Upotoshaji kuhusu makato ya Kodi ya
Ongezeko la Thamani (VAT) katika miamala ya benki na simu za mikononi,
uliotangazwa na baadhi ya benki, umeilazimu Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
kutoa ufafanuzi na kuzuia benki hizo kutoza kodi kwa wateja wao.
Akizungumza na
waandishi wa habari Dar es Salaam jana,Julai Mosi,2016 Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata,
alihoji kwa nini mabenki yametoa matangazo ya kuanza kutoza kodi hiyo, wakati
hata kanuni za utekelezaji wa sheria hiyo hazijatolewa.
Kidata alisema pamoja
na kupitishwa kwa sheria hiyo bungeni, lakini muongozo unaotokana na kanuni
bado haujatolewa, ndio maana TRA imeshindwa kuelewa kwanini taasisi hizo
zimetoa taarifa zao kwa wananchi.
Kutokana na hali hiyo
ya kutoa matangazo ya kutekeleza sheria hiyo, wakati kanuni za kutekeleza
sheria yenyewe hazijatolewa, Kidata alisema kumeonekana dalili za nia ovu.
“Tangu lini mmeona benki au taasisi
ya fedha inaanza kutoa matangazo ya utekelezaji wa sheria za serikali? Hii ni
kwa sababu ya nia ovu.
“Kuna taarifa ambazo si za kweli
zinazoenezwa kupitia mitandao ya kijamii kuwa VAT itatozwa kwenye amana ya
mwenye fedha kwenye benki. Hii si kweli,” alisema Kidata.
Usahihi wa kodi.
“Juzi Bunge la Tanzania lilipitisha
marekebisho ya sheria hiyo ya mwaka 2014 kuanzia Julai mosi mwaka huu kwenye
huduma za kifedha kwa kurekebisha kifungu cha 13 cha jedwali la msamaha wa
kodi, lakini taasisi hizo zimekuwa zikipotosha umma,” alisema.
Alisema kutokana na
upotoshaji huo, TRA imeamua kueleza ukweli kuhusu utekelezaji wa sheria hiyo,
ili kuondoa utata na upotoshaji unaohusu utekelezaji wa sheria hiyo.
Kidata alisema sheria
hiyo inalenga kutoza VAT kwa kiwango cha asilimia 18, kwenye ada ambazo benki
zinatoza wateja wake katika huduma mbalimbali zitolewazo na benki au taasisi za
fedha.
“Ukweli ni kuwa kiasi cha VAT
kitakachotozwa ni asilimia 18 ya kiasi cha gharama ya huduma iliyotolewa na
benki au taasisi yoyote ya fedha na si kwa mteja,” alisema.
Akitolea mfano suala
hilo, Kidata alisema kama ada ya huduma ya benki ambayo mteja ametozwa ni Sh
1,000, VAT itakayotozwa kwenye kiasi hicho ni Sh 152.50 tu na benki kubaki na
Sh 847.50 na si kuwaongezea wananchi mzigo.
“Kiwango hiki cha Sh 152.50 ndicho
kitakachorejeshwa serikalini na benki au taasisi ya fedha baada ya kupunguza
VAT iliyolipwa kwenye manunuzi ambayo yamefanywa kwa benki au taasisi ya fedha
husika.
Kwa mujibu wa sheria hii, VAT haitatozwa kwenye riba inayotozwa na
benki kwenye mikopo,” alisema.
Alisema kuna maelezo
yametolewa na moja ya benki hapa nchini kuwa mtumiaji wa huduma za kifedha,
atatakiwa kulipia kwa fedha taslimu kama muamala husika haukupitia kwenye
akaunti na kuongeza kuwa taarifa hiyo siyo sahihi, kwa kuwa ukusanyaji wa VAT
husika, utafanywa kwa njia ile ile ambayo gharama za huduma za kifedha
zinakusanywa sasa.
Kidata alisema TRA
itatoa maelekezo ya namna utoaji wa risiti za kielektroniki utakavyofanyika,
ili kuwezesha mabenki au taasisi za kifedha kutimiza matakwa ya kisheria ya VAT
ya mwaka 2014 kama ilivyorekebishwa mwaka 2016.
“Hivyo tunazitaka benki na taasisi za
fedha zilizoamua kwa makusudi kutoa taarifa zisizo sahihi kwa umma, kuacha mara
moja vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa.
“Kimsingi benki na taasisi za
fedha zinazohusika zinaagizwa kurekebisha mara moja taarifa
walizokwishazisambaza ili zibebe maudhui sahihi ya marekebisho ya sheria hii,” alisema.
Barua BoT.
Alisema katika hatua za
awali, tayari wamewapa maelekezo Benki Kuu (BoT) ambayo ni msimamizi wao mkuu,
ihakikishe hicho kinachofanyika kinasitishwa na hatua mbalimbali za kisheria
zitachukuliwa.
“Mwanzo benki na taasisi hizo za
fedha zilikuwa zikichukua tozo yote wanayotoza, hivyo sasa tumewataka katika
hiyo hiyo waliyokuwa wakichukua, ndiyo watoe kodi na si kumuongezea mwananchi
mzigo kwa sababu kila kodi ina msingi wake na si kila kodi inapopanda, imlenge
mwananchi. Sisi tumelenga hiyo hiyo wanayotoza,” alisema.
Alitoa mwito kwa mtu
yeyote mwenye uhakika kuwa ameongezewa makato na benki au taasisi za fedha kwa
madai ya utekelezaji wa sheria hiyo, atoe taarifa ili hatua zaidi za kisheria
zichukuliwe.
|
No comments:
Post a Comment