Na. Aron
Msigwa –MAELEZO.
Serikali
imewasimamisha kazi mkurugenzi mkuu wa Bohari ya Dawa nchini (MSD) ,Mkuu wa
kitengo cha Udhibiti na Ubora na Afisa Udhibiti Ubora wa ohari hiyo ili kupisha
uchunguzi dhidi yao kufuatia kuruhusu kusambazwa kwa dawa bandia za kupunguza
makali ya UKIMWI aina ya TT –VIR 30 katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya nchini.
Aidha
imepiga marufuku usambazaji na matumizi ya dawa aina ya TT –VIR 30 toleo na 0C
.01.85 inayotengenezwa na kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Industries Ltd
(TPI) kufuatia dawa hiyo kutengenezwa chini ya kiwango na kutofaa kwa matumizi
ya binadamu.
Akizungumza
leo jijini Dar es salaam Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Hussein Mwinyi
amesema kuwa hatua hiyo imechukuliwa mara baada ya kubaini kuwepo kwa dawa
bandia ya kupunguza makali ya Ukimwi katika hospitali ya wilaya ya Tarime
kufuatia ukaguzi uliofanywa na Wizara ya Afya kupitia Mamlaka ya Chakula na
Dawa nchini (TFDA).
Amesema kuwa
ukaguzi na uchunguzi wa kimaabara dhidi ya dawa hiyo isiyokidhi viwango
ulibainia kuwa nyaraka zilizopo kuhusiana na dawa hizo unaonyesha kuwa Kiwanda
cha Tanzania Pharmaceutical Industries Ltd (TPI) waliiuzia Bohari ya Dawa (MSD)
dawa hiyo bandia toleo namba 0C. 01. 85
iliyotengenezwa nchini mwezi Machi 2011 na kuonyesha mwisho wa matumizi
yake mwezi Februari 2013.
Amefafanua kuwa dawa hiyo bandia ilikua na dawa zenye
rangi mbili tofauti njano na nyeupe na kuwa na viambata tofauti vilivyopaswa
kuwepo aina ya Efaverenz badala ya Niverapine, Lamivudine na Stavudine na
kuongeza kuwa vidonge vilivyokutwa kwenye vifungashio vya dawa husika vilikua
tofauti na vifungashio vilivyosajiliwa na TFDA.
Dkt. Mwinyi
amesema kuwa serikali inahakikisha kuwa dawa zenye ubora unaotakiwa za
kupunguza makali ya UKIMWI zinaendelea kupatikana katika vituo vya kutolea
huduma kote nchini na kuwaagiza waganga wakuu wa mikoa, wilaya na kamati za dawa na Tiba katika vituo vya
huduma za afya kuhakikisha kuwa zinapokea, kuhakiki na kusimamia kikamilifu
ubora na matumizi sahihi ya dawa na vifaa tiba nchini.
Kuhusu
upatikanaji wa dawa hizo amewatoa hofu wananchi
na kuwahakikishia kuwa dawa za
kutosha zenye viwango stahili zitaendelea kupatikana katika vituo vya kutolea huduma za afya
nchini na kuwataka wananchi kutoa kushirikiana na mamlaka husika kwa kutoa
taarifa pale wanapobaini kuwepo kwa dawa zenye ubora wenye mashaka au uvunjifu
wa sheria inayosimamia ubora na usalama wa dawa.
No comments:
Post a Comment