Mwenyekiti mpya wa chama cha
Mapinduzi CCM Dkt John Pombe Magufuli akihutubia mbele ya Wajumbe wa Mkutano
mkuu Maalum wa chama cha CCM mara baada ya kutangazwa rasmi kuwa Mwenyekiti wa
chama hicho.
Mwenyekiti wa tano wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), Rais John Magufuli, amewaomba wanachama wa chama hicho
kumuombea kwa Mungu ili apate uvumilivu wa mtangulizi wake, Mwenyekiti mstaafu,
Jakaya Kikwete.
“Mzee Kikwete wewe una moyo wa
uvumilivu. Sina hakika kama mimi ninao uvumilivu kama wako...umetupa fundisho
kubwa sana,” alisema Magufuli wakati akizungumza kwa mara ya kwanza baada ya
kuchaguliwa kwa kura asilimia 100 kuwa Mwenyekiti wa chama hicho.
Katika kuonesha tofauti yake na
Kikwete katika uvumilivu, Magufuli alikumbusha changamoto aliyokutana nayo
Kikwete, wakati alipoingia katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya
CCM mwaka jana, kupeleka mapendekezo ya majina ya wagombea watano wa urais
waliokuwa wamepitishwa na kikao cha Kamati Kuu, ili wapigiwe kura.
Ndani ya kikao hicho wakati Kikwete,
wajumbe wa Kamati Kuu na wa Baraza la Wazee la Ushauri wakiingia, baadhi ya
wajumbe wa kikao hicho walikiuka utaratibu wa siku zote wa chama hicho, kwa
kuimba kuwa na imani na mmoja wa wagombea wa urais, Edward Lowassa, ambaye jina
lake lilikatwa katika kikao cha Kamati Kuu.
Kupotezwa .
“Siku ile umeingia ukumbini, watu
wakawa wanaimba kuwa wana imani na mtu mwingine, siku hiyo hiyo robo au nusu
yao wangepotea...sifahamu, umetoa fundisho kwa sisi vijana kwamba saa nyingine
uvumilivu ni kitu muhimu,” alisema akimaanisha kama hali hiyo ingemkuta yeye
ndiye Mwenyekiti, hayo ndiyo yangetokea.
Kutokana na uvumilivu aliouonesha
Kikwete katika mkutano huo, Magufuli aliwataka wanachama hao wa CCM kumuombea
kwa Mungu, ili apate angalau nusu ya uvumilivu wa Kikwete, ili katika uongozi
wake mambo yaende salama.
Kuzushiwa JK.
Alimsifu Kikwete kwa kutumia hekima
ya uvumilivu, kwa kuwa kiongozi huyo mstaafu, amesemwa mambo mengi, akazushiwa
na hata kutukanwa kutokana na hatua, uamuzi na vitendo vyake Magufuli.
“Umesemwa mengi, umetukanwa mengi na
umezushiwa mengi kwa ajili yangu, lakini kwa upendo wako na kwa kumtegemea
Mungu, ukakaa kimya...sina cha kukulipa, bali nitafanyia kazi Watanzania na
hasa wana CCM kwa nguvu zote,” alisema Dk Magufuli.
Alitoa mfano wa Kikwete kuzushiwa
alikuwa akikataa kumkabidhi Dk Magufuli uenyekiti wa CCM kwa kufuata desturi ya
chama hicho, akasema Mwenyekiti huyo mstaafu amemshawishi mara nne, lakini yeye
ndiye aliyekuwa akikataa.
“Nakumbuka umeniambia mara nne, ya
kwanza ulikuja kuniambia nikakukatalia bosi wangu, ulinipigia simu na mimi
nikawa naanzisha mjadala mwingine. Nakupa pole na unisamehe sana kwa kuwa
kukukatalia kulisababisha utukanwe,” alisema Rais Magufuli.
Serikali Dodoma.
Kabla ya kumaliza hotuba yake,
Magufuli alitangaza ahadi kwa wanachama hao, kuwa amebakiza miezi minne na
miaka minne kabla ya kumaliza kipindi chake cha miaka mitano na kusema kabla ya
kumaliza kipindi hicho, atakuwa amehamishia serikali yote Dodoma.
Magufuli alisema kwa sasa miundombinu
ya Dodoma inawezesha serikali kuhamia huko, kwa kuwa barabara za kutoka Makao
Makuu hayo ya serikali kwenda sehemu mbalimbali nchini, zinapitika kwa lami.
Mbali na barabara, alisema pia huduma
kwa ajili ya maisha ya watu nazo zinapatikana kwa kuwa mkoa huo una uzoefu wa
kuhudumia wabunge, wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM na mikutano mingine, huku
mkoa huo ukiwa na Chuo Kikuu cha Dodoma, ambacho ndio kikubwa kuliko vyote
nchini.
Alisema, akihamia yeye katika Ikulu
ya Chamwino ambayo alisema ina kila huduma anayohitaji, anatarajia Makamu wa
Rais, Waziri Mkuu, mawaziri na serikali nzima itamfuata.
Babu wa Demokrasia.
Magufuli alisema CCM ndio chama
kilicholea demokrasia hapa nchini na kinaendelea kutoa ulezi huo na kufafanua
kuwa chama hicho ndio babu na bibi wa demokrasia; baba na mama wa demokrasia na
kaka na dada wa demokrasia kwa vyama vyote nchini.
Alisema kwa kuwa Serikali
anayoiongoza inatekeleza Ilani ya chama hicho, hivyo chama hicho ndio mabosi wa
mabosi wote serikalini na kuonya kuwa ambaye hataki hilo, ataondolewa.
Kupendekezwa kwake.
Awali wajumbe wa Mkutano huo Mkuu
Maalumu wa CCM wapatao 2,398 walimpigia kura ya kumchagua Magufuli kuwa
Mwenyekiti mpya wa chama hicho.
Mwenyekiti aliyemaliza muda wake,
Kikwete ndiye aliyesoma pendekezo la NEC kwa wajumbe wa mkutano huo kuhusu
mgombea wa nafasi hiyo.
“Madhumuni ya mkutano huu ni kuchagua
mwenyekiti mpya. Sisi katika Halmashauri Kuu tunampendekeza kwenu Mheshimiwa
Dakta John Pombe Joseph Magufuli ashike nafasi hiyo,” alisema Kikwete saa 7:10
na kauli yake hiyo kupokelewa kwa shangwe, vifijo na vigelegele.
Akimwelezea Magufuli, Kikwete alisema
ana imani isiyo na hata chembe ya shaka kuwa atafanya kazi hiyo vizuri, kwa
sababu ya imani na mapenzi yake makubwa kwa chama hicho na Watanzania.
Alisema Magufuli ametumikia Taifa na
wananchi kwa miaka mingi kwa uaminifu na uadilifu mkubwa, katika wadhifa
mbalimbali aliokuwa nao. Alisema Magufuli amekuwa mbunge na waziri kwa miaka
20, ambapo miaka 10 wakati wa serikali ya Rais Benjamin Mkapa na mingine 10
wakati wa serikali yake.
Alisema pia Magufuli amekuwa mjumbe
wa kamati ya siasa ya wilaya na mkoa, mjumbe wa mkutano mkuu wa wilaya na mkoa
na mjumbe wa mkutano mkuu wa taifa kwa miaka 20, hivyo anakijua mno chama.
Kikwete alisema Magufuli ameongoza
nchi kwa uaminifu na uadilifu mkubwa katika kipindi kifupi cha miezi 8 tangu
alipochaguliwa, hivyo sasa anafaa kuvaa kofia zote mbili.
“Kichwa chake sasa kinatosha avae
kofia zote mbili - ya urais na uenyekiti wa chama. Nawaomba wajumbe wote
tumuunge mkono.
“Tumpe kura zote za ‘Ndiyo’ na
isipotee hata moja,” alisema Kikwete ambaye ameng’atuka baada ya kuongoza Chama
tangu Juni 2006.
“Mimi naondoka na bila shaka yoyote
namwachia Chama Cha Mapinduzi Rais Dakta John Pombe Joseph Magufuli. Nakiacha
Chama Cha Mapinduzi katika mikono salama na nina hakika kitapata maendeleo
makubwa ya haraka,” alisema.
Kura Zatangazwa.
Kazi ya kupiga kura na kuzihesabu
ilipokuwa ikiendelea, viongozi wakuu wa CCM na wastaafu baada ya baadhi yao
kupiga kura, waliondoka kwa ajili ya mapumziko.
Baada ya mapumziko, walirejea ambapo
baada ya salamu za wageni na baadhi ya wanasiasa waliorejea CCM baada ya
kukimbilia upinzani kumalizika, Kikwete alisoma matokeo.
Akitangaza matokeo hayo, Kikwete
alisema kura zilizopigwa zilikuwa 2,398, zilizoharibika sifuri na hivyo kura
halali zikawa 2,398.
Kikwete aliendelea kuwa matokeo
yameonesha kuwa, kura za Hapana ni sifuri na kura za ndio ni 2,398, na hivyo
Magufuli amepitishwa na wajumbe wa CCM kwa nidhamu ya juu ya kumpa asilimia 100
ya kura.
Makamu Wenyeviti.
Awali, Katibu Mkuu wa CCM,
Abdulrahman Kinana alisema mkutano mkuu huo usio wa kawaida, unafanyika kwa
mujibu wa Kifungu cha 7 (103) (4) cha Katiba ya CCM na ajenda yake ni kumchagua
mwenyekiti mpya, kufuatia uamuzi wa Kikwete kung’atuka, akitekeleza utamaduni
wa chama kuachiana madaraka, ili kumpisha Rais John Magufuli.
Aidha, alisema kwa mujibu wa Kifungu
7 (105) (5) (a) cha Katiba hiyo, unapofika wakati wa uchaguzi kazi mojawapo ya
mkutano mkuu ni kuchagua makamu wenyeviti.
Lakini, alisisitiza makamu wote
wawili wa sasa, muda wao haujamalizika kikatiba na utamalizika mwezi Novemba
2017 “Makamu wote wawili hawajamaliza muda wao. Muda wao utamalizika Novemba
2017, hivyo hakuna sababu ya kuwachagua tena. Hapa leo tunachagua mwenyekiti
peke yake,” alitangaza Kinana.
Makamu Mwenyekiti wa CCM kwa upande
wa Bara ni Phillip Mangula na upande wa Zanzibar ni Rais wa Zanzibar, Dk Ali
Mohamed Shein.
Viongozi wengine waliohudhuria
mkutano huo ni pamoja na Marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa,
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Rais wa
Zanzibar Dk Shein , Mawaziri wakuu wastaafu Mizengo Pinda, Cleopa Msuya, Dk
Salim Ahmed Salim, Jaji Joseph Warioba, John Malecela, Makamu wa Rais mstaafu
Mohamed Gharib Bilal na makatibu wakuu wastaafu wa CCM, Yusuf Makamba na Wilson
Mukama.
|
No comments:
Post a Comment