|
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Ashatu Kijaji.
Serikali
ilizindua sera ya Taifa ya huduma ndogo za fedha ili kuhakikisha wakopaji
wakiwemo wajasiriamali wadogo wanalindwa na kupata haki zao bila kudhurumiwa
wanapo hitaji mikopo na huduma zingine za kifedha zitakazowasaidia kujiendeleza
kiuchumi.
Hayo
yameelezwa Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt.
Ashatu Kijaji (Mb) alipokuwa akijibu maswali ya Mbunge Mhe. Khatibu Said Haji
aliyetaka kujua hatua za Serikali kuhusu taasisi za huduma ndogo za kifedha
(Microfinance) kuwatoza wananchi riba kubwa wanapochukua mikopo.
Dkt. Kijaji,
alisema kuwa mwezi Desemba, 2017
Serikali ilizindua sera ya huduma ndogo ya fedha itakayosaidia kuwatambua wakopeshaji na kuwalinda wakopaji wanaohitaji huduma
katika taasisi hizo zikiwemo za mikopo.
“Tunataka
kuhakikisha tunawalinda wakopaji na kuhakikisha wanakopa kwa kuzingatia sheria
na taasisi hizo za fedha zinazingatia sheria, utaratibu na kanuni za utawala
bora”, alisema Dkt. Kijaji.
Alisema
kukamilika kwa sheria ya huduma ndogo ya fedha hivi karibuni kutakua ni
muarobaini wa kutatua changamoto za kifedha kwa wananchi wanaohitaji mikopo kwa
ajili ya kujikwamua kiuchumi.
Akijibu
swali la Msingi la Mbunge huyo kuhusu hatua za Serikali za kuhakikisha Benki
nchini zinapunguza riba ili kuchochea shughuli za biashara, Dkt. Kijaji alisema
kuwa Sekta ya Benki inafanya biashara huria na ilianza tangu mwaka 1991 baada
ya kupitishwa kwa Sheria ya Usimamizi wa Benki na Vyombo vya Fedha ya Mwaka
1991.
“Kupitia
Sheria hiyo, wawekezaji walifungua benki binafsi nchini na gharama za huduma na
bidhaa kuamuliwa na nguvu ya soko hivyo Serikali haina mamlaka ya moja kwa moja
ya kupunguza viwango vya riba katika soko”, alisisitiza Dkt. Kijaji.
Hata hivyo
alizitaja hatua ambazo Serikali imezichukua kwa upande wake kuwa ni pamoja na
kuzitaka benki za biashara kutumia Mfumo wa kuhifadhi na kutoa taarifa za
wakopaji, Benki Kuu kuanza kutoa mikopo ya muda mfupi kwa benki za biashara kwa
kiwango cha asilimia 6.89 na pia kushusha riba kutoka asilimia 16.0 hadi
asilimia 9.0.
Hatua
zingine ni Benki Kuu kupunguza kiwango cha chini cha amana kinachotakiwa
kuwekwa na Benki za biashara kutoka asilimia 10.0 hadi asilimia 8.0 na pia Serikali kuendelea kulipa malimbikizo
ya madai yaliyohakikiwa kwa lengo la kupunguza kiwango cha mikopo chechefu na
kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi.
Aidha Naibu
Waziri huyo ameipongeza benki ya CRDB, NMB na Benki ya ABC kwa kupunguza riba
ya mikopo kutoka asilimia zaidi ya 20 hadi kufikia asilimia 17 hivyo kuwa na
tumaini kuwa Benki zingine zitaendelea kufanya hivyo.
Imetolewa na;
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango
|
No comments:
Post a Comment