Ikiwa ni
takribani mwezi mmoja tu tangu bomu lilipolipuka kwenye mkutano wa Chama Cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), mkoani Arusha, jana tukio kama hilo
lilitokea jijini Dar es Salaam kwenye mkutano wa Mbunge wa Ubungo (Chadema),
John Mnyika, ambao aliutishia kwa lengo la kuwaelezea wananchi mrejesho wa
yaliyojiri bungeni hivi karibuni na kuhamasisha wananchi kushiriki kutoa maoni
kwenye rasimu ya Katiba mpya.
Tofauti na
Arusha, jana bomu hilo lililipuka likiwa kwenye gari la Polisi waliokuwa kwenye
mkutano huo katika viwanja vya Sahara, katika Kata ya Mabibo jijini Dar es
Salaam na kuibua taharuki kubwa kwa wananchi na wafuasi wa Chadema waliokuwa
wamehudhuria mkutano huo.
Polisi
wamethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kwamba bomu hilo lililipuka
kwa bahati mbaya na kwamba ni la jeshi hilo.
Akizungumza
na NIPASHE kwa njia ya simu jana, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya
Kinondoni, Yusuf Mrefu, alisema mlipuko huo ulitokea kwa bahati mbaya na kwamba
haikuwa nia ya polisi kutumia nguvu au kuzuia mkutano wa Chadema.
"Ni
bomu la mkononi. Polisi walikuwa na mazungumzo na viongozi wa Chadema na siyo
kwamba kulikuwa na vurugu au matumizi ya nguvu, ni tukio la bahati mbaya,"
alisema.
Mrefu
alisema pia kwamba Polisi haikuwa imepanga kupiga mabomu kwenye mkutano huo
wala kuuzuia.
"Siwezi
kueleza limetengenezwa wapi, ni aina gani au kazi yake; kwa sababu mimi
mwenyewe nimepewa taarifa kwa simu, sikuwa eneo la tukio, nilikuwa kwenye
msafara wa Makamu wa Rais," alisema.
Aidha, Kaimu
Kamanda huyo bila kufafanua alisema: "Halina madhara." Hata hivyo,
alipoulizwa kazi ya bomu hilo ikiwa halina madhara, alijibu kwamba asingeweza
kueleza zaidi kwa kuwa hakuwa na taarifa za kina kwa kuwa hakuwa eneo la tukio.
Hata
alipoulizwa jina la kitaalamu la bomu hilo alisema hana taarifa za kina.
Wakati
Polisi wakieleza hayo, mashuhuda pamoja na taarifa zilizosambazwa kwenye
mitandao ya kijamii zilidai kwamba mtu mmoja alijeruhiwa kwenye tukio hilo.
Taarifa
zinaeleza kwamba mlipuko huo ulitokea baada ya Mnyika kwenda kwenye gari ya
Polisi kwa nia ya kuwasalimia na ndipo kishindo kilichoashiria mlipuko wa bomu
kilisikika.
Akizungumzia
kuhusu tukio hilo wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Ubungo jana,
Mnyika alidai kuwa waliomba kibali cha kufanya mkutano huo siku tano kabla kwa
kuwaandikia polisi barua, lakini hawakuwajibu hadi jana asubuhi wakiwataka
kusitisha kwa sababu kulikuwa na ziara ya Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib
Bilal, kukagua shughuli za usafi jijini Dar es Salaam.
Mnyika
alisema aliwajibu polisi kuwa hawezi kupokea taarifa za kusitisha mkutano wake
huyo kwa simu bali aliwataka wampe kwa maandishi.
Alisema
baadaye polisi waliandika barua ya kumuagiza asitishe mkutano wake huo kupisha
ziara ya Makamu wa Rais.
Alisema hata
hivyo, alipoangalia ratiba ya ziara ya Makamu wa Rais, aligundua kuwa haikugusa
jimboni mwake na kuwaomba tena polisi wamruhusu kufanya mkutano huo.
Alisema
alimtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Suleiman Kova na
kujibiwa yuko nje ya nchi, hivyo aliwaomba wasaidizi wake wampe kibali lakini
hawamkujibu na kumuomba asubiri wajadiliane kwanza.
Mnyika
alisema kutokana na muda kuyoyoma, alimtafuta Mkuu wa Jesh la Polisi nchini,
Inspekta Jenerali Said Mwema, kumuomba amsaidie, lakini aligonga mwamba baada
ya kumjibu kuwa hawezi kutengua maamuzi yaliyotolewa na kiongozi wake wa chini
na kumtaka aandike barua nyingine ya kuomba kibali cha kufanya mkutano.
"Wakati
naendelea kuwasiliana na viongozi wa polisi kuomba wanipe kibali, nilikuwa
tayari kwenye viwanja vya Sahara na ndipo zikaja defender (magari ya polisi)
tatu za polisi," alisema na kuongeza kuwa:
"Ziliposimama
niliwafuata na kwenda kuwaambia kuwa vipi tena mbona mmekuja wakati nimeomba
kibali cha kufanya mkutano, ndipo lilipolipuka bomu hilo ndani ya gari ambalo
nami nilikuwa nimesimama karibu nalo."
Alisema
baada ya kulipuka bomu hilo, watu walikuwa wamekusanyika katika viwanja hivyo
walikumbwa na taharuki na kukimbia ovyo kunusuru ya maisha yao. Kwa mujibu wa
Mnyika, wakati watu hao wakikimbia ovyo, alikwenda lilikoangukia bomu hilo
kumuwahi majeruhi, Thomas Jarome.
Alisema
polisi nao walikwenda kumuwahi majeruhi huyo na kumbeba 'mzobemzobe' wakati
wakitaka kumuingiza kwenda gari lao, Mnyika na viongozi wengine wa Chadema
waliwazuia na kumpeleka hospitalini ambako alipatiwa matibabu na kuruhusiwa
kuondoka.
Alisema
wakati majeruhi huyo akiendelea kupatiwa matibabu, viongozi wa chama hicho
walikusanyika na kujadili sehemu nyingine ya kwenda kufanyia mkutano wao na
kubaini kuwa Diwani wao wa Ubungo alikuwa na kibali cha kufanya mkutano eneo la
Abiani Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Aliwatangazia
wananchi wafuasi na wapenzi wa Chadema wakiwaomba wahamie Abiani.
Katibu wa
Mbunge wa Ubungo, Gastone Garubindi, alidai bomu hilo lilipigwa na polisi kwa
lengo la kuwatisha wananchi wasihudhurie mkutano huo.
Akizungumza
na NIPASHE majeruhi Jerome, alidai kuwa polisi walikusudia kulipua bomu hilo
kwani lilikuwa mikononi mwao na askari waliopata mafunzo ya kutosha kuhusu
milipuko.
Alisema
baada ya kujeruhiwa, viongozi wa Chadema walimpeleka katika kituo Mabibo ambako
alipewa PF3 na kwenda zahanati Tandale na kutibiwa.
Jerome
alisema baada ya kutibiwa aliruhusiwa kurejea nyumbani na kutakiwa kurudi leo
kwa uchunguzi zaidi na kuchomwa sindano ya pepopunda (tetanus).
Tukio la
jana limekuja huku uchunguzi wa mlipuko wa bomu uliotokea Juni 15, mwaka huu
katika viwanja vya Soweto, Kata ya Kaloleni mkoani Arusha kwenye mkutano wa
kufunga kampeni za udiwani wa Chadema, ukiwa bado unaendelea. Katika tukio
hilo, watu watatu walipoteza maisha na wengine kadhaa kujeruhiwa vibaya. Bomu
hilo linaelezwa kuwa lilipuka kwenye mkusanyiko wa watu mita chache kutoka
jukwa kuu, wakati mkutano huo ulipokuwa umekwisha na shughuli ya kukusanya
michango ikiendelea.
Viongozi wa
juu wa Chadema, Freeman Mbowe na Godbless Lema walikuwapo kwenye eneo hilo.
Hadi sasa
hakuna mtu ambaye amekamatwa kuhusiana na mlipuko huo pamoja na kwamba Serikali
imetangaza donge nono la Sh. milioni 100 kwa mtu atakayefanikisha kukamatwa kwa
mhusika au wahusika wa tukio hilo.
Zaidi ya
watu 70 walijeruhiwa baada ya tukio hilo kufuatia polisi kufyatua risasi za
moto kwa nia ya kukabiliana na wananchi waliokuwa wanawashambulia.
Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda alikaririwa akieleza kwamba bomu lililolipuka Arusha
lilitengenezwa China.
Aidha,
Septemba, 2012 aliyekuwa Mwakilishi wa Kituo cha Chanel Ten mkoani Iringa,
Daudi Mwangosi, aliuawa kwa kupigwa bomu la machozi na askari wa Kikosi cha
Kutuliza Ghasia (FFU) eneo la Nyololo Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa.
Alipigwa
bomu hilo baada ya kupokea kipigo kutoka kwa baadhi ya askari wa FFU waliokuwa
wakiizuia Chadema kuendesha harakati zake za kufungua tawi la chama hicho
katika eneo hilo.
Mwangosi
ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Klabu
ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa (IPC), aliuawa mbele ya wananchi, askari
wa FFU na aliyekuwa Kamanda wa jeshi
hilo mkoani humo, Michael Kamuhanda.
Askari huyo
anayedaiwa kumuua Mwangosi, Pacificus Cleophase Simon (23), alikamatwa na
kufikishwa mahakamani akikabiliwa na tuhuma za mauaji hayo na kesi hiyo bado
inaendelea kutajwa.
CHANZO:
NIPASHE
|
No comments:
Post a Comment