Serikali
ya Tanzania imewatoa hofu watumishi wote wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (RAHCO), na
Shirika la Reli Tanzania (TRL), kwa
kuwahakikishia kuwa ajira zao hazitaathirika kwa kuwa sheria mpya ya Reli ya
Mwaka 2017 imeweka utaratibu maalum kwa watumishi hao kuhamia kwenye taasisi
mpya ya Kampuni ya Reli Tanzania (TRC).
Katibu Mkuu
wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Sekta ya Uchukuzi, Dkt. Leonard
Chamuriho amesema hayo katika mahojiano maalum mjini Dodoma na kusisitiza
taratibu zote za kiutumishi zitafuatwa kwa watumishi watakoendelea na kazi
kwenye kampuni mpya.
"Sheria
mpya ya reli mwaka 2017 imezigatia maslahi ya watumishi kwa kuweka mazingira
mazuri kwa wafanyakzi wa RAHCO na TRL
hivyo atakaetaka kuendelea kutumikia umma katika shirika hili jipya ataendelea
na kazi na atakaetaka kucha kazi basi taratibu za kiutumishi zitafuatwa kwa
mujibu wa taratibu na Kanuni" amesema Dkt. Chamuriho.
Dkt.
Chamuriho amesema kuwa lengo la kuunganisha taasisi hizo ni kuongeza ufanisi wa
shirika hasa kwenye usaifirishaji wa mizigo na kuondoa tofauti zilizokuepo kati
ya RAHCO na TRL ambazo zimekuepo kwa muda mrefu kwenye usimamizi na uendeshaji
wa shirika hilo.
Kwa upande
wa Reli ya Kisasa (SGR) Dkt. Chamuriho amesema kuanzishwa kwa sheria mpya
kutaongeza ufanisi wa utekelezaji wa mradi huo kwa awamu ya kwanza ambayo
inahusisha awamu tano ambapo awamu ya kwanza itajengwa kuanzia Dar es Salaam-
Morogoro, Awamu ya pili Morogoro-Makutupora, awamu ya tatu Makutupora-Tabora,
awamu ya nne Tabora-Isaka na awamu ya tano Isaka-Mwanza.
Aidha
ameongeza kuwa baada ya awamu hizo kukamilika Serikali itaanza awamu ya pili
itakayohusisha sehemu za Tabora-Kigoma, Mpanda-Kaliua na
Ruvu-Tanga-Moshi-Arusha.
Kupitishwa
kwa Sheria ya Reli ya mwaka 2017 na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kunaifuta sheria ya Reli No. 4 ya mwaka 2002 na sheria hii itaanza kutumika
baada ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kuisaini.
Imetolewa na
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
|
No comments:
Post a Comment