|
Taasisi ya Maridhiano
inatarajia kuwasilisha ujumbe kwa Spika wa Bunge la Tanzania, Mhe.Job Ndugai kuomba
kuyakutanisha makundi mawili yanayosigana bungeni ili kuleta muafaka wenye tija
kwa taifa.
Mwenyekiti wa taasisi
hiyo Sheikh Sadick Godigodi , Jana Julai 04,2016 alisema kumeguka kwa Bunge kunakosababishwa na
Kambi ya Upinzani kuona inaonewa na maamuzi ya Naibu Spika, Dk. Tulia Akson
kunahitaji viongozi wa dini kuingilia kati na kupata suluhu.
"Tunatarajia
katika Bunge lijalo litakaloanza Septemba kuwasilisha ujumbe kwa Spika ili
tupewe nafasi ya kutatua mgogoro huu kwa maana wabunge wote wanatakiwa kuwepo
bungeni kuwakilisha matatizo ya wananchi," alisema Sheikh Godigodi.
"Haiwezekani kundi
moja likawa nje na jingine likaendelea, tunahitaji maridhiano ya pande zote
mbili za muhimili huo.”
Kambi ya Upinzani
Bungeni ilisusia Vikao vya Bunge la Bajeti kwa zaidi ya siku 70 kupinga kile
kilichoita kuburuzwa na Naibu Spika katika
uendeshaji wa chombo hicho cha kutunga sheria.
Kambi hiyo, ilianza
kutoka nje Mei 30,2016 baada ya Naibu Sika kukataa hoja ya Mbunge wa Arumeru
Mashariki, Mhe. Joshua Nassari (CHADEMA), ya
kutaka Bunge likatize shughuli zake na kujadili hoja ya kufukuzwa kwa wanafunzi
zaidi ya 700 wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Ingawa kitendo hicho
cha Naibu Spika kiliwaudhi wabunge wa chama tawala (CCM) na Upinzani, Kambi
hiyo haikurudi ndani mpaka Bunge lilipoahirishwa na Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa katikati ya wiki iliyopita.
Mshauri wa mambo ya
kisheria na kidiplomasia wa taasisi hiyo ya Maridhiano, Agustino Matefu alisema
mbali na kusuluhisha migogoro chochezi ya kidini kwa kutoa elimu sahihi kwa
umma, pia wamejikita katika kusuluhisha migogoro sugu kati ya wakulima na
wafugaji nchini.
“Tumetoa mchango mkubwa
wa kuleta suluhu ya migogoro ya ardhi baina ya wafugaji na wakulima mkoani
Morogoro katika wilaya za Mvomero, Kilombero na Kilosa (na) ndio maana
watanzania wanaona hali ni kama sasa imekuwa shwari,” alisema Matefu.
Matefu alisema wamepata
mualiko rasmi kwa uongozi wa Mkoa wa Iringa na wanatarajia kwenda huko baada ya
uzinduzi rasmi wa taasisi hiyo utakaofanyika Julai 13 jijini Dar es Salaam.
Katibu wa taasisi hiyo,
Mchungaji Oswald Mlay alisema kuwa uzinduzi na utambulisho wa taasisi hiyo
utaendana na utoaji tuzo ya amani kwa viongozi na watu mbalimbali waliojitoa
kuhamasisha udumishwaji wa amani nchini.
Wanaotarajiwa kupewa
tuzo ni Mama Maria Nyerere kwa niaba ya Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere
ambae atatunukiwa tuzo ya AMANI UASISI WA AMANI YA TAIFA.
|
No comments:
Post a Comment