Haya Ndio Maagizo ya Rais Magufuli Baada ya Kuipokea ripoti ya CAG -March 27,2017. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Monday, March 27, 2017

Haya Ndio Maagizo ya Rais Magufuli Baada ya Kuipokea ripoti ya CAG -March 27,2017.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo March 27, 2017 amepokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha unaoishia June 30 2016 Ikulu Jijini Dar es Salaam.  Ripoti hiyo imewasilishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Prof. Mussa Juma Assad Ikulu Dar es salaam.

 Akizungumza baada ya kupokea ripoti hiyo, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza Ofisi ya CAG kwa kazi nzuri inayofanya na ameahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na ofisi hiyo ili kukabiliana na mianya yote inayosababisha upotevu wa fedha za umma.

Hata hivyo Rais Magufuli amemuagiza CAG kufanya ukaguzi wa kina katika sekta ya madini na kubaini mianya yote ambayo inasababisha nchi kukosa mapato makubwa hususani katika misamaha ya kodi, mikataba mbalimbali na ulipaji wa kodi.

Haiwezekani Watanzania wanakosa dawa hospitali wakati dhahabu zao zinaondoka, Watanzania wanakosa maji wakati dhahabu zao zinaondoka, Watanzania wanakosa umeme wakati dhahabu zao zinaondoka, Watanzania wanakosa barabara wakati dhahabu zao zinaondoka, nataka ukakague kwa kina hii sekta ya madini ili watanzania wajue chao nini na kama kinapatikana sawasawa?”;- Rais Magufuli.

Waziri Mkuu ukaongoze hicho kikao na wewe CAG uwaambie kila mmoja katika eneo lake juu ya dosari zake, sitaki kuona dosari zinajirudia zilezile kila wakati”;-Rais Magufuli.


Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, CAG anapaswa kuwasilisha ripoti ya hesabu za Serikali kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kabla ya tarehe 31 Machi ya kila mwaka, na baada ya hapo ripoti hiyo huwasilishwa bungeni katika kikao kinachofuata.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
27 Machi, 2017.

HAPA CHINI TAZAMA VIDEO MAZUNGUMZO YA RAIS WAKATI WA HAFLA HIYO YA KUIPOKEA RIPOTI.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad