu ya Quiton kwa dola za
kimarekani badala ya pesa ya kitanzania,wakizingatia mbegu hiyo inazalishwa
nchini.
(iii).Kamati Kuu
imepongeza juhudi za Serikali kuvutia wawekezaji kwenye viwanda vya pamba mjini
Shinyanga, hata hivyo imeitaka Serikali kuangalia upya urasimu katika uwekezaji
wa viwanda nchini hasa vinavyoongeza thamani ya mazao na kutoa ajira nyingi
nchini.
(iv). Kuhusu kilimo cha
mkataba kwa wakulima wa Pamba, Serikali imetakiwa kuratibu utaratibu wa kilimo
hicho cha mkataba ili kuhakikisha kunakuwa na sheria na kanuni zinazosimamia
mfumo huo, ili kuwe na haki kwa pande zote mbili. Aidha wakulima wasilazimishwe
kufanya kilimo cha mkataba bali waingie kwa hiari yao wenyewe.
2. Kuhusu wakulima wa
Korosho.
(i). Pamoja na kuridhishwa
na hatua za muda mfupi kwa msimu wa korosho kwa mwaka 2013/2014 ambazo
zimesaidia bei na soko kuwa afadhali, bado Kamati Kuu imesisitiza Serikali
kujipanga kutatua tatizo la korosho kwa suluhisho la kudumu kwa kuhakikisha
korosho ina banguliwa nchini.
(ii). Serikali imetakiwa
kuangalia upya orodha ndefu ya makato wanayokatwa wakulima hasa wa korosho na
vyama vya msingi au mamlaka zinginezo ili kuondoa makato yasiyo ya lazima ili
kuongeza kipato cha mkulima.
(iii). Serikali pia
imetakiwa kuangalia upya mfumo wa uendeshaji wa vyama vya ushirika nchini ili
uwe ni ule wenye tija kwa wakulima na nchi kwa ujumla badala ya huu wa sasa
unaotoa mwanya kwa walaji kujipenyeza.
3. Kuhusu pembejeo za
ruzuku.
(i). Kamati Kuu imepokea
taarifa ya malalamiko ya wakulima juu ya ufanyaji kazi wa mbolea ya Minjingu na
kuagiza kuwa pamoja na kuendelea na utafiti wa nini kinachotokea kwenye mbolea
hiyo ya Minjingu kiasi cha kuleta malalamiko yote hayo, wananchi wawe huru
kutumia mbolea wanayoitaka badala ya kulazimishwa kutumia mbolea
wanayoilalamikia ya Minjingu.
(ii). Serikali iangalie
utaratibu bora wa kuratibu swala zima la pembejeo za ruzuku ili lifaidishe
zaidi wakulima walio wengi badala ya utaratibu wa sasa ambao licha ya
kulalamikiwa na wakulima unaotoa mwanya kwa watu wachache kutumia vibaya
utaratibu huo kuiibia serikali na wakulima.
4. Kuhusu wakulima wa
mahindi.
(i). Pamoja na Serikali
kuanza kulipa madai ya wakulima wa mahindi kwa mikoa ya Ruvuma baada ya ziara
ya Katibu Mkuu kwenye maeneo hayo, bado serikali imetakiwa kumalizia malipo
yaliyobaki na kuhakikisha wanakomesha utaratibu wa kuwakopa wananchi mazao yao
bila kuwalipa.
(ii). Utaratibu uwekwe wa
kufanya tathimini mapema ya mahitaji na uwezo wa kununua mahindi wa
Serikali ili kuepusha utaratibu wa kuchukua mahindi ya wakulima bila kuwalipa.
5. Kuhusu madai
mbalimbali ya waalimu.
(i). Kamati Kuu
imesisitiza kupandishwa vyeo na kulipwa stahiki zao waalimu ni haki yao
ya msingi hivyo lazima itekelezwe bila kuwa na visingizio na ifanyike kwa haki.
(ii). Kamati Kuu
imeiagiza Serikali kukamilisha haraka uhakiki wa madai ya waalimu na kuwalipa
haki zao zote mapema iwezekanavyo. Lakini Kamati Kuu imeitaka Serikali
kuhakikisha madeni haya hayazaliwi tena kwa kuweka mfumo utakao zuia madeni
haya kuzaliwa.
(iii). Kuhusu wakuu wa
idara mbalimbali wasiotenda haki kwa waalimu, na wale wanaotumia lugha mbaya na
za kejeli kwa waalimu wakibainika wachukuliwe hatua mara moja.
(iv). Pamoja na kuwa
Serikali inaangalia utaratibu bora wa kuboresha mawasiliano kati ya wizara
zinazohusika na kusimamia waalimu, Kamati Kuu imeitaka Serikali jambo hili
lifanyike mapema ili kupunguza malalamiko ya waalimu.
6. Kuhusu ubadhirifu
kwenye Halmashauri.
(i). Kamati Kuu imekemea
watendaji wachache wanaojihusisha na ubadhirifu kwenye Halmashauri mbalimbali
nchini. Imewataka madiwani wa CCM kuwa wakali na wasiamamie vizuri halmashauri
zao kuhakikisha fedha inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kupata thamani ya
fedha.
(ii). Aidha Serikali
imetakiwa kuchukua hatua kali na kwa haraka kwa wote wanaobainika kufanya
ubadhirifu, ili iwe fundisho kwa wengine.
(iii). Serikali
imeshauriwa kuangalia upya sheria kama zinakidhi mahitaji ya wakati na
mazingira ya sasa ili kuongeza uwezo wa udhibiti na kuokoa pesa za walipakodi
zinazopotea kwa walafi wachache kwenye Halmashauri mbalimbali nchini.
7. Kuhusu tatizo la Maji
nchini.
Kamati Kuu ilipokea
taarifa ya tatizo kubwa la maji nchini, ambalo lilijitokeza kila sehemu
aliyotembelea Katibu Mkuu. Chama kimeishauri Serikali kuchukua juhudi na
mkakati wa makusudi na dharura kulitafutia ufumbuzi wa haraka na wakudumu
tatizo la upatikanaji wa maji nchini.
8. Kuhusu migogoro ya
Aridhi, Wafugaji na Wakulima.
Pamoja na kupokea taarifa
juu ya migogoro mbalimbali ya wakulima ,wafugaji na wakulima nchini, kamati kuu
imepongeza uamuzi wa bunge kuunda Kamati teule ya bunge na uamuzi wa kuiagiza
kamati ya kudumu ya bunge ya aridhi, maliasili na mazingira kuchunguza migogoro
hii na kutoa mapendekezo juu ya namna bora ya kuimaliza kabisa migogoro hii.
Aidha kamati kuu imeitaka
Serikali na wabunge wa CCM kuzijadili kwa makini ripoti hizo na kufikia
hitimisho la migogoro hii nchini.
Hata hivyo Kamati Kuu imeitaka Serikali
kuangalia upya utaratibu uliotumika kuwamilikisha watu wachache maeneo makubwa
ya aridhi, ambao wameshindwa kuyaendeleza badala yake wanayatumia kuwakodishia
wakulima wadogo.
Aidha maagizo yote haya
yatatolewa taarifa kwenye Chama mara kwa mara, ili kuwezesha Chama kufuatilia
utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010/2015.
Imetolewa na;-
Nape Moses Nnauye
Katibu wa Itikadi na
Uenezi
14/12/2013
nice information soma Taarifa ya Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM huku Mawaziri saba wakihojiwa
ReplyDelete