Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi iweke mpango maalumu wa kuongeza wataalamu zaidi katika sekta ya afya ndani ya nchi ili kuipunguzia Serikali gharama za kusomesha wataalam hao nje ya nchi.

Waziri Majaliwa Ametoa agizo hilo wakati alipokua akikagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Kampasi ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Afya na Sayansi ya Tiba Muhimbili (MUHAS) na Ujenzi wa Kituo cha Tiba cha Kimataifa cha Muhimbili katika eneo la Mloganzila.

Amesema Serikali zilizotangulia zimefanya kazi kubwa na nchi imefikia hatua nzuri ya kuongeza wataalam ndani ya nchi ambao watakwenda kutatua changamoto ya upungufu wa madaktari bingwa kwenye hospitali za mikoa na wilaya.

Waziri Mkuu amesema ujenzi wa kituo hicho cha tiba cha kimataifa pia utawapunguzia wananchi adha ya kutafuta fedha za kwenda kupata matibabu nje ya nchi.

 Aidha Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Bwana. Humphrey Polepole awatafute watu wote waliohusika na wizi wa lita 1,000 za mafuta ya kuendeshea mitambo katika karakana ya mkandarasi anayejenga Kampasi hiyo ya MUHAS
“Wafanyakazi waache wizi. Lita 1,000 zinaondokaje katika karakana ya mkandarasi? Hii kampuni inayolinda kama imeshindwa kazi iondolewe na Mkuu wa wilaya usimhurumie mwizi,” amesema Waziri Majaliwa.

Lakini pia Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako amesema kukamilika kwa kampasi ya Mloganzila kutasaidia upatikanaji wa madaktari bingwa wengi nchini ambao watapunguza gharama za kupeleka wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi.

Awali, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa. Ephata Kaaya alisema kukamilika kwa hospitali pamoja na kampasi ya chuo kutawezesha kupunguza kwa kiasi kikubwa uhaba wa wataalamu wa afya nchini.

Pamoja na  msongamano wa wagonjwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Ujenzi wa mradi huo umegharimu Dola za Kimarekani milioni 61, ambapo Serikali imetoa Dola milioni 18 na Serikali ya Korea imetoa mkopo wa Dola milioni 43. Kukamilika kwa ujenzi wa kampasi hiyo ya Mloganzila kutawezesha  chuo kuongeza idadi ya udahili wa wanafunzi wa fani ya afya kutoka 4,010 hadi 15,000.

Prof.  Kaaya amesema mkataba wa awamu ya kwanza ya ujenzi wa mradi huo ulisainiwa tarehe 12, Desemba, 2014 na ujenzi ulianza mwezi Julai, 2015 na unatarajiwa kukamilika Oktoba, 2016.

Na Hashim Ibrahim (UDSM-SJMC)

BAADHI YA WAFANYAKAZI   NA WANANCHI WA ENEO LA MLOGANZILA (1)
Baadhi ya wafanyakazi na Wananchi wa eneo la Mloganzila vlcsnap-2016-09-02-18h34m51s172
Waziri Mkuu akionyeshwa moja ya mashine zilizopo hapo
vlcsnap-2016-09-02-18h33m39s160
moja ya mashine zilizopo hapo
vlcsnap-2016-09-02-18h35m13s126
Baadhi ya wafanyakazi wakifuatilia tukio hilo