Waziri Mkuu Mstaafu na Mjumbe wa
Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowasa amemtaka Rais John Magufuli kuwa na
utamaduni wa kufanya mazungumzo na wanasiasa wenzake ili kufikia muafaka wa
mambo mbali mbali ya kisiasa nchini.
Lowasa ameyasema hayo leo wakati wa
mahojiano na Tido Mhando kupitia kipindi cha Funguka kinachorushwa na
Televisheni ya Azam. Lowasa amesema kuwa
siasa ni mazungumzo na siyo kutoa tu amri kama anavyofanya Rais Magufuli.
Kadhalika Lowassa amesema kila mtu
ana wajibu wa kuheshimu amani ya nchi na hakuna mtu mwenye hati miliki ya nchi
hii.
“Serikali haipaswi kuwa na ghadhabu,
inapaswa kuwa na tabia ya kuzungumza. Sisi sote ni Watanzania kwa nini tunaogopa
kuzungumza. Mazungumzo ndiyo njia bora ya kufikia maridhiano. Pia Rais Magufuli
aitazame Zanzibar, tunasikia watu wanashughulikiwa kwa njia mbalimbali,
wanakamatwa, hivyo hawezi kuikwepa Zanzibar kwani hilo ni suala lake.” alisema
Lowassa.
Amesema CHADEMA ipo sahihi kutangaza
operesheni ‘Ukuta’ hapo Septemba 1, mwaka huu na kwamba bado kuna nafasi ya
kufanya mazungumzo kabla ya tarehe hiyo kufika ili kuepusha hali ya migogoro
itakayojitokeza siku hiyo itakapofika.
Akizungumzia barua ya Msajili wa
Vyama vya Siasa kukemea operesheni hiyo, amesema barua hiyo imejaa ghadhabu
zaidi kuliko kuongelea mambo ya msingi ambayo vyama vya upinzani vimekuwa
vikionewa.
Akiongelea suala la wabunge wa
upinzani kutoka na kususia bunge, Lowassa amesema hali hiyo ilisababishwa na
kutokuwepo kwa Spika Job Ndugai ambaye kwa muda mrefu alikuwa nje ya nchi
akiendelea na matibabu.
“Ndugai angekuwepo haya yote
yasingetokea kwakuwa ni mtu makini sana na hata kwa Naibu Spika kuna tatizo la
Kisaikolojia kwasababu aliingia bungeni kwa njia zisizoeleweka na hivyo
kumfanya kushindwa kuhimili kiti vizuri,” amesema.
Hata hivyo amempongeza Rais Magufuli
na kudai kuwa amefanya vizuri katika baadhi ya maeneo lakini kuna maeneo
mengine ambayo angepaswa kuyapa kipaumbele zaidi akitolea mfano wa elimu na
kudai kuwa badala ya kuanza na suala la madawati angeanza na kushughulikia
maslahi ya walimu kwanza, na kutoa kipaumbele kwa tatizo la ajira nchini hasa
kwa vijana.
Kuhusiana na harakati za Serikali
kuhamia Dodoma, Mjumbe huyo wa Kamati Kuu CHADEMA amesema viongozi wote
waliotangulia tangu enzi za Mwalimu Nyerere walikuwa na ndoto za kuhamia Dodoma
lakini kuna mambo yaliyokuwa yanaingilia mipango hiyo na mwisho kushindikana.
“Napongeza harakati na dhamira ya
Serikali ya Awamu ya Tano ya kuhamishia Serikali yote Dodoma lakini napenda
kuwaambia wasiende kwa kasi sana wasije wakavunjika miguu,” ameongeza.
Kuhusiana na hali ya kisiasa
Zanzibar, Lowassa ametoa rai kwa Rais Magufuli aangalie hali ya Zanzibar kwani
yanayoripotiwa kuendelea visiwani humo yanatia kichefuchefu ikiwemo watu
kukamatwa na kuteswa.
“Tusiitenge Zanzibar na badala yake
juhudi za makusudi zifanyike kuweka mambo sawa kwa kufanya mazungumzo kwani
siasa ni mazungumzo,” amesisitiza Lowassa ambaye amedai kuwa ana matumaini
makubwa ya kuingia Ikulu mwaka 2020.
Kuhusu kashfa ya Richmond kumfanya
aondoke CCM kwa hasira baada ya kukosa ridhaa ya chama hicho katika kugombea
Urais, Lowassa amesema hakuondoka CCM kwa hasira isipokuwa alituhumiwa na
kuhukumiwa bila kupewa nafasi ya kusikilizwa.
“CHADEMA sikujipeleka mwenyewe bali
Kamati Kuu CHADEMA ilinifata na kuniomba nijiunge nao katika kupeperusha
bendera yao na mimi niliona ni ‘opportunity’ nzuri hivyo nikakubali nikajiunga
nao na tukafanikiwa kupata kura zaidi ya milioni sita, idadi ambayo siyo ndogo
hata kidogo,” amejinasibu Lowassa.
|
No comments:
Post a Comment