|
Serikali ya Tanzania,
imepanga kupeleka Sh. 18.77 bilioni kila mwezi katika shule za sekondari na
msingi kwa ajili ya kugharamia elimu ili kutekeleza dhana ya elimu bure kuanzia
Januari, 2016.
Taarifa hiyo
ilitolewa Mjini Dodoma jana na Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene wakati akizungumza na
waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa elimu bure.
Alianisha
fedha zitakazotolewa na Serikali kwa ajili ya kugharamia elimu ni pamoja na
gharama za mitihani ya kidato cha nne ambazo zitatolewa moja kwa moja na
Serikali katika Baraza la Mitihani (Necta).
“Serikali
itatoa pia ruzuku ya uendeshaji wa shule Sh. 10,000 kwa shule za msingi na Sh.
25,000 kwa shule za sekondari kwa kila mwanafunzi kwa mwaka.
“Vilevile
itatoa Sh. 1,500 kwa siku kwa mwanafunzi kwa shule za msingi na sekondari kwa ajili ya chakula kwa wanafunzi wanaokaa
bweni,”amesema.
Simbachawene
amesema pia Serikali itatoa fedha kwa ajili ya fidia ya ada Sh. 20,000 kwa kila
mwanafunzi wa shule ya kutwa na Sh. 70,000 kwa mwanafunzi wa sekondari kwa
mwaka.
Amesema
fedha za ruzuku ya uendeshaji wa shule zitasaidia pia uendeshaji wa shule za
hosteli ikiwemo gharama za chakula, mlinzi, mpishi, umeme na maji.
Aliwaagiza
wakurugenzi wa halmashauri husika kuhakikisha fedha hizo zinafika kwa wakati na
zinatumika kwa kazi iliyokusudiwa.
Simbachawene
amesema majukumu ya wazazi pamoja na mambo mengine yatakuwa ni kununua sare za
shule, vifaa vya kujifunzia, gharama za matibabu, nauli, gharama za chakula kwa
wanafunzi wa shule za kutwa na kununua
magodoro, shuka, vifaa vya usafi binafsi kwa wanafunzi wa bweni.
“Natoa wito
kwa viongozi wote wakiwemo wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa
mamlaka za serikali za mitaa kusimamia utekelezaji wa elimu bila malipo,”
amesema.
Aidha,
Simbachawene aliziagiza halmashauri na mikoa ambayo haikufanya vizuri katika
mitihani ya darasa la saba kujieleza sababu za kutofanya vizuri.
“Iwapo
itathibitika kwamba kuna wahusika walizembea kutimiza majukumu yao wachukuliwe
hatua zinazostahili.
“Nawaagiza
pia wakurugezi mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma kwamba ifikapo Februari 15
mwakani wawe wamekamilisha miundombinu ya shule ili wawewezeshe wanafunzi
12,647 waliosalia kujiunga na elimu ya sekondari wanaenda shule,” amesema.
Simbachawene
pia alizitaka kamati za ulinzi na usalama za mikoa na wilaya kuwachukulia hatua
za kisheria watu watakaosababisha wanafunzi kukatisha masomo kwa utoro na mimba
pamoja na wale waliooa watoto wa kike.
‘’Tusifanye
kazi kwa mazoea, tunatakiwa tuendane na kasi ya Rais John Magufuli ya kufanya
kazi kuwasaidia wananchi hasa katika sekta ya elimu,’’ amesema.
Papo kwa Papo >>>> Pata Picha, Habari za Siasa, Kijamii, Biashara, Muziki na Michezo na Nyingine kwa kujiunga na mimi hapa…..FACEBOOK , TWITTER , INSTAGRAM , Pia tutumie tukio la Picha kwa WhatsApp .
|
No comments:
Post a Comment