Pazia la Ligi Kuu VPL 2017/2018- Yanga SC Yapigwa 3-1 na Azam FC. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Tuesday, May 29, 2018

Pazia la Ligi Kuu VPL 2017/2018- Yanga SC Yapigwa 3-1 na Azam FC.

Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara msimu wa 2017/2018 imefikia Tamati yake Jumatatu May 28, 2018 kwa michezo 15 kuchezwa katika viwanja mbalimbali ambapo, Yanga SC wakiwa uwanja wa Taifa Dar es Salaam wamekutana na kipigo cha magoli 3-1 kutoka Azam FC.

Magoli ya Azam FC katika mchezo huo yakifungwa na Yahaya Zayd dakika ya 4, Shaban Iddi dakika ya 60 na Salum Abubakar dakika ya 68 wakati goli pekee la Yanga SC lilifungwa na Abdallah Kheri wa Azam FC aliyejifunga.

Kwa matokeo hayo, Azam FC inamaliza msimu na pointi 58 nyuma ya Mabingwa, Simba SC waliomaliza na pointi 69, wakati Yanga SC wanabaki na pointi zao 52.

Kipigo hicho sasa kinaifanya Yanga SC kumaliza Ligi wakiwa nafasi ya tatu nyuma ya Azam FC waliyopo nafasi ya pili, wakati Timu ya Majimaji FC ya Songea baada ya kutoa sare ya 1-1 na Mabingwa wapya wa Ligi hiyo Simba SC wanaungana na Njombe Mji FC kushuka daraja.

Msimu wa 2018/2019 Ligi Kuu itakuwa na Jumla ya timu 20  kwa timu za Biashara FC ya Musoma, Coastal Union ya Tanga, KMC ya Kinondoni, Alliance ya Mwanza, JKT Tanzania na African Lyon zikipanda daraja kucheza Ligi Kuu.
Simba SC, zamani ikijulikana kama Sunderland msimu huu imetwaa taji la 19 baada ya awali kubeba katika miaka ya 1965, 1966 (kama Sunderland), 1972, 1973, 1976, 1977, 1978, 1979, 1980, 1993, 1994, 1995, 2001, 2002, 2004, 2007, 2009–10 na 2011–2012.
 
Lakini mahasimu wao, Yanga SC wanabaki kuwa Mabingwa mara nyingi wa Ligi Kuu, baada ya kubeba taji mara 27 katika miaka ya 1968, 1969, 1970, 1971, 1972, 1974, 1981, 1983, 1987, 1991, 1996, 1997, 2000, 2005, 2006, 2007–2008, 2008–2009, 2010–2011, 2012–2013, 2014–2015, 2015–2016 na 2016–2017.

Timu nyingine zilizowahi kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu ni Cosmopolitans 1967, Pan African 1982, Azam FC 2013-2014 zote za Dar es Salaam, Mseto SC 1975, Mtibwa Sugar 1999 na 2000 zote za Morogoro, Tukuyu Stars ya Mbeya 1986 na Coastal Union ya Tanga 1988.

1 comment:

Post Bottom Ad