Akizungumza
katika hafla hiyo Mhe. Rais Magufuli
aliwashukuru viongozi wote wa Umoja wa Afrika kwa kuamua jengo hilo liitwe jina
la Mwalimu Julius Nyerere ikiwa ni
kutambua mchango wake katika kupigania amani na usalama na amebainisha kuwa
Mwalimu Nyerere alikuwa Mwafrika halisi na kiongozi mahiri na shupavu.
“Na kwa hakika naweza kusema kuwa alikuwa
mmoja wa viongozi bora kabisa ambaye amewahi kutokea katika Bara letu, katika
maisha yake yote Mwalimu Nyerere alipambana ili kujenga umoja na mshikamano
miongoni mwa Afrika, alikuwa mmoja wa waanzilishi wa umoja huu, sisi Watanzania
kwa hakika tunajivunia sana Mwalimu Nyerere kuwa Baba wa Taifa” alisema
Mhe. Rais Magufuli.
|
Mhe. Dkt.
Magufuli aliongeza kuwa Mwalimu Nyerere alitoa mchango mkubwa katika kupambana
na ubaguzi na unyonyaji wa kila aina, alisaidia ukombozi wa nchi nyingi za
Afrika, na hata alipong’atuka katika hatamu za uongozi wa Taifa la Tanzania
aliendelea kutoa mchango wake kupigania amani katika nchi za Afrika.
“Wito wangu kwenu, waheshimiwa viongozi ni
kwamba, sambamba na kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa jengo hili, itakuwa ni jambo
jema zaidi kama tutajitahidi kufuata nyayo zake pamoja na kuishi maisha ya
viongozi wengine hodari wa Bara hili wakiwemo Hayati Kwame Nkhrumah, Ahmed Ben
Bella, Sekou Toure, Gamal Abdel Nasser na bila kusahau shujaa wetu mwingine
Hayati Nelson Mandela”
alisisitiza Rais Magufuli.
Mkutano wa
28 wa wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika unaendelea leo tarehe 30 Januari, 2017 hapa Addis Ababa.
|
No comments:
Post a Comment