UCHAGUZI MKUU TANZANIA 2015:- Ngoma nzito majimbo haya…’’ - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Thursday, August 20, 2015

UCHAGUZI MKUU TANZANIA 2015:- Ngoma nzito majimbo haya…’’

Mgombea Urais wa Tanzania  wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli ( kulia) pamoja na mwenzake kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), chini ya mwamvuli wa UKAWA,  Mh.Edward Lowassa,(kushoto).

Said Mwishehe/ JAMBO LEO.

VITA ya wagombea Ubunge kwa sasa inahamia rasmi majimboni baada ya vyama vya siasa nchini Tanzania vinavyoshiriki uchaguzi mkuu ujao wa October 25,2015 kumaliza mchakato wa kuteua wagombea wake.

Hatua hiyo inakuja baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kutangaza kuwa, Agosti 22, mwaka huu 2015 ndiyo siku rasmi ya kuanza kwa kampeni kwa ajili ya uchaguzi huo.

Kutokana na hali hiyo, vita ya kuwania majimbo itaanza rasmi na Watanzania wanasubiri kwa hamu kuona mchuano mkali utakaokuwepo kati ya wagombea wa CCM na UKAWA.

Wakati wakiwa na subira hiyo, CCM imetoa orodha ya majina ya wagombea wake wa ubunge, baada ya kumalizika kwa mchakato wa kura za maoni, ambapo yalipitishwa na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), ya chama hicho.

Pia, majimbo 11 yaliyokuwa yakirudia uchaguzi yamemaliza mchakato wake na majina ya wanaogombea yamepitishwa. 

Kwa upande wa CHADEMA,nayo  imetoa orodha ya wagombea wake wa ubunge katika majimbo mbalimbali nchini.

Orodha hiyo ya CHADEMA inakuja baada ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kumaliza mchakato wa kugawana majimbo hayo.

Kwa hatua hiyo, majimbo kadhaa nchini yanatarajiwa kuwa na vita kubwa ya kuwania ubunge kati ya CCM na UKAWA kutokana na majina ya wagombea kwenye maeneo hayo kuwa maarufu.
Pichani ni Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Bw.John Mnyika .

Miongoni mwa majimbo hayo ni Bukoba Mjini, ambapo CCM imemsimamisha mbunge anayemaliza muda wake, Balozi Khamis Kagasheki, wakati Chadema kwa niaba ya UKAWA imemsimamisha Wilfred Lwakatare.

Jimbo la Mwibara, CCM imemsimamisha Kangi Lugola na Chadema Harun Chiriko, wakati Jimbo la Arusha Mjini, Chadema imemsimamisha Godbless Lema na CCM, Philemon Mollel.

Siasa za Jimbo la Arusha Mjini kwa sehemu kubwa zimewataliwa na wafanyabishara wa madini na ndiyo walikuwa nyuma ya Lema katika uchaguzi mkuu mwaka 2010 na sasa CCM imemsimamisha Mollel ambaye ni mfanyabiashara wa madini.

Vita nyingine ya kuwania ubunge itahamia katika Jimbo la Ukonga, ambapo CCM imemsimamisha Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa wakati Chadema, Mwita Waitara.

Katika uchaguzi mkuu mwaka 2010, Waitara aligombea Jimbo la Tarime, alishindana na mgombea wa CCM, Nyambari Nyangwine ambaye aliibuka kidedea.

Wakati wa Jimbo la Kahama Mjini Chadema imemsimamisha James Lembeli na CCM imemsimamisha Kishimba Kibera

Lembeli kabla ya kujiunga Chadema alikuwa kada wa CCM, lakini alihamia Chadema, hivyo jimbo hilo litakuwa na upinzani mkali.

Jimbo la Ubungo, CCM imemsimamisha Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Massaburi, wakati Chadema imesimamisha mwandishi wa habari maarufu nchini, Said Kubenea.

Jimbo la Kibamba, CCM imemsimamisha Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, wakati Chadema imemsimamisha mbunge anayemaliza muda wake Jimbo la Ubungo, John Mnyika.

Wakati Jimbo la Simanjiro, CCM imemsimamisha Christopher Ole Sendeka na Chadema ikimsimamisha, James Ole Millya

Ole Sendeka na Ole Millya kwa muda mrefu wamekuwa mahasimu wa kisiasa.
Pia, Millya aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Mkoa wa Arusha, lakini alitimkia Chadema mwaka 2010.
Pichani ni Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM,Bw. Nape Nnauye.

Jimbo la Nzega Mjini CCM imemsimamisha Hussein Bashe na Chadema, Charles Mabula.

Bashe licha ya kuwa, CCM wakati wa mchakato wa kumtafuta mgombea urais ndani ya CCM alikuwa mfuasi mwaminifu wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa. 

Baada ya Lowassa jina lake kuenguliwa CCM, alihamia Chadema ambako anagombea urais.

Hivyo, jimbo hilo litakuwa na upinzani mkali maana CCM haitakuwa tayari kuona likipotea kwani, Chadema inataka kuonesha uwezo wake wa kukubalika kwa wananchi.

Jimbo lingine ambalo litakuwa na upinzani mkali ni Sikonge, ambapo CCM imemsimamisha George Kakunda na Chadema, Said Nkumba.

Wakati wa mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM, Nkumba alikuwa chama hicho, lakini baada ya kushindwa alihamia Chadema na jina lake limepitishwa kugombea. Kwa sasa Nkumba anamalizia ubunge wake katika jimbo hilo.

Vita nyingine itakuwa katika Jimbo la Moshi Mjini, ambako CCM imemsimamisha Davis Mosha, ambaye mfanyabishara maarufu na aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Yanga SC, atapambana na mgombea wa Chadema, Jafary Michael.

Kwa upande wa Jimbo la Nyamagana, CCM imemsimamisha Stanslaus Mabula ambaye ni Meya wa Jiji la Mwanza, wakati Chadema imemsimamisha mbunge anayemaliza muda wake, Ezekia Wenje.

Siasa za Nyamagana kwa sehemu kubwa zinatawaliwa na nguvu ya vijana na wagombea hao wana ushawishi mkubwa kwa vijana.

Katika Jimbo la Muleba Kaskazini, CCM imemsimamisha Naibu Waziri wa Nishati na Madini anayeshughulikia Nishati, Charles Mwijage, wakati Chadema imemsimamisha mwandishi maarufu, Ansbert Ngurumo.

Wakati wa mchakato wa kura za maoni ndani ya Chadema, Ngurumo alishindwa.

Hata hivyo, Mwijage na Ngurumo wamemekuwa na upinzani mkubwa kisiasa.

Jimbo la Muleba Kusini, CCM imemsimamisha mbunge anayemaliza muda wake, Profesa Anna Tibaijuka na Chadema Alistides Kashasila

Prof.Tibaijuka amekuwa na upinzani mkali katika baadhi ya maeneo ya jimbo hilo, hasa Kata ya Nshamba.

Wakati Jimbo la Iringa Mjini, CCM imemsimamisha Fredrick Mwakalebela na Chadema Mchungaji Peter Msigwa

Uchaguzi mkuu mwaka 2010, CCM ililiengua jina la Mwakalebela, hali iliyosababisha wana-CCM kukasirika na kupeleka kura zao kwa Msigwa.

Katika uchaguzi wa mwaka huu 2015, Mwakalebela na Msigwa wanapambana na hivyo, ushindani wake unatabiriwa kuwa, mkubwa. 

Kwa upande wa Jimbo la Lupa, CCM inawakilishwa na Victor Mwambalaswa na Chadema, Njelu Kasaka.

Kabla ya kujiunga Chadema, Kasaka alikuwa kada wa CCM.

Jimbo la Bunda Mjini, CCM imemsimamisha Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira na Chadema, Ester Bulaya, ambaye kabla ya kujiunga chama hicho, alikuwa CCM.

Bulaya wakati wa mchakato wa kura ya maoni ndani ya Chadema hakufanikiwa kushinda, lakini jina lake limepitishwa na chama chake.

Kwa upande wa Jimbo la Monduli, CCM imemsimamisha Namelock Sokoine, ambaye alikuwa mbunge wa viti maalumu Mkoa wa Arusha na Chadema, Julius Kalanga

Jimbo la Monduli ndilo analotoka mgombea urais kupitia Chadema/Ukawa, Edward Lowassa.

Wakati akiwa CCM, Lowassa alimtambulisha Sokoine katika maeneo mbalimbali kama mrithi wake, baada ya yeye kustaafu ubunge, hivyo ni jimbo ambalo uchaguzi wake unasubiriwa kwa hamu.


PAPO KWA PAPO Pata Picha, Habari za  Siasa, Kijamii, Biashara, Muziki na Michezo na Nyingine kwa kujiunga  na mimi hapa…..FACEBOOK , TWITTER , INSTAGRAM , Pia tutumie tukio la Picha kwa WhatsApp  +255789925630.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad