Mkurugenzi
Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania, Bwana Masanja Kaodogosa (wa pili kulia) akimuonesha
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa kwanza
kulia) kazi ya kukarabati reli ikiendelea unaofanywa na wafanyakazi wa Shirika
hilo baada ya kuharibika kwa mvua wakati wa ziara yake ya kukagua ukarabati huo
katika kijiji cha Mkadage kilichopo wilayani Kilosa mkoani Morogoro.
|
Naibu Waziri
wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akipanda kiberenge kwenda
kukagua ukarabati wa reli iliyoharibika kwa mvua katika eneo la umbali wa
kilomita mia moja lililopo kati ya Kilosa, Morogoro na Gulwe, Dodoma.
|
Naibu Waziri
wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akishuka kwenye
tingatinga inayojaza udongo kwenye eneo lililopo katika kijiji cha Munisagala
kilichopo wilayani Kilosa mkoani Morogoro baada ya kukagua kazi inayoendelea ya
kujenga na kurejesha miundombinu ya reli iliyoharibika na mvua wakati wa ziara
yake kwenye eneo hilo. Katikati ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania
Bwana Masanja Kadogosa.
|
Mhandisi
Mkuu Ujenzi wa TRL Mhandisi Nelson Ntejo akimuonesha Naibu Waziri wa Uchukuzi
na Mawasiliano (kulia) uharibifu wa miundombinu ya reli uliotokea kutokana na
mvua wakati wa ziara yake ya kukagua uharibifu huo na ukarabati unaoendelea
kati ya Kilosa, Morogoro na Gulwe, Dodoma. Katikati ni Mkurugenzi Mkuu wa
Shirika la Reli Tanzania Bwana Masanja Kadogosa.
Serikali
ya Tanzania imetoa miezi sita kwa wananchi wanaolima ndani ya eneo la hifadhi ya reli
inayopita Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro kuhama eneo hilo baada ya kuvuna
mazao yao ili kuhifadhi miundombinu ya reli na kupunguza uharibifu wa
miundombinu hiyo.
Hayo
yameelezwa na Naibu Waziri wa uchukuzi na Mawasiliano wa Wizara ua Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye wakati wa ziara yake
alipotembelea kukagua ukarabati wa reli iliyopo eneo la Kilosa, Morogoro na
Gulwe, Dodoma lenye umbali wa kilomita mia moja baada ya kuharibika kwa mvua na
Serikali kusitisha usafirishaji wa abiria na mizigo kutoka Dar es Salaam kwenda
mikoa mbali mbali na nchi za jirani.
Nditiye
amesema kuwa uharibifu wa eneo hilo ni wa kiwango kikubwa kwa kuwa katika
kipande cha umbali wa kilomita mia moja zilizoharibika kwa mvua baadhi ya
maeneo reli imebomoka, kuhama kwenye njia yake na ardhi husika kuliwa na maji
ya mvua yaliyojaa kwenye mto Mkondoa ambao unapita pembezoni mwa reli
hiyo.
Ameongeza
kuwa uharibifu huo unasababishwa na shughuli za kibinadamu ambapo wananchi
wanaishi na kulima ndani ya mita thelathini upande wa kulia na kushoto mwa reli
ambapo ni hifadhi ya miundombinu ya reli na wananchi hawaruhusiwi kutumia eneo
hilo kwa shughuli yeyote.
“Nakuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli
Tanzania Bwana Masanja Kadogosa ushirikiane na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa kuwahamisha
wananchi wanaoishi ndani ya hifadhi hii wakishavuna mazao yao kwa kuwa kilimo
kinasababisha mmomonyoko wa udongo hivyo kuharibu miundombinu ya reli”,
amesisitiza Mhandisi Nditiye.
Amesema kuwa
Wizara yake itawasiliana na kushirikiana na Wizara ya Maji, Kilimo na
Umwagiliaji ili waweze kukarabati mabwawa makubwa matatu ya Hombolo, Kidete na
Manyara ili yaweze kuhifadhi maji na kuyadhibiti kama ilivyokuwa hapo awali ili
yasipitilize kuingia kwenye mto huo bila kufunguliwa kwa utaratibu na kuharibu miundombinu ya reli.
Naye
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Bwana Masanja Kadogosa amesema kuwa
tayari Shirika lake limeleta vifaa na wafanyakazi katika eneo hilo ambapo
wanafanyakazi kazi mchana na usiku ili kuhakikisha kuwa reli hiyo inaanza
kutumika tena kwa shughuli za usafirishaji wa abiria na mizigo.
Ameongeza kuwa
kwa siku Shirika lake linapoteza takribani shilingi milioni mia mbili ambazo ni
chanzo cha mapato kwa Shirika hilo na Serikali kwa ujumla.
Bwana
Kadogosa alifafanua kuwa reli hiyo imekuwa ikikumbwa na changamoto ya
kuharibika kila baada ya kipindi cha miaka kumi ambapo iliwahi kuharibika tena
mwaka 1998, 2007 na sasa mwaka huu 2018 kutokana na mabadiliko ya majira ya
mvua, tabia nchi na hali ya hewa.
Ameongeza
kuwa Serikali inaendelea na mazungumzo na wafadhili wa kutoka Japan na
mkandarasi anayejenga reli ya kisasa ili kuweza kupata mwarobaini wa kudumu wa
kudhibiti na kuondoa kabisa uharibifu wa miundombinu ya reli hiyo.
|
No comments:
Post a Comment