|
Producer nguli wa
muziki nchini John Shariza a.k.a Mann Water (chini kushoto) akiweka saini
kwenye hati ya mkataba wa lebo ya KOMBINENGA kurasimisha usimamizi wa kazi za
msanii Abbas Hamisi Kinzasa almaarufu kama 20% (Twenty per Cent) akishuhudiwa
na Wakili msomi Iddi M. Gogo wa Alpha Attorneys
(juu kulia) aliyefanikisha zoezi hilo, pamoja na meneja uzalishaji wa
Combination Sounds, Rowel Moses (juu kushoto) kwenye studio za Combination
Sounds Kinondoni Studio jijini Dar es salaam.
Na Sultani Kipingo
Mfalme wa Afro Pop
nchini Abbas Hamisi Kinzasa almaarufu kama 20% (Twenty per Cent) anavunja
ukimya na kurejea kwa kishindo kwenye anga ya muziki, huku akiwa msanii wa kwanza kusaini mkataba
na lebo mpya ya KOMBINENGA inayoendeshwa na producer nguli John Shariza a.k.a
Mann Water.
Twenty Percent, ambaye
mwaka 2011 alitwaa tuzo saba za Kilimanjaro Music Awards (KTMA) kwa mpigo, huku
Mann Water akisomba tuzo mara mbili mfululizo
za producer bora (mwaka 2013 na 2014), tayari amesharekodi vibao vitano
na anatarajia kuachia ngoma moja mpya ya kwanza Julai 18, 2016, katika kuandaa
albamu yake ya SAUTI YA GHARAMA.
"Nimerudi
kuwachinja tena" anasema Twenty Per cent, akiwa anakamilisha kurekodi
katika studio za Combination Sounds iliyoko Kinondoni Studio jijini Dar es
salaam. "Nimerudi kurudisha sauti ya gharama kwa jamii. Sauti inayofundisha. Sauti
inayoonya. Sauti inayoburudisha. Sauti inayozengua kila mtu, " anaogeza.
Tayari Tweny Per cent
ameshasaini mkataba wa miaka mitano na lebo ya KOMBINENGA, katika hafla fupi
iliyofanyika Jumapili katika ofisi za Combination Sounds. Kuanzia sasa shughuli
zote za msanii huyu zitasimamiwa na lebo hiyo chini ya Producer Mann Water.
Wakili msomi Iddi M.
Gogo wa Alpha Attorneys ndiye aliyefanikisha zoezi hilo la kutiliana saini
mkataba lililoshuhudiwa pia na meneja uzalishaji wa Combination Sounds, Rowel
Moses.
"Namkubali sana
Twenye Pa kwani ni msanii aliyetimia na hutumii shuruba wakati wa kurekodi
maana ana kipaji cha ajabu cha kutunga akiwa wima na kukariri hapohapo",
anasema Mann Water, ambaye ameshafanya kazi na
wasanii nyota kibao wakiwemo Lady
Jay Dee, Ali Kiba, Ommy Dimpoz,
Christian Bella, MB Dogg, Juma Nature, Mr Blue na wengine wengi.
Twenty Percent alitamba sana tokea mwaka 2006
kwa wimbo wake wa "Manemane" uliomfanya ashinde tuzo ya KTM, kabla ya
kuweka historia ya kusomba tuzo saba kwa mpigo mwaka 2011. wakati huo nyimbo
zilizompandisha chati zilikuwa ni "Tamaa Mbaya" na "Ya nini Malumbano" na
"Maisha ya Bongo"
Mbali na Muziki Twenye
Percent pia alitamba sana kwenye tasnia ya filamu ambapo alicheza kwenye mchezo
uliofahamika kwa jina lake la 20%. Baada ya hapo akaamua kupumzika kwa muda na
kujishugulisha na shughuli za kilimo.
"Kilimo kinaendelea vyema na sasa
nimeamua kurudi kwenye gemu ili kuwachinja tena" alimalizia, akiinuka
kuelekea kwake Kimzichana, Mkuranga, Mkoa wa Pwani, anakoishi.
|
No comments:
Post a Comment